Na.
Immaculate Makilika -MAELEZO
Serikali ya Awamu ya
Tano yafanikiwa kuleta mabadiliko ya kiutendaji yaliyosaidia kuongeza ufanisi
katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza leo jijini
Dodoma, kwenye kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binandamu,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, George
Mkuchika alisema “Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, inasimamia kikamilifu maadili katika utumishi wa umma, na katika
kipindi cha miaka minne tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika utumishi wa umma.”
Aliongeza “kiwango cha uadilifu katika
utumishi wa umma kimeongezeka kwa kiasi kukubwa. Hivyo, ninapenda kutumia
nafasi hii kuwapongeza watumishi wote ambao wameitikia wito wa Serikali wa
kuzingatia maadili katika utumishi wa umma”
Waziri Mkuchika,
alibainisha juhudi mbalimbali ambazo Serikali imezichukua katika kuhakikisha
utumishi wa umma unazingatia maadili, ikiwa ni pamoja na kutunga sheria
mbalimbali zinazosimamia wa utendaji katika Utumishi wa Umma kama vile Sheria
Na. 13 ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, Kanuni za Kudumu za
Utumishi wa Umma, Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma, na miongozo mingine ya
kiutumishi ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara.
Adha, jitihada nyingine
za Serikali ni maboresho katika programu mbalimbali, pamoja na kuimarisha
uadilifu katika sekta ya umma, kwa kutekeleza Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa
na Mpangokazi wake, ambapo taasisi zote za umma zinapaswa kuwa na Kamati za
Kusimamia Uadilifu.
Vilevile, Waziri
Mkuchika amewataka viongozi wote katika utumishi wa umma kusimamia sheria,
kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi ili kutekeleza azma ya Serikali ya
kuboresha utumishi wa umma kuwawezesha wananchi kupatiwa huduma bora na bila
usumbufu wa aina yoyote.
Ambapo, alisisitiza
kuwa Rais Magufuli, amekuwa kila mara
akionesha kutokuvumilia watendaji wabovu
Serikalini, na wananchi
wameonyesha kufurahishwa na juhudi na msimamo wa Rais pamoja na Serikali yake
katika kusimamia maadili katika utumishi wa umma. Umakini na uharaka wa
Serikali katika kuchukua hatua dhidi wa watumishi wasiozingatia maadili sio tu
umeongeza ufanisi kazini bali pia umeongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa,
alisema kuwa watumishi wa umma wanatakiwa kukemea mambo mabaya na kuwa mfano
bora kwa wengine.
Naye, Kamishna wa Maadili,
Jaji Mstaafu Harold Nsekela, aliipongeza Serikali kwa kufanya maadhimisho ya
maadili na haki za binaadamu nchini kwa vile yanatoa fursa kwa vongozi na
watumishi wa umma kujitathimini.
“Naishukuru Serikali
kwa kuona umuhimu wa kuheshimu mikataba ya Kimataifa na kuiridhia, kwani
maadhimisho haya ni muhimu yanatoa fursa ya kujitathimini kama taifa limefanya
jitihada za kutosha za kupambana na rushwa, kuzingatia misingi ya utawala bora,
maadili na haki za binaadamu”.
Kongamano la
Maadhimisho Siku ya Maadili na Haki za Binandamu, limefikia kilele leo, likiwa
na kauli mbiu inayosema maadili katika Utumishi wa Umma ni nguzo muhimu katika
kuimarisha Utawala bora na Haki za binadamu, limehudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa utumishi wa umma pamoja na watumishi wa umma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...