RAIS
Dkt. John Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza Nchini kutathimini utendaji kazi
wake kutokana na mwenendo usioridhisha wa jeshi hilo katika kutekeleza miradi
mbalimbali inayopewa na Serikali.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa Nyumba za Makazi ya Maafisa na Askari wa Jeshi
hilo, leo (Alhamisi Januari 23, 2020) Ukonga Jijini Dar es Salaam, Rais
Magufuli alisema ameshangazwa na kasi isiyoridhisha ya utekelezaji wa miradi
katika jeshi hilo licha ya kuwa na ukubwa wa kambi 129 nchini.
Akitolea
mfano Rais Magufuli alisema Jeshi la Magereza lina jumla ya kambi 129 huku Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) likiwa na kambi 24 tu, lakini ameshangazwa na Magereza kujengewa
nyumba za askari wake na JKT huku akishindwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa
walionao katika magereza mbalimbali nchini.
‘’Baada
ya kutoa msamaha wa wafungwa zaidi ya 5000, sasa hivi katika magereza yote
nchini kuna zaidi ya wafungwa 13,000 lakini tunashindwa kujenga nyumba za
askari wetu, udongo kutoka kwa mungu tunao, hamna budi kujipanga na kuweka
mikakati ili kuimarisha makazi ya askari ambao wanateseka’’ alisema Rais
Magufuli.
Alisema
mwezi Machi 2016 Serikali ilitoa kiasi cha Tsh Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi
wa nyumba za askari magereza katika eneo la Ukonga Jijini Dar es Salaam na
kutoa zabuni hiyo kwa Jeshi hilo pamoja na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),
ambapo pamoja kutumia miezi 27 walishindwa kuikamilisha kazi hiyo kwa kufikia
asimilia 40-45 ya ujenzi wake.
Akifafanua
zaidi alisema kutokana na kutoridhishwa na kasi hiyo, Serikali iliamua kuipa
zabuni ya ujenzi wa mradi huo huo, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo ndani ya
kipindi cha miezi 6 kuanzia mwezi Machi hadi Desemba mwaka 2019 ilikamilisha
asilimia 55 ya ujenzi mradi huo kwa kutumia kiasi cha Tsh Bilioni 3 na kufanya
mradi wote kutumia Tsh Bilioni 13.
Alibainisha
kuwa ipo baadhi ya miradi mikubwa inayosuasua kutekelezwa na Jeshi hilo, ikiwemo
Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha Viatu katika Gereza la Karanga unaojengwa kwa
ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Jeshi
la Magereza Nchini, ambao hadi sasa ujenzi wake hauridhishi kwani hakuna hata
jengo moja lililokamilika hadi sasa.
‘’Mashine
za kiwanda kile tayari zimewasili katika Bandari ya Dar es Salaam, lakini hadi
sasa ni jengo moja tu lililofikia asilimia 49 ya ujenzi ndilo limesimama, sasa
hizo mashine zitaenda kufungwa wapi, Mkataba wa Bilioni 9 umesainiwa, na ni
mradi wenye ubia, kwa nini tunakwama’’ alisema Rais Magufuli.
Aidha
Rais Magufuli aliipongeza JKT kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanya katika
kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa nchini ikiwemo ujenzi wa ukuta wa
Mererani, Ujenzi wa Mji wa Serikali Dodoma na Ukuta wa Ikulu Dodoma wenye urefu
wa Kilometa 27, na kulitaka Jeshi la Magereza kuiga mfano huo katika kujenga na
kuboresha nyumba za makazi ya askari wa Jeshi hilo.
Kwa
upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi
alisema Wizara yake inatambua juhudi kubwa zinazofanywa Rais Dkt. John Magufuli
katika kuimarisha na kuboresha maslahi ya Maafisa na Askari wa Majeshi ya
Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi ya
askari.
Waziri
Mwinyi alisema katika Makazi hayo, yenye jumla ya ghorofa 12 zikiwemo ghorofa 8
za makazi askari na ghorofa 4 za makazi ya maafisa, zina jumla ya nyumba 172
zenye uwezo wa kutunza familia za maafisa na askari wa vikosi vya majeshi ya
ulinzi na usalama.
Naye
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisema Wizara hiyo itaendelea
kuhakikisha kuwa suala la ulinzi na usalama wa nchi linaendelea kusimamiwa kwa
nguvu zote nchini kupitia vyombo vya dola ili kuwawezesha wananchi kushiriki
kikamlifu katika shughuli za maendeleo.
Nyumba za Maafisa na Askari Magereza zilizofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwenye sherehe ya kukabidhi nyumba hizo kwa Jeshi la Magereza leo
Alhamisi Januari 23, 2020
Alhamisi Januari 23, 2020
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...