
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Dkt. Mohamed Mohamed akifungua mafunzo ya siku moja kwa wataalam tarajali yaliyofanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala MNH-Mloganzila Bi. Njoikiki Mapunda akizungumza wakati wa mafunzo elekezi kwa tarajali 19 ambapo amewataka mafunzo wanayopewa yawe na manufaa kwao kwa kuwaongezea utii na uadilifu

Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Heavenlight Majule akiwasilisha mada kuhusu udhibiti wa rushwa mahala pa kazi.

Afisa Maadili kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Hamadi Bakari akiwasilisha mada ya maadili ya Utumishi wa Umma kwa wataalam tarajali.

Wataalam tarajali wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mafunzo hayo katika Hospitali ya MNH-Mloganzila.
Wataalam tarajali wa kada mbalimbali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wamepatiwa mafunzo elekezi lengo ikiwa ni kuwaelekeza maadili mema ya utumishi wa umma mahala pa kazi
Akitoa mada katika mafunzo hayo Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Heavenlight Majule amesema maadili mema ndio msingi utakaowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
“Ukosefu wa maadili mahala pa kazi umepelekea haki za watu kupotea kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa ambavyo vimepelekea watoa huduma kutoa huduma zilizo chini ya viwango” amesema Bi. Majule.
Aidha ametaja vyanzo mbalimbali vya mmomonyoko wa maadili ambavyo vinaathiri mienendo ya watumishi wa uuma kuwa ni pamoja na tamaa yaani kutoridhika na kile wanachokipata kwa mwajiri, ubinafsi, muundo wa maisha na aina ya marafiki.
Kwa upande wake Afisa Maadili kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Hamadi Bakari amesisitiza kuwa maadili mema ni pamoja na kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, bidii ya kazi, huduma bila upendeleo, uadilifu, uwajibikaji, kuheshimu matakwa ya sheria pamoja na matumizi sahihi ya taarifa.
“Maadili mema ni kufanya kilicho sahihi ambapo imeainisha katika kanuni ya 65 ya maadili ya utendaji katika utumishi wa Umma ya marekebisho ya mwaka 2005 inayoelezea sifa za mtumishi mwadilifu” amesema Bw. Bakari.
Awali akizungumza na tarajali hao Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya MNH-Mloganzila Dkt. Mohamed Mohamed amewasisitiza wataalam tarajali kuwa mafunzo wanayopatiwa hospitalini hapa yawasaidi katika kufanya kazi kwa utii na uadilifu.
Mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na elimu elekezi ya kuzuia na kupambana na rushwa mahali pa kazi, huduma mbalimbali zinazotolewa hospitalini hapa, mafunzo ya masuala ya ukimwi mahala pa kazi, maadili ya utumishi wa umma na kanuni za kazi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...