Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imeuagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufanya mapitio ya tathimini ili kuzifuta Jumuiya za Maji ambazo zimeshindwa kuhudumia wananchi.

Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso wakati akizungumza na mameneja Ruwasa wa Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania bara katika mkutano wa mrejesho wa uhakiki na tathimini ya utekelezaji wa mpango wa malipo kwa matokeo awamu ya nne.

Mhe Aweso amesema kumekuepo na changamoto ya usimamizi na uendashaji wa miradi ya maji katika halmashauri nyingi nchini na hiyo inatokana na Jumuiya zinazoendesha miradi hiyo kukosa taaluma ya maji.

" Mkurugenzi wa Ruwasa nikuagize uanze kufuatilia hizi Jumuiya ambazo zinaendesha miradi ya maji nchini kwa sababu nyingi zimekosa sifa ya kusimamia miradi yetu na haina wataalamu ambao wanaweza kutengeneza hata koki," Amesema Waziri Aweso.

Aidha amesema changamoto nyingine inayowakabili watu wa vijijini ni ukubwa bei za maji kulinganisha na maeneo ya Mijini huku akitolea mfano 'Unit' Moja inayouzwa jijini Dar es Salaam kwa Sh 1800 kwa vijijini itauzwa Sh 5,000.

" Ndugu zangu azma ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli imedhamiria kumtua ndoo mwanamke ukubwa wa bei ya maji kwenye maeneo ya vijijini kunazidisha ugumu kwa wananchi badala ya kuwapunguzia kero.

Ruwasa mnapaswa kuzingatia bei ya maji, lengo letu ni kuwe na usawa na unafuu kwa wananchi wetu wote wa mjini na vijijini. Pamoja na kuwepo kwa gharama za uendeshaji wa miradi lakini mnapaswa mtambue kuwa serikali haina nia ya kuumiza wananchi wake bali kuwahudumia," Amesema Mhe Aweso.

Mhe Waziri amewataka wahandisi hao kuhakikisha miradi 153 ambayo inagharimu kiasi cha Sh Bilioni 66 inakamilika haraka kwani kwa kipindi kirefu imekua ikisuasua.

Awali akisoma taarifa hiyo Mkurugenzi wa Ruhasa, Clement Kivegalo amesema serikali inashirikiana na washirika wake wa maendeleo katika kutekeleza programu ya maendeleo ya sekta ya maji ambapo kwa sasa utekelezaji wake upo kwenye awamu ya pili ilyoanza mwezi Julai 2016.

Amesema utekelezaji wa awamu ya pili umejikita katika vipaumbele vilivyoanza kutekelezwa katika awamu ya kwanza ikiwa ni pamoja na kurekebisha mapungufu ya awali.

" Mojawapo ya mapungufu yaliyojitokeza katika awamu ya kwanza ni uendelevu wa miradi kutokana na mkazo mdogo katika usimamizi wa huduma na matengezo ya miundombinu na hasa kwenye maeneo ya vijijini.

Katika juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo serikali na wadau tulibuni programu wezeshi kadhaa za kuimarisha uendelevu wa miradi na huduma. Mojawapo ya programu hiyo ni ya malipo kwa matokeo ambayo inatekelezwa Nchi nzima chini ya ufadhili wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID)," Amesema Kivegalo.

Amesema programu hiyo imetengewa jumla ya Paundi Milioni 65 sawa na Sh Bilioni 194.5 fedha hizo zikiwa ni sehemu ya Paundi Milioni 154 za DFID ikiwa ni mchango wake katika utekelezaji wa awamu hiyo ya maji.

" Fedha hiyo ndiyo inayotumika sasa chini ya mpango wa PbR ambayo ni Paundi Milioni 65 ambapo matumizi yake yatafikia ukomo Machi 2020 na hadi sasa tushatumia Paundi Milioni 36 ikiwa ni ndani ya miaka mitatu, " Amesema Kivegalo.

 Naibu Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso akizungumza katika mkutano wa pamoja na Mameneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) jijini Dodoma leo.
 Mwakilishi wa Serikali ya Uingereza ambayo taasisi zake ikiwemo DFID zinashirikiana na serikali ya Tanzania katika maendeleo ya sekta ya maji akizungumza katika mkutano wa pamoja wa Naibu Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso na Mameneja wa RUWASA wa Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania bara leo jijini Dodoma.
 Mameneja wa Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania bara pamoja na wadau mbalimbali wakiwa kwenye mkutano na Naibu Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso jijini Dodoma leo.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (katikati) akifuatilia mkutano wake na Mameneja wa RUWASA wa Mikoa yote ya Tanzania bara leo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof Kitila Mkumbo na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...