Na Said Mwisehe,Michuzi Blogu ya jamii
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo limebaini kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Bara Philip Mangulla mwili wake umekutwa na sumu.
Akizungumza leo Machi 9,2020 jijini Dar es Salaam ,Kamanda Mambosasa amewaambia waandishi wa habari kuwa jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja taasisi nyingine lomebaini kuwa mzee Mangulla ndani ya mwili wake kulikuwa na sumu na kwamba ni jinsi gani sumu hiyo imeingia mwilini ,uchunguzi bado unaendelea kufanyika.
"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam litachukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayebainika kupanga ,kuratibu na kutekeleza uhalifu huo awe ni mwana familia, kutoka ndani ya Chama, nje ya chama, ndani ya nchi au nje ya nchi au awe Serikalini au chama chochote cha siasa,"amesema na kuwa Machi 2, 2020, Polisi walipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa CCM ya kuwekewa sumu mzee Philip Mangula.
Kamanda Mambosasa amefafanua Februari 28, mwaka huu Mangula aliaguka ghafla katika ofisi ndogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM ) zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyokuwa ikijadili mambo mbalimbali ya Chama.
Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yanajadiliwa ni pamoja na adhabu ya wanachama watatu waliokuwa wanatuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa maadili ndani ya chama hicho. Wanachama hao ni Katibu Mkuu mstaafu Yusuph Makamba,Katibu Mkuu mstaafu Abdulrahman Kinana pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe.
Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa amesema kuwa katika taarifa hiyo walielezwa kwamba Mangula alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baada ya kufika alilazwa chumba cha uangalizi wa karibu (ICU).
Mbali na taarifa ya Mangulla kuwekewa sumu, Kamanda Mambosasa amesema pia Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kumkamata jambazi sugu Boniface Nikodemasi (37) mkazi wa Vikindu akiwa na silaha ya kivita aina ya AK 47 yenye namba 1952TPB3954 ikiwa na risassi tatu ndani ya Magazine.
Ameeleza kuwa Machi 7, mwaka huu saa tano kamili asubuhi maeneo ya Majoe Pugu alikamatwa mtuhumiwa huyo na kwenda kuwaonesha askari alipoficha silaha hiyo maeneo ya Vianzi Mkoa wa Kipolisi Rufiji."Mtuhumiwa huyo amekuwa akituhumia silaha hiyo kufanya uhalifu maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Pwani."
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...