Tunapoadhimisha kumbukumbu ya siku ya Mwanamke Duniani hii leo Machi 8, 2020 ikiwa ni miaka 25 tangu wanawake kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wakutane jijini Beijing, China kujadili maendeleo ya wanawake,Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inapenda kuungana na Watanzania wote katika kusherehekea maadhimisho haya ambayo kimsingi yanatoa fursa kwa wanawake kufanya marejeo ya hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kuboresha mustakabali wa wanawake nchini.

Tume inatambua kuwa, Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa imeridhia mikataba ya haki za binadamu kuhusu wanawake ikiwemo makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa beijing mwaka 1995.

Miongoni mwa maeneo ambayo Serikali imeyafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa wakati tunaadhimisha siku ya mwanamke mwaka huu ni pamoja na usawa wa kijinsia katika kushiriki kwenye kufanya maamuzi, upatikanaji wa huduma za afya kwa mama na mtoto, kukemea ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike na kuwajengea mifumo ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosema “kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania kwa sasa na baadae”. Serikali imepiga hatua kubwa na mpaka sasa tunashuhudia kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Tume inatumia fursa hii kupongeza kwa dhati jitihada za Serikali katika kujenga mifumo sahihi kwa mwanamke kujiletea maendeleo yake.

Aidha, katika kuyapa kipaumbele masuala ya wanawake Tume inaendelea kutekeleza Mpango Kazi wake wa Miaka Mitano (2018/ 2023) ambapo moja ya malengo yake ni kuhakikisha wanawake wanaweza kufikia mifumo ya kupata haki kwa urahisi zaidi.

Licha ya juhudi za Serikali na Wadau za kahakikisha haki za wanawake zinapatikana kwa usawa na watu wengine, bado kuna changamoto ya ukatili kwa wanawake na kutokuwateuwa kwa wingi kugombea nafasi za kisiasa. Hivyo, Tume inatoa mapendekezo kwa Serikali, Wadau na jamii kwa ujumla kama ifuatavyo;

Tume inaiomba Serikali iendelee kuweka mazingira mazuri kwa wanawake kwa kuwaongezea nafasi zaidi katika ngazi za maamuzi ili kuweza kufikia maendeleo ya kweli ifikapo mwaka 2025.

Tume inazishauri mamlaka za umma na binafsi kuongeza juhudi za kuelimisha jamii kuhusu kuachana na mila zote potofu dhidi ya mwanamke ili kumpa fursa nzuri ya kuweza kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Tume inashauri vyombo vinavyosimamia upatikanaji wa haki hususan Mahakama na jeshi la Polisi kuimarisha na kuongeza kasi ya ushughulikiaji wa mashauri yanawayohusu wanawake.

Tume inaishauri Serikali pamoja na wadau wa haki za binadamu kupitia sheria zote zinazowagusa wanawake ikiwemo sheria za kimila kwa madhumuni ya kuzifuta, au kuzirekebisha ili ziendane na Katiba ya Nchi, Azimio la Beijing na mikataba mbalimbali ya kimataifa na ya kikanda.

Tume inawatakia Wanawake Maadhimisho mema.

Imetolewa na:


(SIGNED)

Jaji (Mst.) Mathew P. M. Mwaimu
MWENYEKITI

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Machi 8, 2020

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...