Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Singida, Aran Jumbe akizungumza mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho ngazi ya mkoa muda mfupi kabla ya kujiuzulu nafasi yake.
Mwenyekiti mpya wa chama hicho Mkoa wa Singida, Hamis Mtundua akizungumza baada ya kuchaguliwa.
Mtundua akijaza fomu maalamu ya uongozi. Kushoto ni Afisa Kazi Mkoa wa Singida, Boniface Ntalula.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT ngazi ya mkoa wakifuatilia uchaguzi huo.
Mwenyekiti mpya wa Kitengo cha Wanawake (KE) Mkoa, Beatries Mbao akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi akiwasili kwa ajili ya kufungua mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi akihutubia wajumbe wa mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi, akionesha fulana na kofia kea zilizoandaliwa na chama hicho kama vazi rasmi la Maadhimisho ya Sherehe ya Mei Mosi mwaka 2020.
Wajumbe wa mkutano huo wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa uchaguzi ngazi ya mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri akizungumza katika mkutano huo.


Na Godwin Myovela

MWENYEKITI maarufu wa Chama cha Walimu nchini (CWT), mkoani hapa, Aran Jumbe, ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo, na badala yake Mkutano Mkuu wa chama hicho ngazi ya mkoa umemchagua aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Singida mjini (Manispaa), Hamis Mtundua kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.

Sambamba na hilo kupitia mkutano huo mkuu wa kikatiba, wanachama wa chama hicho walipokea taarifa ya kusudio la kustaafu kwa kigezo cha ukomo wa utumishi wa umma kwa aliyekuwa Katibu wa CWT mkoani hapa, Joseph Nehemia kuanzia mapema mwezi ujao.

Akizungumza wakati akiwaaga Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mkoa, mkoani hapa juzi, Jumbe alisema akiwa na akili timamu na bila kushinikizwa na mtu yeyote ameamua kutogombea tena nafasi hiyo, kwanza; ni kutokana na sababu ya demokrasia, pia amebakiza muda mfupi wa kustaafu, na zaidi anakabiliwa tatizo la kiafya linalomlazimu apumzike baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.

“Nawashukuru walimu wote, serikali na hasa kipekee Mkuu wa Mkoa wa Singida (Mwalimu Nchimbi)na wadau wote wa elimu kwa ushirikiano mkubwa mlionipatia kwa kipindi chote cha uongozi wangu katika kufanikisha malengo na mikakati ya chama chetu hususani kwenye eneo la upatikanaji wa maslahi na stahiki za walimu,” alisema.

Jumbe kutokana na mvuto wa kipekee alionao kwa takribani kipindi chake chote cha miaka kumi alichohudumu, wengi hupenda kumpambanua kama mtu jasiri, mahiri, asiye na makuu, mwenye ushirikiano wakati wote, mwenye msimamo kwa maslahi ya walimu, na asiyependa njia za mkato.

“Nimsihi mwenyekiti wangu wa sasa (Mtundua) na viongozi wote walio chini yake waendelee kudumisha umoja na mshikamano uliopo, wazingatie miiko na maadili katika kupokea na kutatua kero za wanachama, na wahakikishe wanatekeleza masuala yote kwa kuzingatia kanuni, miongozo na katiba ya CWT iliyopo- tena kwa mipaka waliyonayo,” alisisitiza Jumbe.

Pia aliwataka viongozi wote wateule ndani ya chama hicho kuhakikisha wanashirikiana ipasavyo na serikali katika kutafuta njia bora, mathalani mabaraza ya kisekta katika kufikia haki zote stahiki na maslahi ya walimu, kuchapa kazi, na kuunga mkono kwa vitendo Ilani ya chama Tawala chini
ya Jemedari na kipenzi cha walimu wote nchini, Rais John Magufuli.

“Rais Magufuli ni msikivu, anajali sana maslahi ya walimu,ni mwalimu mwenzetu, na anatupenda sana walimu, ndio maana tangu aingie madarakani hatujawahi kugoma. Bila shaka wala kigugumizi Magufuli ni wetu na tunamuunga mkono kwa uongozi wake uliotukuka …hapa tunasubiri tu mda wa kupiga kura ufike ili tumrudishe tena,” alisema Jumbe.

Awali, akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi, alipongeza umahiri mkubwa wa kiutendaji na ufanisi unaofanywa na CWT ya kipindi cha sasa kwa kushirikiana na serikali katika kutafuta stahiki mbalimbali za walimu kote nchini.

“Nawasihi walimu wenzangu kwa umoja wetu tushikamane, tuendelee kumuombea na kumuunga mkono Rais wetu mpendwa, ili kwa uwezo wa Mungu azidi kufanya mambo makubwa zaidi na zaidi kwa ustawi wa walimu wote nchini na taifa kwa ujumla…tumpe nafasi,anastahili,” alisema Nchimbi

Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Afisa Kazi mkoani hapa Boniface Ntalula, viongozi wengine waliochaguliwa kwa ngazi ya mkoa ni pamoja na Mwekahazina (Didas Mwekwa), Mwenyekiti wa
Kitengo cha Wanawake “KE” (Beatrice  Mbao), na Mwakilishi Vijana (John Sebastian).

Wengine ni KUT-Taifa (Aminiel Mfinanga), Mwakilishi Walimu wenye Ulemavu ‘VU’ (Benjamin Mayengela), Mjumbe Kamati Tendaji ndani ya TUCTATaifa (Didas Mwekwa), na Mwakilishi wa Kitengo cha Wanawake ‘KE’ ngazi ya mkoa (Mary Ndele).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...