Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo ambao ni wadau wa
kilimo, ukarimu na utalii wakifuatilia mada wakati wa warsha hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, akizungumza
wakati wa ufunguzi rasmi wa warsha hiyo.
Mratibu wa Programu ya Uwanagenzi Pacha VETA, Ndugu
Francis Komba, akisisitiza jambo kwa washiriki wakati akiwasilisha mada juu ya
wajibu wa wadau hao katika kufanikisha utoaji mafunzo kwenye sekta hizo.
Washiriki wa warsha wakiwa katika picha ya pamoja na
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu (katikati). Kulia kwake ni
Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Bi. Stella Ndimubenya na Mkuu wa
Chuo cha VETA Manyara Ndugu Felix Ole Ndukai. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa
VETA Kanda ya Kati Ndugu John Mwanja na Balozi wa programu ya Uanagenzi Pacha
na Mkulima wa mjini Babati Ndugu Jitu Son.
Mmoja wa washiriki akichangia mada wakati wa warsha hiyo.
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendesha
warsha kati yake na wadau wa sekta za Kilimo na Ukarimu na Utalii na kuweka
mikakati ya kuzalisha wataalam mahiri wa sekta hizo kupitia programu ya Uanagenzi
Pacha (Dual Apprenticeship Training System, DATS.)
Akifungua warsha ya wadau hao katika chuo cha VETA Manyara
Desemba 30, 2020, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa
mafunzo kupitia programu hiyo yanamwezesha kijana kupata ujuzi wa fani husika
akiwa chuoni na sehemu ya kazi, hivyo kumwezesha kwa kiasi kikubwa kujifunza
kwa vitendo na kuendana na mahitaji ya soko la ajira pamoja na kupata uzoefu na
uelewa wa mazingira halisi ya kufanyia kazi.
Amesema wadau hao wana mchango mkubwa sana katika
kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa kwa ufanisi na kuzalisha
nguvukazi mahiri itakayochangia kuongeza tija na uzalishaji kwenye sekta hizo.
“VETA inatambua umuhimu wa kushirikiana na waajiri
kwenye sekta mbalimbali kutoa mafunzo kwa kuwa ushirikiano huo unawezesha
kuandaa nguvu kazi mahiri zaidi inayoendana na mahitaji halisi ya viwanda hasa
kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya mafunzo hayo yanafanyika sehemu za kazi,”amesema.
Kwa mujibu wa Dkt Bujulu,programu hiyo imeendelea
kufanya vizuri tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012 kwa ushirikiano na Hamburg Chamber of Craft (HWK) ya Ujerumani ambapo jumla ya
wanagenzi 448 wamefuzu mafunzo hayo kwenye fani za Ukarimu na Utalii, Ufundi
Umeme, Ufundi Magari, Ujenzi, na Ufundi wa zana za kilimo.
Dkt. Bujulu amewataka wadau hao kushiriki kikamilifu
katika utekelezaji wa programu hiyo ili kuweza kuandaa wafanyakazi wenye
viwango wanaohitajika katika kuleta mapinduzi katika sekta hizo.
Mkurugenzi wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi Bi. Stella Ndimubenya amesema warsha hiyo imelenga kuwajengea
uwezo wasimamizi wa mafunzo hayo viwandani, juu ya namna bora ya kutekeleza
programu hiyo, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zitokanazo na
utekelezaji wake.
Mratibu wa programu hiyo Ndugu. Francis Komba amesema
kuwa VETA imeamua kutoa mafunzo ya Uanagenzi pacha katika sekta hizo baada ya
tafiti za soko la ajira kufanyika katika mikoa mbalimbali na kubaini mahitaji
makubwa ya wataalamu wa hoteli na utalii pamoja na ufundi wa zana za kilimo kwa
ngazi ya ufundi stadi.
Balozi wa programu ya Uanagenzi pacha na Mkulima wa
mjini Babati Ndugu Jitu Son ameishauri VETA kupanua wigo wa utoaji mafunzo ya
ufundi stadi kupitia programu hiyo na kuwezesha vyuo vingi zaidi kutumia
programu hiyo yenye manufaa makubwa kwa wanagenzi na waajiri.
Mmoja wa wasimamizi
wa programu hiyo ya Uanagenzi Pacha kutoka Moivaro Lodges, Serengeti Ndugu Musa
Elphas amesema kuwa mfumo huo wa mafunzo umesaidia wenye hoteli kupata
wafanyakazi bora zaidi kwa kuwa wenye hoteli wanapata fursa ya kushiriki kuwandaa
wakati wa mafunzo.
Naye msimamizi wa wanagenzi pacha kutoka TPC Ndugu
Boniface Mwambaya amesema kuwa kiwanda chake kimefaidika na mafunzo hayo kwa
kuwapata wanagenzi wanaofanya kazi kwa weledi na umakini.
Mmoja wa wanufaika wa programu hiyo katika fani ya
Ukarimuna Utalii Ndugu Azizi Ally amesema programu hiyo imemsaidia kupata ujuzi
kwenye eneo la hoteli na kufanikiwa kujiajiri ambapo kwa sasa anamiliki Mgahawa
wake na amefanikiwa kuajiri vijana wenzake wanne na hata sasa ameamua kupeleka
vijana wawili kujiunga na mafuzo hayo kama mchango wake kwa jamii na kuwataka
waajiri wenzake kuona umuhimu wa kuendelea kushiriki kutoa mafunzo hayo ya
uwanagenzi pacha.
Mfumo wa utoaji mafunzo ya Uanagenzi pacha unahusisha kuhudhuria mafunzo ya vitendo kwenye karakana na darasani (VETA) na kufanya vitendo zaidi katika sehemu za kazi. Mafunzo hayo ni ya miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka mwanagenzi anatumia wiki 20 VETA na wiki 32 kwa mafunzo ya viwandani.
Mfumo wa mafunzo ya
Uanagenzi Pacha ulianzishwa mwaka 2011/12 kwa ushirikiano kati ya VETA na Hamburg Chamber of Crafts (HWK) ya Ujerumani,
ambapo kwa sasa unatekelezwa katika vyuo vinne vya VETA vya Moshi RVTSC
(Ukarimu na Utalii), Dar es Salaam RVTSC (Ufundi Umeme na Ufundi Magari), Simanjiro
DVTC (Uashi) na Manyara RVTSC (Ufundi wa Zana za Kilimo). Viwanda na kampuni
zaidi ya 150 zimenufaika na mafunzo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...