Na Muhidin Amri,Mbinga
ZAIDI ya wakulima 4000 kutoka vijiji mbalimbali katika Halmashauri ya
Mbinga mkoani Ruvuma, wamepatiwa msaada wa mbegu bora za mahindi
zitakazowasaidia kuongeza uzalishaji na kukuza vipato vyao.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa mbegu hizo Kaimu Afisa kilimo
wa Halmashauri Deodatus Kisima alisema, mchakato wa mpango huo umetokana
na maombi ya uhitaji wa mbegu kutoka serikali kuu kupitia serikali ya
mkoa ambapo awali walikubaliwa kupata tani 4.
Kwa mujibu wa Kisima,kutokana na mahitaji makubwa ya wakulima katika
Halmashauri hiyo Serikali ikaona ni vyema kuwaongezea hadi kufikia
tani 8,hata hivyo katika hatua ya mwisho ya Utekelezaji wa mpango huo
Halmashauri ilifanikiwa kupata tani 11 ambazo ni sawa na kilo 11,000 za
mbegu ya mahindi zenye thamani ya shilingi milioni 77.
Kisima alisema, katika mpango huo kila mkulima atapata kilo 2 hadi 4 ya
mbegu aina ya ni DK 90-89 ambazo zinafaa kwa mazingira ya ukuaji wa
zao ma mahindi katika Halmashauri hiyo.
Alisema,uteuzi wa wakulima ulifanywa na maafisa watendaji wa maeneo
yaliyolengwa kupata mbegu kwa ajili ya kilimo cha mahindi ambapo maeneo
yaliyolengwa na kupatiwa mbegu hizi ni vijiji vya kata ya AmaniMakolo,Mkako,Namswea,Muungano,Matiri,Muhongozi,Kitumbalomo,Kigonsera,Kihangimahuka na Lukarasi.
Alisema, katika kuhakikisha kuwa zoezi linatekelezwa kwa
ufanisi,Halmashauri imeorodhesha na kupata wakulima ambao wamenufaika na
mpango huo ambapo wataalam wa kilimo kutoka maeneo hayo wameelekezwa
namna ya kusimamia zoezi hilo.
Kisima, ameishukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa mbegu kwani
zitasaidia sana kuongeza uzalishaji katika ngazi ya kaya,
Halmashauri,mkoa na Taifa.
Akizindua mpango huo na kukabidhi mbegu kwa wakulima, Kaimu Mkurugenzi
wa Halmashauri ya wilaya Samwel Komba amewataka wakulima waliobahatika
kupata mbegu hizo kuzitumia vizuri na kushirikiana na wataalam wa kilimo
ili waweze kupat mavuno mengi.
“kimsingi sisi kama Halmashauri tunaishukuru sana Serikali kwa kuwezesha
kupata mbegu hizo,tunaamini zitasaidia sana kuinua uzalishaji na hali
ya uchumi kwa wakulima na Halmashauri yetu na kuleta mabadiliko
chanya”alisema Komba.
Amewataka maafisa kilimo na watendaji wa vijiji kuhakikisha mbegu hizo
zinawafikia walengwa katika maeneo husika na kuepuka kugawa kwa viongozi
au kwa kujuana.
Alisema, mbegu hizo zimetolewa kwa wakulima kama fidia na janga la
korona na lina lengo la kuongeza uzalishaji kwa wakulima wa Halmashauri
hiyo na kuishukuru serikali kwa msaada huo wa mbegu za mahindi.
Amewataka wasimamizi wa mpango huo kufikisha mbegu hizo kwa walengwa na
kuhakikisha wanazingatia maelekezo yaliyotolewa na serikali badala ya
kupeleka mbegu hizo katika maeneo na kwa watu wasio stahili.
Alisema, serikali imetoa mbegu hizo ili kuwa na matokeo chanja kwa
kuongeza uzalishaji wa zao la mahindi katika Halmashauri hiyo na
kuongeza pato la kiuchumi kwa wakulima.
Komba alisema, lengo la serikali kutoa mbegu hizo ni kuongeza
uzalishaji wa mahindi sambamba na kutatua changamoto ya ajira kwa
wananchi hasa vijana kupitia sekta ya kilimo ambayo kwa muda mrefu
imeleta mafanikio makubwa kwa wakazi wa Mbinga na maeneo mengine ya mkoa
wa Ruvuma.
Baadhi ya wakulima waliopata mbegu hizo Jakson Lwena na Ester Mapunda
wameishukuru Serikali kwa kuwapatia msaada huo wa mbegu ambao unakwenda
kuongeza uzalishaji wa mahindi katika maeneo yao.
Hata hivyo,wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa mbegu za
mazao mengine kama maharage,mpunga na hata kahawa mazao yanayostawi
vizuri katika wilaya ya Mbinga ili waweze kupanua wigo wa kilimo na
kujinasua na umaskini.
Kaimu Afisa kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Deusdedit Kisima kushoto,akimuonesha Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Samwel Komba sehemu ya shehena ya mbegu bora za mahindi zilitolewa kwa wakulima wa Halmashauri hiyo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji mashambani.
Picha 1 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma Samwel Komba kushoto,akimpa mfuko wa mbegu ya mahindi mkulima wa
kijiji cha Mkako Ester Mapunda zilizotolewa na serikali kwa ajili ya
kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kuleta tija.
Picha zote na Muhidin Amri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...