SHULE ya St Anne Marie Academy imepewa ngao kutambua mchango wake kwenye sekta ya elimu kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma kwenye matokeo ya kitaifa shule yake ya msingi na sekondari.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo zilizoandaliwa na Wizara ya Elimu na Ufundi, imefanyika hivi karibuni ambapo Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ubungo, Abdul Buhety alikabidhi tuzo mbalimbali kwa shule zilizofanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba mwaka 2019/2020.
Afisa Elimu aliipongeza shule ya St Anne Marie iliyoko Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam kwa kuwa ya kwanza Mkoa wa Dar es Salaam na ya nane kitaifa kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2019/2020.
Amesema shule hiyo imeongoza Mkoa wa Dar es Salaam miaka kwa miaka sita mfululizo na kuingia kwenye 10 bora kitaifa ikiwa shule pekee yenye wanafunzi zaidi ya 100 ambao wote wamepata ufaulu kwa daraja A.
Akizungumza mara baada ya kupokea ngao hiyo, Mkuu wa shule hiyo, Gladius Ndyetabula amesema mafanikio hayo ni matunda ya ushirikiano baina ya uongozi wa shule, walimu na watumishi wote.
Amesema imekuwa kawaida kwa shule hiyo kuwapa motisha wanafunzi wake kila wanapofanya vizuri kitaaluma na ndiyo sababu shule imekuwa ikipata matokeo mazuri kwenye mitihani mbalimbali ya kitaifa.
Ameongeza kuwa, wanatarajia kuanza kuwapeleka nchini Dubai, Uingereza hadi Marekani wanafunzi watakaokuwa wanafanya vizuri kwenye mitihani yao ili iwe chachu kwa wengine kufanya vyema kwenye mitihani ya ndani na ile ya kitaifa.
"Shule imejiwekea utaratibu wa kuwapa motisha wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi na huwa tunakawaida ya kuwapeleka mbuga za wanyama kama Serengeti, Mikumi, Ngorongoro hivyo tutaanza kuwapeleka Ulaya," amesema
Juni mwaka 2019, Spika wa Bunge Job Ndugai aliwamwagia sifa wanafunzi wa shule ya St. Anne Marie Academy kwa kufanikuwa kuwa wa kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2018.
Pia Ndugai alitoa pongezi hizo bungeni wakati akiwatambulisha wanafunzi wa shule hiyo walioenda kujifunza shughuli za Bunge kama motisha kutokana na kuipaisha shule hiyo kitaifa.
Katika pongezi hizo, alisema shule hiyo kwenye matokeo ya mwaka 2018 ilifanikiwa kuwa ya kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ya kwanza Wilaya ya Ubungo na ya sita kitaifa hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa shule zilizofanya vizuri zaidi kwenye mitihani hiyo.
Aidha, Ndugai alimpongeza Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza kwa kuwekeza kwenye elimu hivyo kuchangia jitihada za serikali katika kuboresha kiwango cha elimu nchini.
“Haya ndiyo mambo wabunge tunatakiwa tufanye siyo mbunge unamiliki Noah au mbunge unamiliki boda boda lazima tuvuke tujiongeze tuwekeze kwenye elimu kama alivtyofanya Rweikiza,” alisema Ndugai na kuwafanya wabunge waangue kicheko.
Makamu Mkuu wa shule ya St. Anne Marie Academy Amos Joseph, akiwaongoza wanafunzi wa shule hiyo kushangilia ngao waliyopewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka sita mfululizo kwenye matokeo ya kitaifa ya shule ya msingi. Walipata tuzo hiyo wakati wa hafla iliyaondaliwa na Manispaa ya Ubungo mwishoni jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi wa shule ya St Anne Marie Academy ya Mbezi kwa Msuguri jijini Dar es Salaam wakifurahia na Makamu Mkuu wa shule taaluma, Amos Joseph, ngao waliyopewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi kwa kuwa miongoni mwa shule 10 bora zilizofanya vizuri na kuwa ya nane kitaifa kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2019 na kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka sita mfululizo.
Wanafunzi wa shule ya St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam wakishangilia na walimu wao baada ya kupewa ngao ya kutambua mchango wao kwa elimu kwa kuwa ya kwanza Mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka sita mfululizo kwenye matokeo ya taifa mwaka 2019 na kuwa ya nane kitaifa ikiwa na wanafunzi zaidi ya 100.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...