Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Kulia) akizungumza na wakandarasi, Menejimenti ya Wizara hiyo na waandishi wa habari katika hafla ya kuwakabidhi wakandarasi mikataba ya kazi ya ujenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wakandarasi hao katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab
Chaula akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa kandarasi ya Raddy Fibre Solution Ltd, Ramadhani Hassani Mlanzi
mkataba wa kazi ya ujenzi wa
Miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika hafla iliyofanyika katika viwanja
vya Bunge, jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wa Wizara hio Mhe.Dkt. Faustine
Ndugulile na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi wakishuhudia.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile (Kulia) akizungumza na wakandarasi, Menejimenti ya Wizara hiyo na
waandishi wa habari katika hafla ya kuwakabidhi wakandarasi mikataba ya kazi ya
ujenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.
Zainab Chaula na wakandarasi hao katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
Na Faraja Mpina- WMTH
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amewaagiza wakandarasi wanaokwenda kutekeleza
miradi minne ya miundombinu ya mawasiliano yenye thamani ya shilingi bilioni
7.5, kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo ndani
ya muda wa mkataba bila kuongeza hata siku moja ya ziada.
Dkt.
Ndugulile alizungumza hayo alipokuwa katika hafla ya
makabidhiano ya mikataba ya kazi hiyo baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.
Zainab Chaula na wakandarasi hao wazalendo ambao ni Shirika la Mawasiliano
Tanzania (TTCL), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Raddy Fibre
Solution Ltd katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
Miradi hiyo ni pamoja na kujenga,
kupanua na kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuunganisha na
kuimarisha mawasiliano kutoka Mkoa wa Singida hadi Mkoa wa Mbeya, maeneo ya Mkoa
wa Mtwara ili kuunganisha mawasiliano kati ya Tanzania na Msumbiji na kutoka
eneo la Mji wa Serikali Mtumba hadi Msalato jijini Dodoma.
Aliongeza kuwa jumla ya kilomita 409 zitaunganishwa na Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano katika maeneo hayo na Halmashauri 12 nchini zitawekewa vibao vya
majina ya mitaa/barabara na namba za nyumba katika kutekeleza Mradi wa anwani
za makazi na postikodi.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa lengo ni kuhakikisha mpaka kufikia mwaka
2025 asilimia 80 ya wananchi wanapata mawasiliano ya uhakika na kushiriki
katika kuinua uchumi wa kidijitali kupitia biashara mtandao, ambapo mnunuzi na
muuzaji lazima wawe na mawasiliano ya mtandao na mnunuzi kuwa na anwani ya
makazi ili afikishiwe bidhaa aliyonunua mpaka nyumbani kwake.
“Sina shaka na wakandarasi wazalendo, mtajiengua ninyi wenyewe iwapo
mtakuja na visingizio vya kutokamilisha kazi kwa wakati, mkafanye kazi mchana
na usiku kuhakikisha miradi inakamilika ndani ya muda wa mkataba na ubora
unaokubalika”, Dkt. Ndugulile
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa Wizara inaendelea na mchakato wa
kushughulikia suala la vifurushi na bando na kuomba wananchi kuwa na subira
mpaka mwisho wa mwezi huu ili Wizara kuja na tamko rasmi ambalo halitaathiri
mapato ya watoa huduma, mapato ya Serikali na vilevile kutomuathiri mwananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi wasipokee
maelekezo yeyote kuhusu miamala binafsi kwa njia ya simu bali njia sahihi ni
kwenda kwenye vituo vya mawakala vinavyotambulika na vilivyosajiliwa na
makampuni ya simu.
“Tunataka kuimarisha mifumo ya mawakala wa makampuni ya simu ili kuweza
kuwabaini na kuwachukulia hatua mawakala ambao sio waaminifu”, Dkt. Ndugulile
Amesema kuwa, Serikali imeanza mkakati wa kushughulika na watu
wanaotoa lugha za matusi, kashfa na utapeli
mitandaoni ambapo mpaka
sasa genge la watu 17 wanaoongoza genge la uhalifu mitandaoni waliokuwa
wamejificha mkoani Morogoro wameshakamatwa na muda wowote watapandishwa
mahakamani.
Ameongeza kuwa Serikali ina nia njema ya kujenga mazingira wezeshi ya
kuweza kutumia mitandao ya mawasiliano na katiba ya nchi inaruhusu wananchi kukosoa
kwa lugha ya staha, huku akisisitiza kuwa lugha za matusi, kashfa na kejeli
hazitovumilika.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...