Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederick
Clavier(wa pili kushoto) akizungumza kuhusu siku ya kimataifa ya kusherehekea
lugha ya Kifaransa ambapo ameelezea jitihada zinazoendelea katika kuhakikisha
Watanzania wengi nao wanazungumza lugha ya Kifaransa.
wa Ufaransa nchini Tanzania Frederick Clavier(wa
pili kushoto) akisisitiza jambo.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
UBALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania umesema upo
kwenye mchakato wa kuandaa programu maalum ya muda mrefu ya kuwa inatoa mafunzo
ya lugha ya Kifaransa kwa walimu kati ya 50 hadi 100 kila mwaka ambao
wakishaifahamu vema nao watafundisha wanafunzi katika shule zao.
Lengo la kuandaa programu hiyo ambayo kwa sasa
bado mazungumzo yanaendelea kati ya Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederick
Clavier na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa
Paramagamba Kabudi pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Profesa
Joyce Ndalichako ili kuona namna nzuri ya kuifanikisha programu hiyo.
Akizungumza leo Machi 10, 2021 jijini Dar es
Salaam wakati akielezea siku ya kimataifa ya kusherehekea lugha ya Kifaransa
Duniani kote, Balozi Clavier ametumia nafasi hiyo kuelezea mikakati ambayo
wanaifanya kuhakikisha lugha hiyo inapata nafasi ya kuzungumzwa na watu wengi
nchini Tanzania.
"Tunaendelea na mazungumza na Waziri Kabudi,
pamoja na Wizara ya Elimu chini ya Profesa Joyce Ndalichako ili kuwepo na
utaratibu wa kufundisha lugha ya Kifaransa kwa walimu wa kada mbalimbali na
watakapomaliza nao watakwenda kufundisha wanafunzi.
"Katika programu hiyo iwapo itaanza basi kwa mwaka tutakuwa tunafundisha lugha ya Kifaransa kati ya walimu 50 hadi 100 na hivyo baada ya miaka mitatu au mitano tutakuwa na walimu wengi ambao wanajua kuzungumza Kifaransa.Programu hiyo itakuwa ya muda mrefu wastani wa kuanzia miaka 10,"amesema Balozi Clavier.
Amefafanua kuwa mazungumzo yatakapokamilika watatoa taarifa rasmi ya lini sasa programu hiyo itaanza ingawa kuna Watanzania mbalimbali ambao wamekuwa wakijifunza na kuzungumza Kifaransa.
Aidha amesema wengine ambao watanufaika na
programu hiyo itakapoanza ni wanadiplomasia ambao wengi wao wamekuwa
wakizungumza lugha zaidi ya moja, na watamani Kifaransa kinakuwa moja ya lugha
ambayo itasomwa na kada hiyo.
Kuhusu siku ya kimataifa duniani ya kusherehekea
lugha ya Kifaransa, Balozi Clavier amesema kila ifikapo Machi ya kila mwaka
familia ya nchi ambazo watu wake wanatumia lugha ya Kifaransa nchini wamekuwa
wakikutana na kusherehekea kwa kufanyika matukio mbalimbali.
Amesisitiza kuwa lugha ya Kifaransa imekuwa
miongoni mwa lugha ambayo inazungumzwa na mamilioni ya watu duniani kote, na
kwamba nchi ya Ufaransa itaendelea na jitihada za kuhakikisha watu wengi zaidi
wanazungumza lugha hiyo.
Balozi Clavier ametumia nafasi hiyo kutaja nchi
kadhaa ambazo zinazungumza lugha hiyo huku akifafanua kwa Tanzania kumekuwepo
na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa chachu kwa Watanzania kujifunza lugha
hiyo kupitia programu ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Peter Van Acker amesema
wamekutana leo kimaalum kwa ajili ya
kusherehekea Francphoinie huku akifafanua nchni Ubelgiji wanazungumza lugha
kama Kiholanzi, Kifaransa na Kijerumani."Kuzungumza lugha tofauti ni
muhimu sana.
"Leo niko hapa na malozi wenzangu tukiwa na
mwenyeji wetu Balozi wa Ufaransa, kwa maana nusu ya watu wangu wanazungumza
Kifaransa, kwa bahati mbaya mwaka huu hatutapata fursa ya sawa na mwaka jana ya
kukuza lugha nzuri ya Kifaransa kutokana na changamoto ya janga la Corona
ambayo imeharibu sherehe zetu.
"Kwa hiyo tutakuwa na sherehe za
mkondoni yaani online , tutakuwa na
hafla tatu tofauti kupitia njia ya mtandao , kwanza tutaonesha jinsi ya kuoka
waffle ambayo ni keki ndogo iliyookwa
kwa chuma na kukaushwa maarufu nchini Ubelgiji , pili tutashirikishana nawe
uzoefu wa wanafunzi wa kitanzania nchini Ubelgiji, tatu tutatoa habari kuhusu
fursa za masomo nchini kwao,"amesema Balozi Acker.
Awali Balozi wa Morroco nchini Tanzania Abdelilah
Benryane amezunungumza kwa kirefu kuhusu siku ya kimataifa ya kusherehekea
lugua ya Kifaransa duniani huku akitumia nafasi hiyo kuelezea namna ambavyo
mamilioni ya watu duniani wamekuwa wakifurahia kuzungumza lugha ya Kifarasa.
Amesisitiza umoja na mshikamano kwa familia ya Francophonie na wataendelea
kuhamasisha nchi nyingi zaidi watu wake kuzungumza lugha hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...