Na Lulu Mussa, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amezitaka Asasi zisizo za Kiserikali/Asasi za Kiraia (NGOs, CBOs na CSOs) zinazojihusisha na shughuli za Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kushiriki kikamilifu katika kusukuma mbele agenda ya Mazingira Nchini.
Waziri Jafo ameyasema hayo hii leo katika kikao maalumu kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma kilichojadili mchango na majukumu ya Asasi zisizo ya Kiserikali katika Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini.
Jafo amesema lengo la Serikali ni kuhamasisha utendaji kazi wa Asasi hizo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu stahiki na kuimarisha uratibu wa shughuli za Usimamizi wa Mazingira nchini na kudumisha mahusiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Asasi zisizo za Kiserikali zinazohusu Hifadhi ya Mazingira.
“Leo ni siku ya ndoto
yangu kukutana na wadau muhimu katika kusukuma mbele agenda ya Mazingira, hii
inanipa faraja kubwa kuona tunao wadau wengi sana wenye nia ya dhati katika kusukuma
mbele agenda hii muhimu”
Jafo amesema bajeti ya
Mazingira ni ndogo na kupitia wadau hao ametoa rai kwao kujikita zaidi katika usimamazi wa mazingira kwa
kushirikiana na Serikali ili kuratibu shughuli za Mazingira kwa ufanisi zaidi katika
Mikoa yote.
“Nafahamu, nyinyi
mmekuwa wadau wakubwa katika hifadhi ya mazingira nchini na mmekuwa mkijitoa
katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu agenda
hii muhimu ya mazingira kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo,”
Waziri Jafo alisisitiza.
Waziri Jafo amezitaka
asasi hizo kusogeza huduma katika maeneo mengi nchini ili kuleta tija na
kupambana na uharibifu wa mazingira ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na
shughuli za kibanadamu zisizo endelevu.
“Ndugu zangu hatuwezi
kupata uchumi endelevu bila kudhibiti mazingira yetu, uharibifu wa mazingira
duniani ni wakutisha, athari za mabadiliko ya tabianchi nsi kubwa na kumekuwa
na ongezeko la kina cha maji katika Mito, Mabwawa na Maziwa kutokana kuongezeka
kwa mvua juu ya wastani,” Jafo alisisitiza.
Awali Katibu Mkuu Ofisi
ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga alisema Serikali na Asasi za Kiraia
zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia misingi ya Uwazi, Uadilifu,
Sera, Sheria, Taratibu na Miongozo ya Serikali inayolega kuongeza ufanisi, tija
na uendelevu katika usimamizi wa mazingira nchini.
Mmoja wa washiriki wa
Mkutano huo Bi. Winifrida Shonde kutoka Asasi ya Tanzania Environment and
Empowerment Movement (TEEM) aliishauri Serikali kuhakikisha kila asasi za
zisiso za kiraia kupewa majukumu ya kuainisha malengo katika katika hifadhi ya
mazingira ili kuweka utaratibu bayana wa utekelezaji wa shughuli za usimamizi
wa mazingira hapa nchini.
Katika
kikao hicho baina ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs, CSOs & CBOs)
kimehusisha takribani washiriki Mia Mbili kutoka kote nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...