Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa  Sifuni Mchome  Akikaangalia  Zahanati ya Jeshi la Polisi Wilayani Mpanda Mkaoni Katavi ambayo imeshakamilika ujenzi wake lakini  imeshindwa kuanza kutoa huduma kutokana na kukosekana kwa vifaa tiba, madawa na samani. Katibu Mkuu ameahidi kuichangia shilingi  Milioni Tano.
Katibu Mkuu  Mchombe na Katibu John Jingu  wakibadilishana mawazo na  Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Katavi baada ya kuitembelea zahanati hiyo.


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa  Sifuni Mchome, ametoa ahadi ya kuchangia  shilingi milioni tano   ukiwa ni  mchango wake wa kusaidia  kukamilisha Zahanati ya  Jeshi la Polisi  Wilayani Mpanda, Mkoani Katavi.

Ametoa mchango huo baada ya   Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Benjamin E. Kuzuga  kuelezea  kwamba, Jeshi la Polisi Mkoani humo limekamilisha ujenzi wa  Zahanati yake, lakini bado haijaanza kutoa huduma kutoka na  ukosefu wa vifaa tiba, madawa  na samani.

Aidha  Kamanda Kuzunga alieleza kwamba kama   Zahanati hiyo  ingeanza kutoa huduma basi pia     kituo cha mkono kwa mkono ( one stop center) ambacho pamoja na mambo mengine  kingeweza kutoa huduma na faragha  kwa akina  mama na watoto  wahanga wa vitendo vya   ukatili wa kijinsia.

Hayo yamejili  wakati wa kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki   wilayani Mpanda , Mkoani  Katavi  kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria , Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na baadhi    ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi  mkoani  Katavi. Kikao hicho  kilichofanyika katika Bwalo la Polisi kilikuwa ni cha kubadilishana  mawazo kuhusu hali ya utoaji wa Hakijinai  kwa upande wa Jeshi la  Polisi.

“Changamoto  moja kubwa ni ya kutokuwa na  kituo cha mkono kwa mkono ( one stop center) kutoka na kutokuanza kufanya kazi kwa Zahanati yetu ambayo ujenzi wake umetokana na  michango ya askari na maafisa  na kuchangiwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi  ( IGP)   na baadhi ya  wadau wengine, hata hivyo jengo limeshindwa  kuanza kazi kutokana na  kutokuwa na vifaa tiba, madawa na samani” akasema ACP Kuzunga.

Amebainisha kwamba ujenzi  wa Zahanati umegharimu takribani shilingi Milion 70. Na kwamba zinahitajika shilingi milioni 24 kwaajili ya  ununuzi wa vifaa tiba na mambo mengine na tayari  wameshanunua  baadhi ya vifaa  vyenye  thamani ya shilingi  milioni 3.

“Katika hili la Zahanati, kwanza niwapongeze kwa juhudi zenu hizi, basi mimi  nitachangia shilingi Milioni Tano  ili zisaidie mambo fulani fulani  kwasababu jambo mmlilolibuni ni  jema” akaahidi Katibu Mkuu Profesa Mchome.

Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchombe akiambatana na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto, walipata fursa ya kuitembelea Zahanati hiyo wakiongowa na Kamanda wa Polisi ambaye aliwaeleza kwamba,Zahanati hiyo  ina vyumba vya madaktari vitatu, chumba cha maabara, chumba cha kuhifadhia dawa na chumba wa akina  Mama na chumba cha watoto.

 Kuhusu upatikanaji wa madaktari,  Kamanda ACP Benjamin Kuzuga amesema Mganga  Mkuu wa Mkoa pia ameahidi kuangalia uwezekano wa kusaida katika eneo hilo.

Wakati  Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Profesa Mchombe akiahidi kutoa milioni Tano, kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. John Kingu  ameahidi kuisaidia  zahanati hiyo  gari pamoja na  vifaa vingine ili hatimaye zahanati iweze kuanza kazi  haraka iwezekanavyo.

Awali Katika kikao hicho cha  Makatibu Wakuu na Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi ,RPC  pia alielezea ukosefu  wa majengo  ya Kituo vya Polisi karibu katika wilaya zote za mkoa huo pamoja  na ukosefu wa  nyumba za askari .

Akasema hata Ofisi yake ipo katika  Jengo ambalo ni Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mpanda.

“Waheshimiwa Makatibu Wakuu, kwa kuwa Mkoa huu ni mpya,  tunashida sana ya Majengo ya Vituo vya Polisi , hata askari wetu wanaishi uraiani ama katika nyumba za kupanga au walizojenga wenyewe. Kiutendaji wa majukumu yetu hali hii si salama sana, kwa sababu ikitokea dharura tu   itakuwa  shida sana kukutana na kukusanyika mara moja.  Na ndiyo maana kiutaratibu  askari wanatakiwa kuishi kambini ili kukitokea  dharura yoyote inakuwa rahisi kuwasiliana”

Aidha  RPC Kuzuga  pia ameeleza kwamba hali hiyo ya kutokuwa na Vituo vya Polisi kumepelekea kutokuwapo kwa vyumba maalumu vyenye mazingira mazuri ya kusikiliza na kuchukua maelezo ya wahanga  waliohujumiwa kijinsia na kwamba katika baadhi ya maeneo imebidi  askari na wahanga hao  kukaa chini ya miti ili kuchukua maelezo  yao au kuwapatia huduma nyingine stahiki.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Profesa  Mchome, amesema Jeshi la Polisi ni sehemu ya  mnyororo  wa mchakato wa  kuijenga Tanzania iliyobora na wananchi wake kutekeleza majukumu yao bila hofu na hivyo kujiletea maendeleo yao binafsi na  maendeleo ya taifa lao.

  Na kwa sababu hiyo, amelitaka Jeshi  la Polisi Mkoani Katavi,  kama chombo cha utoaji wa HakiJinai kutekeleza majukumu yake kwa weledi, kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu ambazo Jeshi hilo limejiwekea  pamoja na Sheria za Utumishi wa Umma.

Akasema  Jeshi la Polisi pamoja na changamoto mbalimbali  bado limeweza kutekeleza majukumu yake ya utoaji Hakijinai, na akalitaka kutumia sheria ya ufifishaji wa makosa hasa yale makosa madogomadogo ambayo yanaweza kuishia au kumalizwa  katika Kituo cha Polisi na hivyo  kujipunguzia wenyewe mzingo wa mafaili ya upelelezi lakini  kuvisaidia pia vyombo vingine vya  utoaji hakijinai mzigo wa kuendesha mashataka na kesi na mlundikiano wa wafungwa na mahabusu.

Amebainisha kwamba, katika mnyororo wa  utoaji Hakijinai,  Serikali  ya awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeelekeza  mambo ya kutekeleza na  Jeshi la Polisi kama sehemu ya Serikali mnaowajibu pia wa kuyatekeleza.

Akayataja  baadhi ya mambo hayo   kuwa ni pamoja na kutenda haki kwa kila kosa na kwa weledi, uadilifu, kujiamini  kuwajibika na kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu na  kumaliza  baadhi ya mashauri kwa njia ya upatanishi  na utoaji wa adhabu mbadala badala ya kukimbilia mahakamani pasipo ulazima wa kufanya hivyo, mahakama iwe chombo cha mwisho kabisa.

  “Ujumbe wa Mhe. Rais Samia  Suluhu Hasani  kuhusu eneo la utoaji haki katika maeneo mbalimbali ni kutenda haki, tusimbambikie watu kesi, anataka haki itendeke kwa wakati na kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu, Jeshi la Polisi ni  sehemu ya  mnyororo wa utoaji wa haki lakini pia mnao mchango mkubwa sana katika kuijenga nchi yetu kiuchumi” akasisitiza  Katibu Mkuu Mchome.

Akalipongeza pia Jeshi hilo la Polisi  kwa kazi nzuri inayofanya kupitia Dawati la Jinsia,  Dawati ambalo limekuwa  kimbilio na faraja  wahanga wa matukio mbalimbali hasa ya udhalilishaji wa kijinsia wanaotafuta haki zao.

Makatibu Wakuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Utumishi na Utawala Bora,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wapo katika Ziara ya Kikazi ya Kawaida  ambayo imewafikisha katika Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi na katika  mikoa hiyo yote Makatibu Wakuu hao wamekuwa na vikao mbalimbali na Wadau wa Mnyororo wa Utoaji  Hakijinai na Watumishi wa Serikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...