Na Mwandishi wetu, Manyara

HAKIMU wa Mahakama ya Mkoa wa Manyara, Simon Kobelo amemuhukumu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Tawi la Maisaka Kati Mjini Babati, Bakari Khatibu Yangu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya laki tatu kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa mwinjilisti wa Kanisa la KKKT mtaa wa Komoto Daniel Jacob Tango.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Makungu amesema Mwenyekiti huyo wa CCM Yangu ameingia hatiani baada ya kukiri makosa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Amesema alitenda kosa hilo ili amwachie mwinjilisti huyo kiwanja ambacho Mwenyekiti huyo alikuwa akidai ni mali ya CCM.

Amesema awali, kesi hiyo namba CC 24/2020 ilifikishwa katika mahakama hiyo na mawakili wa TAKUKURU Martin Makani na Evelyne Onditi, Juni 26 mwaka 2020 ambapo mshtakiwa alikana mashtaka yake.

"Baada ya kukana makosa yake mawakili wa TAKUKURU waliwasilisha vielelezo na ushahidi ulioiwezesha Mahakama kumwona mshtakiwa ana kesi ya kujibu mashtaka baada ya kutakiwa kujitetea aliamua kutoisumbua mahakama kwa kukiri makosa yake yote ya kuomba na kupokea rushwa kama alivyoshtakiwa," amesema Makungu.

Amesema baada ya kukiri makosa yake Mahakama ikatoa ikatoa adhabu kwa mujibu wa kifungu cha 15 (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 ambapo mshtakiwa Yangu aliweza kulipa faini hiyo ya shilingi laki tatu na hivyo kukwepa kifungo cha miaka miwili kwenda jela.

"Tunatumaini kuwa hukumu hii itakuwa fundisho kwa viongozi ndani ya chama tawala hasa wa ngazi ya chini wenye utajiri wa fikra haba wanapopitapita na kuwaaminisha wananchi kuwa hawawezi kuguswa na TAKUKURU kwa sababu ni chama kilichowaajiri na kinaongoza Serikali," amesema Makungu.

Ametoa rai kwa viongozi wa aina hiyo wakumbuke  kuwa ibara ya 13 (1) ( 5) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza usawa mbele ya sheria kwa watu wote bila kuzingatia utaifa wao, kabila, pahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini jinsia na hali yao ya kimaisha.

"Kwa msingi huo kiongozi wa chama tawala au vyama vingine vya upinzani, sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 inakuhusu na inaweza kuchukua mkondo wake pale unapovunja sheria hiyo ili mradi nafasi hiyo iwe ni kutekeleza majukumu yanayohusiana na umma wa Watanzania kama ilivyofanya kwa Bakari Khatibu Yangu," amesema Makungu.
 

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...