KITUO cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kilichopo Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine(SUA) kimesema pamoja na mambo mengine, moja ya mkakati ni kuandaa watalaamu kwa ajili ya kufanya tafiti na kutoa takwimu sahihi zinazohusu hewa ukaa.
Kwa mujibu wa kituo hicho kinawajibu wa kufanya tafiti na kupata takwimu zikiwemo za uharibifu wa misitu na mazingira pamoja na utekelezwaji wa Mpango au Mkakati wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa.
Wakizungumza wakati wa semina mbele ya waandishi wa habari za mazingira nchini kupitia Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira(JET) maofisa wa kituo hicho wametumia nafasi hiyo kufafanua masuala mbalimbali yanayofanywa na kituo hicho cha kitaifa kufuatilia hewa ukaa.
Akifafanua wakati wa semina hiyo, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Profesa Eliakim Zahabu ameeleza kituo hicho cha kitaifa kimekuwa kikifuatilia kwa karibu athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na kwa sasa Kituo hicho kinaandaa watalaamu ambao watakuwa wakifanya tafiti mbalimbali.
"Tunayo mikakati mingi kama Kituo chaTaifa cha Kufuatilia Kaboni , na miongoni mwa mkakati ni kuwa na watalaam wetu ambao watabobea kwenye kufanya tafiti na kutoa takwimu.Tunayo sensa ambayo imefanyika huko nyuma hasa inayohusu uharibifu wa misitu na mazingira kwa ujumla, hivyo tunatarajia kufanya utafiti mwingine,"amesema Profesa Zahabu.
Ameongeza uwepo wa takwimu sahihi utasaidia kufahamu hali halisi iliyopo chini inayohusu uharibifu wa misitu ambayo ndio inayovyonza hewa ukaa na kuiifadhi ili dunia iendelee kuwa sehemu salama.
"Tukiwa na watalaamu wetu , kisha wakafanya utafiti nchi nzima tutakuwa na taarifa sahihi ingawa tunayo takwimu iliyofanyika huko nyuma na kuonesha uharibifu mkubwa wa mazingira,"amesema na kuongeza uharibifu huo wa mazingira umechangia uwepo wa mabadiliko ya tabianchi na madhara yake yamekuwa wakiongezeka siku hadi siku.
Kuhusu semina hiyo kwa waandishi wa habari za mazingira, Profesa Zahabu amesema "Tuko hapa kwa ajili ya kuelimishana kuhusu mabadiliko ya tabianchi, pia kujenga mahusiano kati ya kituo na waandishi wa habari ili hata tunapoihabarisha jamii tuwe tunazungumza lugha moja".
Wakati huo huo, Mkuu wa Ndaki ya Wanyamapori, Misitu na Utalii SUA Profesa Suzana Augustino ametumia nafasi hiyo kueleza Tanzania ni miongoni mwa nchi mwanachama wa mpango wa kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa wenye lengo la kupunguza gesijoto ambayo kwa namna moja hadi nyingine imekuwa na athari mbalimbali.
Pia amesema nchini Tanzania bado kuna fursa ya kunufaika na Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa (MKUHUMI)."Jambo hili litasaidia kuimarisha misitu nchini na kuimarisha mazingira kwa ujumla.Tunafahamu wananchi wa kipata elimu watakuwa na uwezo wa kuuza hewa ukaa."
Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa JET John chikomo amezungumzia umuhimu wa semina hiyo iliyoandaliwa na kituo hicho kwa waandishi wa habari za mazingira na kwamba semina hiyo imekuja wakati muafaka hasa kutokana na kuendelea kujitokeza kwa athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na uharibifu wa mazingira.
"Ni jambo jema waandishi wa habari za mazingira kushiriki kwenye semina hii ambayo imewaongezea uelewa.JET katika miradi yetu tumekuwa na semina kwa ajili ya waandishi na wahariri."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...