Leandra Gabriel na Avila Kakingo - Michuzi TV
KATIKA kuhakikisha jamii inaelewa zaidi juu ya majukumu yanayotekelezwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC,) tume hiyo imekutana na kutoa semina ya kitaifa kwa wahariri na waandishi wa habari Mkoani Dar es Salaam kuhusu nguvu za atomiki, matumizi yake pamoja na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa na jamii kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa semina hiyo Mkuu wa ofisini ya (TAEC,) kanda ya Dar es Salaam Dkt. Wilbroard Muhogora ameeleza namna tume hiyo inavyolinda watu na mazingira katika kuhakikisha hawaathiriki na mionzi na wamekuwa wakipima sampuli 9400 za vyakula ndani ya miezi mitatu chini ya wataalamu wapatao 1942 nchi nzima.
Amesema, Tume hiyo imekuwa ikidhibiti matumizi salama ya mionzi ili kulinda Umma, wafanyakazi na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi pamoja na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya jamii na uchumi.
Katika kuhakikisha usalama kwa jamii dhidi mionzi Muhogora amesema, Tume imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa viashiria vya mionzi katika vyakula vinavyoingizwa ndani ya nchi kuhakikisha kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu.
"Kwa upande wa mazingira tume hufuatilia viasilia vya mionzi katika madini, makaa ya mawe, fosfeti, mbolea pamoja na vifaa vya ujenzi pia tume hufanya uchambuzi mionzi kwa sampuli zote zinazoletwa na wateja na baadaye kutoa vibali vya kuthibitisha ubora wa sampuli hizo." Amesema.
Awali akifafanua kuhusu dhana ya mionzi Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Prof. Lazaro Busagala amesema jamii imekuwa ikihusianisha dhana ya mionzi/ nguvu za atomiki na mabomu jambo ambalo siyo sahihi na kueleza kuwa, mionzi ina faida nyingi kwa maendeleo na ustawi wa katika jamii na hutumika katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, mifugo na viwanda na kusisitiza kuwa isipotumika kwa usahihi inaweza kuingia katika mnyororo wa chakula ambao ni hatari kwa afya ya binadamu na wanyama.
Akifungua mafunzo hayo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alisema kuwa matumizi sahihi ya nguvu za atomiki zimekuwa zikinufaisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, mafuta, gesi, kilimo, mifugo na viwanda.
Prof. Ndalichako aliishauri jamii kufatilia taarifa zinazotolewa na tume hiyo ili kufahamu faida na tahadhari zinazotolewa ili kuweza kujiepusha na mionzi hatarishi.
Pia aliwataka waandishi wa habari kuendelea kutumia vyema kalamu zao katika kuhabarisha jamii kwa namna ya kujenga jamii imara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...