KAIMU Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Vonesi Uiso amesema kwamba tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA) tangu kuanzishwa kwake imekuwa na wajibu wa kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Amesema hayo wakati akifungua mkutano wa kikao kazi ulioandaliwa na TMDA kwa kukutana na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara pamoja na Dar es Salaam.Mkutano huo wa kikao kazi umefanyika jijini Arusha.
Akizungumza zaidi mbele ya wahariri hao na maofisa wa TMDA wakiongozwa na Mkurugenzi wao Mkuu Adam Fimbo , Uiso amesema "Nyote ni mashahidi wa umuhimu wa taasisi hii hususan katika kipindi hiki cha majanga ya dunia ya milipuko ya magonjwa kama CORONA na mengineyo mengi.
"Tofauti na bidhaa nyingine, dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni bidhaa nyeti zinazoweza kuwa na madhara makubwa ya kiafya kwa watumiaji kama vile kusababisha ulemavu, kupoteza maisha na kudhoofisha uchumi wa nchi kama hazikudhibitiwa ipasavyo.
"Kwa mantiki hiyo bidhaa hizo zinahitaji kudhibitiwa kwa utaratibu wa namna ya pekee; lengo likiwa ni kuzuia madhara ya aina hiyo kwa walaji. Ili TMDA ifikie lengo hilo, bidhaa hizi zinahitaji kuhakikiwa usalama, ubora na ufanisi wake kabla ya kuruhusiwa kutumika, kazi ambayo inasimamiwa na TMDA,"amesema Kaimu Mganga Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha.
Amefafanua baadhi ya majukumu ya msingi ya Mamlaka hiyo katika kuhakikisha afya ya wananchi inalindwa ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopo katika soko ni salama na zenye ubora.
Pia ina jukumu la kudhibiti matangazo ya bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kuzuia matangazo yenye nia ya kupotosha umma kwa lengo la kibiashara ambapo matangazo ya aina hiyo hutolewa katika vyombo vya habari mnavyovifanyia kazi.
"Napenda kuwaeleza suala la kudhibiti matangazo ni la kisheria na katika kuhakikisha utekelezaji wake, zipo Kanuni za Udhibiti wa Matangazo ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi zilizoandaliwa chini ya Sheria Sura 219 na zilianza kutumika tangu mwaka 2010.
"Hata hivyo, kati ya changamoto kubwa ambazo Mamlaka imekuwa ikikabiliana nazo toka kuanzishwa kwake ni kushuhudia kutolewa kwa matangazo ya bidhaa inazozidhibiti kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii bila kibali cha TMDA ambapo ni kinyume na matakwa ya Sheria na Kanuni na hivyo kuchangia kupotosha jamii,"amesema Uiso.
Pamoja na changamoto hiyo katika vyombo vya habari, amesisitiza anafurahishwa na ushirikiano ambao umeendelea kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikitoa taarifa kwa Mamlaka kuhusu ukiukwaji wa sheria hususan urushwaji wa matangazo bila kibali cha TMDA.
Aidha, ametoa pongezi kwa vyombo vya habari, wahariri na waandishi ambao wamekuwa wakitoa taarifa mbalimbali kuhusu umuhimu wa kudhibiti bidhaa unaofanywa na TMDA na hivyo kuongeza tija na uelewa wa Jamii.
"Ni kwa kuzingatia umuhimu wenu na michango yenu ndio maana tunakutana ili tuweze kujadiliana kwa pamoja na kutoa maoni yatakayosaidia TMDA katika kuboresha huduma zake na hivyo kufanikisha lengo kuu la kulinda afya za watumiaji wa bidhaa hizi ambao kimsingi ni sisi wenyewe pamoja na familia zetu, ndugu, jamaa, majirani na marafiki.
"Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba haiwezi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila ushirikiano wenu. Ni imani yangu kuwa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuishirikisha jamii mtaweza kuelewa matatizo yaliyopo yanayohusiana na usalama na ubora wa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219 inatekelezwa na wadau wote kwa ufanisi,"amesema.
Aidha amesema mtakumbuka hivi karibuni, TMDA imekuwa ikitoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa dawa mbalimbali bandia na duni katika nchi yetu. Uwepo wa dawa hizo bandia ni hatari kwa afya za wananchi.
"Hivyo, ninawaomba sana muendelee kutumia vyombo vyenu kuwaelimisha wananchi kuhusu suala hili hususan kuwaelimisha wafanyabiashara waache mara moja kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka maeneo yasiyo rasmi.
"Na pia katika maeneo ambayo ni kinyume cha Sheria kwani mara zote bidhaa hizo huwa si salama kwa matumizi ya walaji. Ikmbukwe kwamba Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote atayepatikana na bidhaa duni au bandia kwa kigezo kuwa hawakujua wakati huo huo wakiwa wamesababisha madhara kwa watumiaji," Amesema Uiso.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...