Na Amiri Kilagalila,Njombe
MKUU wa wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa Kasongo amewataka watumishi wa halmashauri ya mji wa Njombe kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano na kutekeleza matarajio ambayo Serikali imeweka kwa wananchi wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuwa na uelewa wa pamoja na kuepusha migogoro katika kufanya maamuzi na kutekeleza kazi za kufikisha maendeleo kwa Wananchi.

Kissa amesema kuwa katika kusukuma gurudumu la Maendeleo na kuifanya Njombe kuwa mbele usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo ni jambo ambalo anatarajia kulianza na amepanga kufanya ziara za kushtukiza na ziara rasmi ili kujionea utendaji halisi uliopo katika Sekta ya Afya na Elimu na amewataka Watumishi wa Sekta hizo kujiandaa na kurekebisha kasoro ambazo pengine zinaweza kuleta kero kwa Wananchi kwenye maeneo hayo. Aidha ametaka katika kila miradi uwepo wa nyaraka zote muhimu.

Akipokea taarifa fupi ya utekelezaji wa shughuli za Maendeleo kwa mwaka 2020/2021 katika Halmashauri taarifa iliyowasilishwa na Mchumi wa Halmashauri Emma Lunojo Mhe. Kissa ameipongeza Halmashauri kwa kazi nzuri iliyofanyika.

“Taarifa hii inaonesha picha halisi ya uchapakazi, uzalendo na ari ya kuleta matukio makubwa kwa Nchi ya Tanzania. Niwapongeze kwa Kazi kubwa ambayo mmeifanya. Tufanye kazi kwa ubunifu. Sisi tumepata bahati ya kufanya kazi kwa niaba ya Watanzania wengine wote. Wote wangeweza kupewa nafasi Ila tumepewa dhamana kwa ajili ya wengine” Alisema Mkuu wa Wilaya.

Miongoni mwa maelekezo aliyoyatoa ni kuhakisha kuwa Watumishi wanawahudumia Wananchi kwa Wakati na kutumia busara na hekima katika kuwaelekeza Wananchi wanaofika kupata huduma na kuacha tabia ya kuwashambulia Wananchi kwa maneno yasiyofaa.

Akitoa salamu za Shukrani kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Mganga Mkuu wa Halmashauri Dkt. Yesaya Mwasubila amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuteuliwa na hatua aliyoichukua ya kuja kuzungumza na Watumishi wa Halmashauri hiyo na amesema kuwa yale yote ambayo ameyaelekeza yatakwenda kutekelezwa na kuahidi ushirikiano mkubwa katika kazi.

Mara baada ya kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kissa Gwakisa Kasongo leo amezungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji Njombe na anataraji kuanza ziara ya kikazi katika Wilaya ya Njombe kuanzia Jumanne ya tarehe 13 Julai 2021 kwenye kila Kijiji, Mtaa na Kata.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...