Prisca Ulomi na Faraja Mpina, Dodoma
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji amezungumza na wajumbe wa Mkutano wa ALAT unaojumuisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kwenda kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa kuifanya kuwa ajenda ya kudumu katika mabaraza ya madiwani na vikao vyote vya kisheria vinavyofanyika katika Halmashauri zao
Hayo ameyazungumza wakati wa Semina ya kujenga uelewa na kuhamasisha utekelezaji wa mfumo huo kwa wajumbe wa ALAT jijini Dodoma leo Septemba, 2021 na kuwasisitiza kwenda kudhihirisha wanaweza kutekeleza kwa vitendo kwa sababu dhamira ipo, bajeti ipo na uwezo upo wa kulikamilisha uwekaji wa Mfumo huo
Dkt. Kijaji amewataka viongozi hao kwenda kuwashirikisha watendaji wao na waheshimiwa madiwani ambapo watashuka mpaka katika ngazi ya kata,Kijiji, mtaa na kitongoji katika halmashauri zote 184 nchi nzima ili manufaa ya mfumo huo yafahamike kwenye jamii na kuwe na muitikio chanya wa utekelezaji wake
Amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ni mfumo mama wa mifumo yote ya utambuzi tuliyonayo nchini inayoiwezesha Serikali kumfikia mwananchi mahali alipo na mwananchi kuweza kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi na kijamiii kwa kufikishiwa huduma na bidhaa mpaka mahali ambapo mwananchi huyo yupo
“Tunapokwenda kurahisisha utoaji wa huduma kupitia Anwani za Makazi na Postikodi inamaanisha hata uchumi wa mwananchi utaenda kukua hivyo wakurugenzi na wenyeviti ambao ndio mnaowahudumia wananchi moja kwa moja mlibebe hili”, alizungumza Dkt. Kijaji
Amesema kuwa “Dunia inaelekea kwenye uchumi wa dijitali ambapo biashara na huduma zinatolewa kwa njia ya mtandao na kufikishiwa popote ulipo duniani, nasi tunataka kama nchi tuweze kufikia huko na kwa mapenzi mema ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake ya Awamu ya Sita amesema tunakwenda kuuwezesha mfumo huu kukamilika”.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 imeimarisha Mfumo wa Anwani za Kitaifa ambao unamtambulisha kila mwananchi mahali alipo kwa kutumia Anwani za Makazi na Postikodi
Amesema kuwa zoezi la kusimika mfumo huo lilizinduliwa rasmi mwaka 2016 na kwa ushirikiano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Halmashauri zote nchini zinaendelea na utekelezaji wa kusimika mfumo huo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Wizara hiyo kupitia kamati tendaji ya kutekeleza Mfumo huo imefanya kazi ya ziada kuhakikisha ajenda ya Mfumo huo inasikika, inaeleweka na inatekelezeka na imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 kila nyumba iwe na Anwani ya Makazi
“Sisi kama Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/22 tuna bajeti ya Halmashauri 17 tu za kusimika Mfumo wa Anwani za Makazi, lakini kila Mkurugenzi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ana bajeti ya kutekeleza Mfumo huu ila utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua hivyo tulikaa na kujipanga kuhakikisha kuwa utekezaji huu unafanyika katika Halmashauri
zote nchi nzima
Naye Bi. Elizabeth Mrema akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema kuwa Wizara hiyo inajukumu la kutafsiri mipaka ambayo imetangazwa na Serikali na kutengeneza ramani za mikoa, wilaya, viwanja vilivyopimwa na kumilikisha ardhi ambapo takwimu husika ndizo zinazotumika na zinakuwa ndio msingi wa kuwekewa Anwani ya Makazi na Postikodi
Naye Katibu wa ALAT Taifa Moses Kaaya ameipongeza Wizara husika kwa kuandaa semina inayohusu kwenda kutekeleza mfumo wa dunia wa Anwani za Makazi na Postikodi na kuwataka wenyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri kulipa suala hilo umuhimu kwa kuwa ni suala la msingi kwa maendeleo ya Taifa letu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula akizungumza wakati wa semina kuhusu utekelezaji na manufaa ya Anwani za Makazi na Postikodi katika kwa wajumbe wa ALAT inayojumuisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini iliyofanyika jijini Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Festo Dugange akizungumza wakati wa semina kuhusu utekelezaji na manufaa ya Anwani za Makazi na Postikodi katika kwa wajumbe wa ALAT inayojumuisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini iliyofanyika jijini Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe akizungumza wakati wa semina kuhusu utekelezaji na manufaa ya Anwani za Makazi na Postikodi katika kwa wajumbe wa ALAT inayojumuisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini iliyofanyika jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa ALAT Taifa Moses Kaaya akizungumza wakati wa semina kuhusu utekelezaji na manufaa ya Anwani za Makazi na Postikodi katika kwa wajumbe wa ALAT inayojumuisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini iliyofanyika jijini Dodoma
Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji (wa nne kulia walioketi) wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara hiyo baada ya ufunguzi wa semina ya Anwani za Makazi na Postikodi kwa wajumbe wa ALAT inayojumuisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini iliyofanyika jijini Dodoma
Baadhi ya wajumbe wa ALAT Taifa wakifuatilia semina ya Anwani za Makazi na Postikodi iliyotolewa kwao na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI; na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyofanyika jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...