Na Munir
Shemweta, BAHI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma
kuongeza kasi ya upimaji ardhi katika maeneo mbalimbali ili kuepuka ujenzi
holela.
Alisema, kwa sasa maeneo mengi katika
halmashauri hiyo yamepanuka kimji na hivyo kuhitaji kupangwa vizuri kwa
kuzingatia taratibu za mipango miji ili kuepuka ujenzi holela.
" Kwa sasa mji wa Bahi unapanuka kwa kasi
na cha msingi hapa ni kuwahi kupima maeneo na kama hakuna mpango basi mji huu
utakuwa na shida na cha msingi ni kuweka nguvu katika kupanga na kupima ili
usiwepo ujenzi holela" alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi alisema hayo tarehe 22
Sept 2021 wilayani Bahi wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi
katika halmashauri ya wilaya hiyo akiwa katika muendelezo wa ziara yake katika
wilaya za mkoa wa Dodoma.
Katika kinachonekana kuongeza kasi ya upimaji
ardhi katika wilaya ya Bahi, Naibu Waziri wa Ardhi aliagiza kuundwa timu ya
mkoa kwa ajili ya kupima takriban viwanja 8000 ilivyokwama kwenye zoezi
la urasimishaji makazi holela.
" Kwa kuwa makampuni yaliyokuwa yakifanya
urasimishaji makazi holela Bahi yameshindwa kukamilisha kazi kwa wakati naagiza
ofisi ya ardhi mkoa kukaa na mkurugenzi wa halmashauri ya Bahi iundwe na timu
ya mkoa ije hapa kwa gharama ya mkurugenzi ili kukamilisha upimaji"
alisema Dkt Mabula.
Aidha, Dkt Mabula ameitaka halmashauri ya wilaya
ya Bahi kuangalia namna ya kuwawezesha watumishi wa umma kwa kuwapatia viwanja
kwa makundi ili waweze kununua kwa kulipa kwa awamu.
" Muwawezeshe watumishi wa umma kuwa
na rasilimali ardhi kwa kuwaptia viwanja maana leo uko Bahi kesho uko eneo
lingine na zipo halmashauri zimefanya hivyo lengo kumuwezesha mtumishi kupitia
sekta ya ardhi katika kumiliki na kupata makazi" alisema Naibu Waziri wa
Ardhi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani
Dodoma Mwanahamisi Munkunda amemshukuru Naibu Waziri wa Ardhi kwa uamuzi wa
kuagiza kuundwa kwa timu ya mkoa kwa ajili ya kukamilisha ulipimaji wa zoezi la
urasimishaji.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ya Bahi ameomba pia
eneo la Zanka katika wilaya hiyo nalo kufanyiwa upimaji katika viwanja vyake
181 ambapo alisema kati ya viwanja hivyo ni 17 pekee ndivyo vilivyopimwa hasa
ikizingatiwa eneo hilo kwa sasa inakuwa kwa kasi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Bahi eneo la
Zanka ni eneo muhimu ambalo baadhi ya maeneo yake yameanza kuingia kwenye
migogoro ikiwemo ile ya kuuziana mara mbili na kusisitiza eneo hilo haliwezi kuachwa
bila ya kupimwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...