WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa amewaelekeza
watendaji wa ofisi yake kufanya ufuatiliaji ili kuwashusha vyeo Maafisa
Utumishi katika Taasisi za Umma walioshindwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia
Suluhu Hasssan la kuwapandisha vyeo watumishi wenye sifa za kupanda madaraja.
Mhe. Mchengerwa
ametoa maelekezo hayo leo wakati akifungua kikao kazi cha Watendaji Wakuu wa
Wakala za Serikali chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji hao kilichofanyika
katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Mhe. Mchengerwa
amesema, Afisa Utumishi yeyote aliyezembea na kusababisha Watumishi wa Umma
kutopandishwa madaraja achukuliwe hatua kwa kushushwa cheo na kuhamishwa kituo
cha kazi ili iwe ni fundisho kwa wengine wanaoshindwa kuwajibika ipasavyo.
“Fanyeni upembuzi na kuwaondoa
Maafisa Utumishi wote waliobainika kutotekeleza wajibu wa kuwapandisha madaraja
watumishi wenye sifa stahiki, kwani nimekuwa nikipokea malalamiko toka kwa
watumishi wa taasisi mbalimbali,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Ameongeza kuwa, ofisi
yake ilifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha taarifa za kiutumishi
zilizotumwa na waajiri zinafanyiwa kazi kwa lengo la kuwapandisha vyeo
watumishi husika, hivyo amewapongeza watendaji wa ofisi yake kwa kutekeleza vema
wajibu wao.
Mhe. Mchengerwa ameeleza
kuwa, Mhe. Rais anawajali sana Watumishi wa Umma na ndio maana alitoa agizo la
kuwapandisha vyeo katika kipindi ambacho mijadala ya bajeti Bungeni ilikuwa
ikiendelea jambo ambalo katika hali ya kawaida isingekuwa rahisi kutekelezeka.
“Mhe. Rais anatambua
kuwa nguzo ya Serikali kiutendaji ni Watumishi wa Umma hivyo haiwezi kufanya
vizuri iwapo haitowajali watumishi wake na ndio maana aliagiza wapandishwe
madaraja,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Akitoa neno la
shukrani kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa
Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Emmanuel Shindika amemshukuru Mhe. Waziri kwa
kukubali wito wa kukutana na Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali na kumuahidi
kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa.
Dkt. Shindika amemhakikishia
Mhe. Mchengerwa kuwa Watendaji Wakuu hao wa Wakala za Serikali watahakikisha
wanahimiza uwajibikaji kwa Maafisa Utumishi wao ili waendane na kasi ya
kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amehimiza uwajibikaji kwa Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali ili waweze kuendana na Kaulimbiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...