Na Said Mwishehe, Michuzi TV

TATIZO la dawa za kulevya lina madhara makubwa katika maisha ya wananchi,uwezo wa rasimali watu na maendeleo endelevu ya nchi yetu ya Tanzania na sote ni mashahidi kwani madhara kwa watumiaji wa dawa hizo yanaonekana hadharani, teja anajificha wapi bwana!

Kwa kutambua ukubwa wa athari zinazotokana na dawa za kulevya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kupambana na tatizo hilo kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama na hasa mapambano hayo yanatekelezwa kwa usahihi na weledi mkubwa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupmbana na Dawa za Kulevya nchini(DCEA).

Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya nchini kwetu inafika mwisho, imekuwa makini kudhibiti njia zote ambazo zinatumiwa na wafanyabiashara ya dawa za kulevya aidha kuingiza nchini au kupitisha dawa hizo kwenda nchi nyingine.Sote ni mashahidi angalau sasa biashara ya dawa za kulevya imepungua.

Katika kukomesha dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeendelea kuweka mikakati ya kudhibiti upatikanaji wa dawa za kulevya, kupunguza uhitaji wa dawa hizo, kupunguza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Katika mkakati wa kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya nchini , jukumu la msingi hapo ni kutoa elimu kwa jamii ili kujiepusha na matumizi ya biashara ya dawa za kulevya ambapo katika eneo hilo Mamlaka imeeleza kwa kina namna ambavyo imejipanga kutoa elimu kwa umma.

Tunafahamu kwa muda mrefu tangu Mamlaka ilipoundwa na kuuanza kazi rasmi imekuwa ikitoa elimu kupitia njia mbalimbali kwa jamii ya Watanzania, lengo la kuelimisha kuhusu madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya.Hata hivyo Mamlaka hiyo ipo kwenye mkakati mpya wa kutoa elimu kwa umma.

Katika mahojiano yaliyofanywa hivi karibuni kati ya Michuzi TV na Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi amefafanua hatua kwa hatua jinsi ambavyo wamekuwa wakitoa elimu kuhusu madhara na mikakati iliyopo katika kuhakikisha kuna na mpango mkakati wa kuifikisha elimu hiyo kwa Watanzania wengi zaidi.
" Katika kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya nchini Mamlaka imeendelea kutoa elimu ka wananchi kwamba jamii inakuwa na ufahamu mkubwa kuhusu tatizo la dawa za kulevya, inaelewa kuna madhara gani, na ikishakuwa na uelewa wataacha kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

"Watu wengi wanajiingiza kwenye dawa za kulevya kwasababu hawaambiwi madhara yake wanaambiwa,hawawakwambii kwamba ukitumia utakuwa mraibu wa hizi dawa za kulevya , utaathirika na kuwa teja.Ukianza kutumia unaambiwa wale mateja wanakula unga mchafu,matokeo yake watu wanajiingiza kwenye dawa za kulevya.

"Kwa hiyo sisi Mamlaka tunawaambia hakuna unga halisi(Original)wala mchafu, unga ni unga, ukitumia unafika kule waliko wale wanaonekana stendi wakiwa wachafu na muda wote wanasinzia hovyo.Vijana wanaotumiwa kusafirisha dawa za kulevya nao hawawaambia madhara yake , wanafichwa kuambiwa ukweli.Hawaambiwi kwamba dawa zinaweza kupasuka tumboni ukafa, hawaambiwi unaweza kukamatwa ukafungwa maisha au kunyongwa kama utakamatwa China,"amesema Dk.Mfisi.

,Hivyo katika elimu ambayo Mamlaka inaitoa kwa wananchi, inaeleza ukweli wa madhara ya kutumia dawa za kulevya na kwa kufanya hivyo wanaamini watapunguza idadi ya wanaokwenda kutumia dawa za kulevya ,watapunguza watu wanaokwenda kufanya biashara.

"Kwa mfano sasa hivi tunataka kuweka kwenye mtaala wa shule kuanzia darasa la tatu mpaka vyuo vikuu, somo la dawa za kulevya litakuwa linafundishwa na watu kufanya mitihani ili kuhakikisha kamba vijana wanafahamu madhara ya dawa hizo.Tunafahamu asilimia 90 ya watanzania wanapita kwenye mfumo wa shule kuanzia msingi, sekondari hadi chuo kikuu.
"Tukisikia wanaokwenda kuandikishwa shule ya msingi ni asilimia 99 tunakadiria asilimia hiyo yote wanakwenda kupata elimu, hivyo tukianza kutoa elimu kuanzia elimu ya msingi tutakuwa na jamii kubwa ambayo inaelewa madhara ya dawa za kulevya, hivyo wengi wataogopa kutumia kwani watakuwa wanajua madhara yake.

" Tunachoendelea kukifanya hivi sasa kabla ya kuanza kwa somo linalohusu madhara ya dawa za kulevya kuna majadiliano yanaendelea kati yetu na watalaamu wa mitaala ili baada ya hapo tuwe na kauli ya pamoja jinsi gani elimu hiyo itatolewa.Kuna njia mbili tunafikiria, kwanza kuangalia namna ya kuliweka kwenye masomo mengine maana kama litakuwa somo peke yake tutawabebesha mzigo wa masomo wanafunzi.
"Kwa mfano hata katika somo la uraia basi tunaweza kuongeza na somo la dawa za kulevya kulingana na kiwango cha elimu kinachotolewa kwa wanafunzi.Tutakachokifanya tutaongeza content kwenye hilo somo, lakini kama watakubali liwe somo linalojitegemea sisi tutafurahi zaidi,"amesema Dk.Mfisi.
Amefafanua ukiondoa mchakato wa kupeleka somo la madhara ya dawa za kulevya kuanzia elimu ya msingi,Mamlaka imekuwa ikitoa elimu katika maeneo mbalimbali kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, mabanga, maigizo ya sanaa, vikundi vya ngoma asili na njia nyingine ambazo wanaamini zinafikisha elimu kwa haraka.

Amesema katika kutoa elimu hiyo Mamlaka inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo kutoka taasisi binafsi na taasisi za Serikali.Tunazo taasisi nyingi zinatoa elimu kwa jamii kuhakikisha tunafikia watu wengi zaidi, tunajua sio watu wote wanasikilia redio na televisheni, hivyo tunatoa elimu kokote watu waliko, lengo kubwa ni kuwafikisha ujumbe kuhusu madhara ya dawa za kulevya ili wasijiingize.

Mbali ya kutoa mkakati wa kutoa elimu, Dk.Mfisi anaeleza Mamlaka inafahamu kwamba matumizi ya dawa za kulevya yanaambatana na matatizo mbalimbali, hivyo moja ya majukumu yao ni kupunguza madhara yanayosababishwa na dawa za kulevya.Upunguzaji wa madhara hayo umegawanyika sehemu mbili, sehemu ya kwanza kutoa elimu kwa watu wanaotumia dawa za kulevya.

"Watumiaji dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga wanapata maambukizi ya VVU lakini pia wanaambukizwa sana TB kutokana na yale mazingira wanayoishi.Tafiti zimefanyika, watumiaji dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga kati ya asilimia 26 hadi 44 wameathirika na UKIMWI. Kwa watumiaji wa dawa za kulevya wanawake wao wameathirika zaidi na UKIMWI, karibia asilimia 61 wameathirika na wanapoupata hawabaki nao wenyewe.

"Watumiaji dawa dawa za kulevya hawana haja na wanawake ,wenyewe starehe yao ni uunga, lakini wanatmbea na watu ambao sio watumiaji a dawa za kulevya ili wapate fedha za kwenda kununua unga.Kwa hiyo UKIMWI ambao tunasema ameupata kwa njia ya kujidunga atausambaza kwa mtu mwingine kwa njia nyingine.

"Kwa hiyo sasa tusipokuwa tunapunguza haya madhara tutaiangamiza jamii yote, watu wengine wanashangaa kwanini mnahangaika na hawa mateja?Lakini jibu ni kwamba tukiwaacha maana yake yale matatizo waliyonayo yanaingia kwenye jamii, wana matatizo mengi wabakaba ili wapate fedha za kununua unga, wanaiba ,wanafanya mambo mengi yasiyokubalika na jamii ya Watanzania ambayo imejaa kila aina ya ustaarabu.

"Kwa wanawake wanaojihusisha na dawa za kulevya wengi wao hufanya biashara ya ngono ili wapate fedha , na tunasema kundi hilo limeathirika kwa asilimia 61 nawanakuja kufanya ngono na watu wengine, hivyo UKIMWI kwenye jamii hautaisha, kwa hiyo kazi mojawapo ya Mamlaka yetu kuhakikisha inatoa elimu kwanza,"amesema Dk.Mfisi.

Akifafanua zaidi kuhusu mamlaka hiyo iliyoanza baada ya kutungwa sheria mwaka 2015 na ikaanza kutumika 2017,Dk.Mfisi anasema Mamlaka hiyo ilianzishwa ili kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, huko nyuma kulikuwa na Tume ambayo yenyewe ilikuwa inaratibu tu mapambano ya dawa za kulevya, hivyo ilikuwa haiwezi kufanya yenyewe.

"Ilikuwa haina uwezo wa kukamata, haiwezi kumfikisha mtuhumiwa mahakamani,kwa hiyo ilikuwa ni taasisi ambayo mapambano ya dawa za kulevya ilikuwa inategemea vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kwa mfano Polisi a baadae ikaundwa kikosi kazi na kazi ya tume ilikuwa kuratibu tu mapambano.Hivyo Serikali ikaona chombo hiki ni dhaifu na hakiwezi kumaliza tatizo,
"Kwa hiyo ilivyotungwa ile sheria ndio ikapatikana Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo ina imepewa nguvu zote, Tunapeleleza, tunawakamata, tunawapekuwa na kushikilia mali zao na tuna kibali na DDP kuendesha zile kesi mahakamani.Hivyo ni Mamlaka ambayo imekamilika na inauwezo mkubwa wa kupambana na dawa za kulevya.

"Mapambano hayo yanatekelezwa kwa kufauata nguzo kuu nne, nguzo ya kwanza tunapunguza uingiaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini, sasa hii inafanya kazi na divesheni tatu, divisheni ya kwanza ni ya Intelejinsia ambayo kazi yake ni kutafuta taarifa ya wauzaji wa dawa za kulevya na kujua mienendo yao ili waweze kukamatwa.

"Wakishakuwa na taarifa zao wanawapa wenzetu wa divisheni ya operasheni ambao hao wanakwenda kukamata na wakishakamata kesi inapelekwa mahakamani na ikifika mahakamani kuna divisheni ya sheria. Hawa intelejinsia wanatafuta taarifa, wakishakamlisha watu wa operesheni wanaenda wanakamata, na baadae hamakani na divisheni ya sheria inaendesha hizi kesi .


"Kwa hiyo ni muungano wa pamoja , kupunguza uingizaji, usambazaji wa dawa za kulevya nchini.Kuna nguzo nyingine ya kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya nchini na katika kupunguza mahitaji wanatoa elimu kwa wananchi.

"Nguzo ya tatu tunajua matumizi ya dawa za kulevya yanaambatana na matatizo mbalimbali, hivyo ndipo linapoingia jukumu la kupunguza madhara yanayosababishwa na dawa za kulevya.Tunafika mahali tunawatafuta wanaotumia dawa za kulevya na tunawashauri waachane na hiyo na kuapeleka kwenye matibabu, tunawapa bomba za sindano za kujidunga wakati tunawaelimisha waache.

"Nguzo ya nne uhusiano wa kimataifa, wafanyabishara wa dawa za kulevya hawana mipaka , mtu anauza dawa akiwa Tanzania lakini anauza katika nchi nyingine Hong Cong, China,Marekani na nchi nyingine mbalimbali.Kuna baadhi ya wafanyabiashara wa dawa hizo ukiwakamata unakuta Marekani wanasema huyo tunamtafuta,"amesema Dk.Mfisi.

Amefafanua kwa mazingira ya aina hiyo wakiona ushahidi mwingi uko Marekani basi mtuhumiwa anapelekwa huko hata kama ni Mtanzania, ni makubaliano tu ya kisheria kubadilishana watuhumiwa.

Katika eneo la ukamataji wa watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya kwa mujibu wa Dk.Mfisi ni kwamba hakuna taarifa ya idadi kamili , ingawa taarifa ya hali ya dawa za kulevya mwaka 2018 ilionesha waliokamatwa walikuwa zaidi ya Watanzania watanzania 1000 ambao walikuwa wamekamatwa nchi mbalimbali wakijihusisha na dawa za kulevya.

"Kwa hiyo wanaweza kuwa wameongezeka au wamepungua, sababu kubwa wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya hawana mipaka na ili kuwadhibiti wafanyabiashara hao lazima tuwe na ushirikiano na wenzao.Tunafanya kazi na mashirika mbalimbali wanaojihusisha na mapambano ya biashara ya dawa za kulevya.Lengo letu ni kuhakikisha tunawadhibiti".

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...