Na Damian Kunambi, Njombe.

Ikiwa ni wiki kadhaa zimepita tangu naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya kutembelea eneo la daraja la mto Ruhuhu akiwa sambamba na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ambapo wananchi wa kata ya Ruhuhu waliwasilisha kilio chao cha kuomba kumaliziwa kwa daraja hilo hatimaye serikali imeanza mchakato kwa kuwasilisha vyuma vitakavyotumika katika ujenzi huo.

Vyuma hivyo ambavyo vinatarajiwa kuanza kufungwa ndani ya miezi miwili na kukamilisha daraja hilo imekuwa ni furaha kubwa kwa wananchi hao pamoja na wamilikiki wa mabasi ambao wamekaa tayari kwa kusafirisha abiria na kuongeza masafa zaidi.

Emmanuel Mgaya ni miongoni mwa wamiliki wa mabasi hayo ambayo yanatarajia kusafirisha abiria na kuongeza masafa amesema fursa hii wamekuwa wakiisubiri kwa kipindi kirefu hivyo wanaiomba serikali ikamilishe ujenzi huo kwa wakati ili kuweza kufungua njia.

Amesema kwa sasa wanasafirisha abiria kutoka wilaya ya Nyasa mpaka mpakani mwa wilaya ya Ludewa ambayo inatenganishwa na mto ruhuhu na kuwalazimu abiria kuvuka mto kwa kutumia mtumbwi ambapo endapo lingekuwepo daraja wangeweza kusafiri kwa gari kwa umbali mrefu zaidi.

Naye Adam Ngatunga ni miongoni mwa wakazi wa kata hiyo amesema kwa asilimia kubwa mahitaji yao ya msingi wanategemea kutoka upande wa Ruvuma hivyo daraja hilo litakapokamilika wataweza kupata huduma na kusafirisha biashara zao kwa urahisi zaidi.

"Huwa tunapata changamoto kubwa hasa tunapokuwa na wagonjwa mahututi au mama mjamzito, watu wamekuwa wakifia kwenye mitumbwi na wajawazito kujifungulia humo humo kitu ambacho kinaleta fedheha kwetu hivyo kwa hatua hii iliyofikiwa na serikali ni matumaini yetu ujenzi huu utakamilika mapema na suala la wananchi kuliwa na Mamba wanapovuka mto ikawa ni historia", Amesema Ngatunga.


Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ombi lake ambalo alikuwa akilipambania bungeni kwa nguvu zote.

Amesema daraja hilo lina umuhimu mkubwa sana kwa wananchi wake na litakapokamilika litafungua fursa nyingi za kiuchumi kwani kutaruhusu muingiliano wa watu kwakuwa magari ya kwenda mikoa na wilaya za jirani yatapita hapo.

"Naishukuru serikali kwa kusikia kilio changu na wananchi hawa, natumai mpaka kufikia mwezi Desemba daraja hili litakuwa limeshaanza kutumika hivyo wananchi wangu sikukuu ya Christmas ya mwaka huu mtaisherehekea mkiwa na daraja", Amesema Kamonga.

Basi la abiria la SABAS likiwasili eneo la mto ruhuhu tayari kwa kushusha abiria kutoka wilaya ya Nyasa na kisha kupanda mtumbwi kuelekea wilaya ya Ludewa


Kontena lililobeba vyuma vya kufungia daraja la mto Ruhuhu vikishushwa ili kumalizia ujenzi wa daraja hilo.
Baadhi ya vyuma vya kufungia daraja la mto ruhuhu vikiwa vimeteremshwa kwenye kontena

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akipokelewa kwa shangwe na wananchi wa kata ya Ruhuhu alipofanya ziara katika kata hiyo
Baadhi ya wakazi wa kata ya Ruhuhu wilayani Ludewa wakishusha bidhaa zao kwenye mitumbwi walizotoka kununua wilaya ya Nyasa

 Katibu wa chama cha mapinduzi wilayani Ludewa Bakari Mfaume akiwa ndani ya mtumbwi akielekea upande wa Nyasa ambako kumehifadhiwa vifaa vya ujenzi vya dara mto ruhuhu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...