Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imesema haitomvumilia mtumishi yeyote wa umma ambaye atafanya uzembe kazini huku ikiwataka kuacha kulegalega na kushindwa kutekeleza wajibu wake ambapo imesisitiza kwamba lengo lake ni kuendelea kuwatumikia watanzania kwa kasi kubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi wakati alipokua akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

Ndejembi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia imeonesha jitihada kubwa ya kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuwapandisha madaraja, kuongeza mishahara na kulipa malimbikizi ya madai yao huku akiwataka watumishi nao kuacha uzembe na kutanguliza maslahi ya umma mbele.

"Ofisi ya Rais Utumishi haitosita kumchukulia hatua mtumishi yeyote ambaye analegalega na kufanya uzembe kazini, hatutosita kumchukulia hatua yeyote iwe kwenye Barabara, Afya au Maji kwa sababu Wizara yetu inahusika na watumishi wote, iwe Kilimo, Elimu na kwingineko kote tutakapokuta kunalegelega tutachukua hatua.

Rais Samia anatekeleza kwa vitendo azma ya Serikali kuwajali watumishi wake, Wilaya ya Hai jumla ya watumishi 825 wamepata promosheni katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai na kati ya hao 31 wamebadilishiwa kada ambayo ni mambo waliyokua wanalilia muda mrefu sana lakini pia watumishi 459 tumeshawalipa malimbikizo yao waliyokua wanadai, hivyo kwa hatua hizi za Serikali niwatake mchape kazi kwelikweli," Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Naibu Waziri Ndejembi amesema utendaji bora wa watumishi wa umma ndio unaowapa imani wananchi kwa Serikali yao hivyo wao kama Wizara inayohusika na watumishi haitoruhusu kuona mtumishi yeyote anavunja imani ya wananchi kwa Serikali yao.

" Utendaji kazi wenu ndio unaoleta imani ya wananchi kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla, Sasa nyinyi mkilegalega imani ya wananchi kwa serikali nayo itapungua hivyo niwaombe mzidishe kasi ya kuwatumikia watanzania ambao wana imani na Serikali yao," Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Ziara hiyo ya siku tatu mkoani Kilimanjaro ililenga kuzungumza na watumishi wa umma ambapo Naibu Waziri Ndejembi alizungumza na watumishi wa Manispaa ya Moshi, Halmashauri ya Moshi na Halmashauri ya Hai pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na Mkurabita na kuzungumza na waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Mkoa wa Kilimanjaro.

 

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na watumishi kada mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambapo amesisitiza kuwa Serikali haitomvumilia mtumishi yeyote mzembe.
Watumishi wa kada mbalimbali Katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi alipofika kuzungumza nao leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...