Na Joseph Lyimo
WACHIMBAJI
wa madini ya Tanzanite na wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kupatiwa chanjo ya covid-19 na
kuepuka na maneno potofu ya mitandaoni kuwa watageuka kuwa mazombi.
Mchimbaji
wa madini ya Tanzanite Juma Seif amesema dhana potofu zinazotolewa na
baadhi ya watu zinapaswa kubezwa kwani serikali haiwezi kuwaletea tatizo
kwenye suala la afya ya watanzania.
“Tuondokane
na dhana potofu zinazotolewa na watu wasio na uelewa juu ya chanjo na
kuzusha kuwa mara baada ya kuchanjwa utageuka kuwa zombi au mtu wa
kutisha,” amesema Juma.
Amesema
amepata chanjo ya covid-19 kwenye kituo cha afya Mirerani Agosti 8
mwaka huu na hajapata kupata madhara yoyote baada ya zoezi hilo.
Amesema
wadau wa madini wanatakiwa kupata chanjo ili hata ikitokea bahati mbaya
anapata maambukizi ya corona hapati maumivu makubwa kwa sababu
alishapatiwa chanjo.
Mjumbe
wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, MAREMA Tawi la
Mirerani, Japhary Matimbwa amesema wadau wa madini ya Tanzanite
wanatakiwa kuchanja na kuachana hofu na dhana potofu.
Matimbwa
amesema dhana kuwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania hayati John Pombe
Magufuli aligoma chanjo kutumika hapa nchini siyo ya kweli kwani alitoa
agizo uchunguzi ufanyike kwanza ndipo chanjo itumike.
Amesema
mara nyingi watanzania huwa wanawalisha maneno marehemu ambayo hawapo
hivyo haitakiwi kuzungumza maneno mengi zaidi ya kupata chanjo.
“Hili
suala la kusema marehemu alisema hivi akasema vile huwa ni kisingizio
tuu mbona marehemu wengine wanasema nikifa mke wangu asiolewe ila baada
ya miezi sita anaolewa na wengine wanasema nikifa nyumba yangu msiuze na
baada ya mwaka watoto wanauza na kugawana pesa,” amesema Matimbwa.
Ameongeza
kuwa wadau wa madini wanatakiwa kupata chanjo japokuwa wengine
wangeweza kukimbilia chanjo hiyo endapo wangeambiwa ni chanjo ya ukimwi.
“Waachane
na maneno ya kwenye vijiwe, serikali haiwezi kuwaletea sumu na
tumeshapewa maelezo na wataalamu kuwa chanjo hii ni nzuri na haina
tatizo lolote nipo sawa baada ya chanjo,” amesema Matimbwa.
Amesema
yeye amechanja Agosti 6 mwaka huu kwenye kituo cha afya Mirerani hivyo
anawaasa wananchi wa eneo hilo wakapate chanjo ili kupambana na janga la
corona.
Mganga mfawidhi
wa kituo cha afya Mirerani Dkt Deogratius Mazengo amesema wakazi
mbalimbali wa eneo hilo wamejitokeza kupata chanjo ya covid-19 katika
kituo hicho.
Dkt Mazengo
amesema kwenye wilaya ya Simanjiro kuna vituo vitatu vya kupatiwa chanjo
vya Mirerani, Orkesumet na Naberera, hivyo wananchi washiriki zoezi
hilo.
“Mwitikio wa watu ni
mzuri na wengine wanatoka wilaya za jirani za Arumeru mkoani Arusha na
Hai mkoani Kilimanjaro hivyo wananchi wa eneo hilo wafike kupata huduma
hiyo,” amesema Dkt Mazengo.
Amesema
chanjo hizo ni salama zimedhibitishwa na shirika la afya duniani WHO na
serikali ya Tanzania imezipitisha rasmi kutumika kwake.
Amesema
tangu wameanza kutoa chanjo hiyo hakuna mtu aliyepata madhara hivyo
wananchi wajitokeze kupata chanjo hiyo ambayo ni salama na
anawakaribisha sana.
Amesema
chanjo hiyo inatolewa kwa watu wenye kuanzia umri wa miaka 18 na
wanawake wajawazito wanapaswa kusubiri kwanza hadi wajifungue.
Mwenyekiti
wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo, amewahamasisha
wananchi wa eneo hilo kuchanja na kuondokana na dhana potofu kuwa.
“Tusiwe
na maneno mengi ambayo siyo yakitaalamu ukiona hata Rais Samia Suluhu
Hassan amechanja na kuzindua zoezi hili na hakuna kiongozi anaweza kuua
watu wake,” amesema Kobelo.
Amesema
hata Dkt Mwele Malecela ambaye ni mtaalamu wa afya aliyepo nje ya nchi,
amekuwa akitoa elimu ya afya kuhusiana na chanjo na ameelimika juu ya
chanjo hiyo hivyo wadau wa madini wakashiriki kuchanja.
Mkuu
wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere akizungumza na waandishi
wa habari hivi karibuni mjini Babati amesema wamepokea kiasi cha dozi
15,000 za chanjo za covid-19.
Makongoro
amesema maeneo mbalimbali ya hospitali, vituo vya afya na zahanati, za
wilaya tano za mkoa huo za Babati, Simanjiro, Mbulu, Hanang’ na Kiteto,
zimepatiwa chanjo hizo.
“Wananchi
wanatakiwa kushiriki kikamilifu kupata chanjo hizo kwani serikali
imeshafanikisha kuzisambaza maeneo mbalimbali ya mkoa wetu,” amesema
Makongoro.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...