Na Mwandishi wetu, Geita
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuimarisha taasisi zake hususan Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili ziweze kutoa huduma bora na nafuu kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na uchorongaji wa miamba ili kujua uwepo na wingi wa mashapo.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua Maonesho ya nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayozishirikisha sekta za madini yanayofanyika Mkoani Geita na kwamba hatua hiyo, itasaidia wachimbaji wadogo kuendesha shughuli zao kwa tija na uhakika na hivyo, kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
"Natoa mwito kwa wachimbaji kutumia taasisi hizi ili kupata taarifa za mashapo ya madini na kuchimba kwa uhakika. Katika hili, ninaielekeza Wizara ya Madini kuhakikisha suala la local content linasimamiwa kikamilifu. Aidha, kampuni yote makubwa yatumie huduma za GST na STAMICO ispokuwa pale ambapo itathibitika wameshindwa ndipo waagize nje,amesema.
Pia amesema sekta ya madini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na maendeleo ya mtu mmoja mmoja nchini na matarajio ya Serikali ni kuongeza zaidi mchango huo kupitia shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji madini, usanifu madini na utoaji wa huduma katika shuguli za madini.
"Lengo la Serikali ni kufungamanisha ustawi wa sekta ya madini ili uchangie kukua kwa Sekta nyingine za kiuchumi na huduma zikiwemo viwanda, ujenzi, usafirishaji, mawasiliano na nishati,"amefafanua.
Awali Waziri Mkuu alipata nafasi ya kuyatembelea baadhi ya mabanda ya wadau wa sekta ya madini ambapo alipata fursa ya kushuhudia namna wachimbaji wadogo wanavyofanya shuguli zao na hivyo kutoa mwito kwa wachimbaji hao na wadau wote kwa ujumla kutumia vizuri fursa ya maonesho hayo.
Maonesho hayo ambayo yamefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na yanatarajiwa kufungwa Jumapili ya Septemba 28 mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...