Na Said Mwishehe, Michuzi TV
Fuatilia
historia ya kijana Ahmed Khatibu maarufu Ahmed Zolla ambaye kwa sasa
anaishi mkoani Morogoro ni miongoni mwa Watanzania walioamua kwa hiyari
yao kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
Khatibu
alizaliwa mwaka 1982 visiwani Zanzibar alianza kujihusisha na utumiaji
wa dawa za kuelevya akiwa na umri wa miaka 14, alianza kujihusisha na
dawa za kulevya kwa lugha rahisi akiwa mtoto. Kwa Tanzania mtoto ni yule
aliyekuwa na umri chini ya miaka 18, Inasikitisha.
Tunafahamu
changamoto wanazopitia watumiaji wa dawa za kulevya, wanapitia magumu
mno, wanaishi maisha ya kutoaminika kutokana na aina ya tabia ambazo
watumiaji wengi wa dawa za kulevya wanazo.
Anayetumia dawa za kulevya kuiba, kupora, kukaba na kufanya kila aina ya matendo ya hovyo ni jambo la kawaida.
Ndio
nawazungumzia watumiaji wa dawa za kulevya ambao wengine tunapishana
nao barabarani, wachafuuu. Unajua kwanini wanakuwa wachafu? Jibu ni
kwamba wakioga wanaondoa Stimu, hivyo hawako tayari kuiondoa yaaani
atumie fedha kuipata halafu kirahisi tu aiondoe kwa kuoga, kwake hapana,
hayuko tayari.
Kijana
Khatibu amepitia maisha yote wanayoishi Waraibu, anaeleza hatua kwa
hatua jinsi ambavyo aliishi wakati anatumia dawa za kulevya.
Aliishi maisha ya hovyo sana, alipora,aliiba na wakati mwingine alilazimika kudanganya.
Aina
ya maisha aliyopitia , ndiyo yaliyomfanya kwa hiyari yake kuamua
kuachana na utumiaji wa dawa za kulevya, ameamua kuwa shuhuda wa
kueleza magumu na machungu aliyopitia , hataki kurudi nyuma na moyo wake
umebaki na machungu kutokana na jinsi ambavyo ameishi maisha ya hovyo,
anaumia kwa muda alioupoteza.
Kupitia
makala haya maalum ,Khatibu anafafanua hatua kwa hatua alivyoingia
kutumia dawa za kulevya na hadi alipoamua kuacha kutumia dawa
hizo."Niliingia katika utumiaji wa dawa za kulevya kutokana na kukaa
vijiweni na maskani.
"Kwa
sasa nimeacha , nimekuwa nikihamasisha vijana wengine kuacha, nimeamua
kuanzisha Sober House mkoani Morogoro, inaitwa Free at Last Sober House
na huu ni mwaka wa nane nipo Morogoro naendelea na kazi hii.
Kuhusu
athari za dawa za kulevya Khatibu anaeeleza zipo nyingi, ukiondoa
watumiaji wengi wa dawa za kulevya kuwa na HIV na TB, pia kuna madhara
mengine mengi ya kiafya, mtumiaji wa dawa za kulevya ni rahisi kupata
magonjwa yasiyoambukiza .
"Nimepata
strock ( kupooza ) mkono kwasababu ya kutumia dawa za kulevya,wakati
natumia nilikuwa najidunga sindano, hivyo imekwenda kuua mishipa ya
mkono na kunifanya nipooze, kuna wengine wameathirika HIV kwasababu ya
kuchoma sindano. Wapo ambao wamepata TB,"anaeleza.
Katika
kuhakikisha anajiondoa kwenye utumiaji wa dawa za kulevya ametumia njia
mbalimbali ,alikwenda hospitali lakini hakuweza kuacha kwasababu
hakupata elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya."Niliacha baada ya
kwenda Sober House, nilipata elimu ya kutosha, nashukuru Mungu nimeacha
na sasa nahamasisha wengine kuacha.
"Lakini
katika kuacha huko pia nilifuata hatua 12 ambazo ni kanuni rahisi ya
kumsaidia anayetumia dawa za kulevya, hatua ya kwanza ni kufungua akili
kwamba nataka kuacha , pili nia ya kweli. Ninachoweza kueleza kabla ya
kuingia katika hizo hatua unachotakiwa kukifanya ni kuwa muwazi na uwe
na hamu ya kile unachotaka kufanya,"anasema Khatibu.
Akifafanua
zaidi anasema pamoja na kuacha kutumia dawa za kulevya,changamoto kubwa
ni kuaminika katika jamii, ni ngumu jamii kuamini kama
umeacha."Nimetumia dawa kwa miaka 12 , sasa kumtengenezea mtu imani ni
changamoto, hivyo nia inabaki kwao mwenyewe, ukiaminiwa au usipoaminiwa
unakuwa mwenyewe."
Pamoja
na hayo anaeleza katika Sober House nyingi kinacholiwa ni mboga za
majani, ugali na maharage na hivyo ndivyo vyakula ambavyo vinamuwezesha
aliyekuwa anatumia dawa za kulevya kupata afya na nguvu."Tunakula hivyo
vyakula tu lakini ladha haipo mdomoni."
Aidha
Khatibu anasema kuwa changamoto nyingine anayokutana nayo mtumiaji wa
dawa za kulevya anapoamua kuacha kutumia ni maradhi."Unapoacha kutumia
dawa za kulevya kuna maradhi mengi yanaibuka mwilini,lakini nashauri
vijana na Watanzania kuachana na kutumia dawa za kulevya."
BAADA YA KUACHA
Khatibu
anasema hivi " Baada ya kuacha dawa za kulevya imenichukua miaka mitano
nikaingia hatua ya pili kuoa, na ndugu zangu niliwaambia nataka kuwa
mtu mzima na moja kwa moja wakaamini nimebadilika, nimetumia dawa za
kulevya kwa miaka 12, nilianza nikiwa na miaka 14 tangu unga ukiwa bure.
"Nakumbuka
kuna mabraza walikuwa wanatoka Ulaya wanakuja maskani kule Zanzibar na
mimi nikawa napenda kuwa nao na walikuwa wanakuja na zawadi, hivyo
nikajiukuta naingia kwenye kutumia na nakumbuka kete moja nilikuwa
nanunua sh.200, sasa hivi inauzwa shilingi 5000 hadi sh.6000, nilianza
kutumia mwaka 1994.
"Kwa
hiyo kuingia ilikuwa rahisi lakini kutoka ikawa shida, nakumbuka
nilikuwa nacheza sana mpira hivyo nilikuwa na mashibiki wengi, leo
najutia nimepoteza kipaji changu cha mpira.Wito wangu kwa vijana wengine
kuishi bila kutumia dawa za kulevya inawezekana kwani hata mie
imewezekana.
"Jambo
la pili vijana wasijaribu kuiga, hata mimi huko awali nilikuwa na fedha
nyingi, nilikuwa namiliki gari yangu aina ya Toyota, nilikuwa na
kiwanja ambacho nilinunuliwa kutokana na uwezo wangu wa kucheza mpira,
nilikuwa napata hela kupitia mpira.
"Cha
ajabu kadri siku zilivyokuwa zinaenda nikawa ninajiibia mwenyewe, ukiwa
mteja unajiibia mwenyewe, unakuwa na kiatu kizuri unauza, unakuwa na
simu unaona haina maana unauza, hivyo nilikuwa naidanganya nafsi yangu
mwenyewe, hadi mwisho nikaanza kuuza viti vya nyuma vya gari yangu.
"Alikuja
jamaa yangu akaniambia gari yake viti vya nyuma watu wanalalamika
wanaumia,hivyo akaniambia nimuuzie vyangu , kweli nikauza , nilianza tu
kwa taratibu lakini mwisho nikauza na gari yangu kwa Sh.650,000 tu
wakati gari niliinua Sh.milioni 3.5.Hakuna mteja anayeanza kumuibia mtu,
mteja cha kwanza ataanza kujiibia mwenyewe, nimeuza nguo, nimeuza kila
kitu na kibaya zaidi nimeuza nafsi yangu,"amesema Khatibu.
Anaongeza
kwa sasa moyo wake unaumia sana, hasa akikumbuka aliyopitia huko awali
wakati anatumia dawa za kulevya, na kibaya zaidi akikumbuka aliyopitia
na sasa moyo wake umekuwa na wivu, anatamani awe na maisha mazuri
kushinda mwanzo.
"Lakini
changamoto iliyopo ni kwamba walioacha kutumia dawa za kulevya
hawaamini, kwangu nashukuru nimesimama imara, nahamasisha wengine
waache, hivyo kila nikipata nafasi ya kuzungumza na Watanzania
nawahamasisha kuacha kutumia dawa za kulevya," anasema Khatibu , kijana
mpole,mcheshi, mtaratibu ambaye kwa sasa anaishi maisha huru baada
kuachana na kutumia dawa za kulevya.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...