Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KLABU ya Barcelona ya Hispania rasmi imefika makubaliano na Beki wake wa zamani Mbrazil, Dani Alves kurejea katika timu hiyo kwenye Kikosi cha wakubwa msimu huu, Alves atajiunga na Barca lakini hatoruhusiwa kucheza kwa sasa hadi mwezi Januari mwakani.
Alves anakutana na Kocha Xavi Hernández ambaye alicheza naye FC Barca, hivi karibuni akipewa jukumu la kukinoa Kikosi hicho, Kupitia Tovuti yao rasmi, FC Barcelona wamethibitisha kurejea kwa Beki huyo akitokea katika Klabu ya nchini kwao Brazil ya São Paolo.
“Nimerejea Barcelona, nipo nanyi, nimefurahi kurejea nyumbani, natarajia kuwaona wote muda si mrefu. Tufurahi na tuijenge timu hii tunayoipenda”, amesema Dani Alves kupitia kipande kifupi cha video alichoweka kwenye kurasa za Mitandao yake ya kijamii
Alves anayesifika kucheza nafasi ya Beki wa pembeni na kushambulia mithili ya Winga, ametajwa na Klabu hiyo ya Barcelona kuwa alikuwa kipenzi cha Makocha waliopita katika timu hiyo, wakiwemo Pep Guardiola, Tito Vilanova, Tata Martino na Luis Enrique, licha ya kuwa kipenzi cha Mashabiki wengi wa Klabu hiyo yenye maskani yake mjini Catalania.
Baada ya kuitumikia Juventus msimu mmoja wa 2016-2017, Alves aliondoka kwenye Klabu hiyo na kujiunga na Paris Saint-Germain ambapo alicheza misimu miwili na baadae alijiunga na São Paulo kabla ya kurejea tena FC Barcelona msimu huu wa 2021-2022.
Dani Alves alicheza Barcelona tangu msimu wa 2008-2009 hadi 2015-2016 akitokea katika Klabu ya Sevilla FC ya Hispania alipotumikia miaka mitano, na akiwa na misimu Nane ndani ya Barca alicheza michezo rasmi 391 na kufunga mabao 23 pekee.
Alves amecheza timu ya taifa ya Brazil, akifanikiwa kutwaa mataji Sita, hivi karibuni ametwaa Taji moja kubwa la Tokyo Olympic Games, Japan katika mchezo wa Fainali akicheza dhidi ya Nyota Òscar Mingueza, Éric Garcia and Pedri wakiwa na timu ya taifa ya Hispania ambao kwa sasa atakuwa nao kwenye Kikosi cha Barca.
Kwa jumla ameshinda mataji 23 akiwa na FC Barcelona: mataji 6 Ligas, 4 Copas del Rey, 3 Champions League, 3 Club World Cups, 3 Spanish Super Cups na 4 European Super Cups. Pia ametwaa mataji na Juventus (2), Paris Saint-Germain (6) na São Paulo (1) kabla ya kutejea Catalonia. Amewahi kushinda mataji akiwa EC Bahia (3), Sevilla (5) na Brazil (6), akitajwa kuwa Mchezaji mkongwe mwenye mataji 46.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...