SHIRIKA la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Shirika la Reli Tanzania (TRC) wamekubaliana kutekeleza mradi wa utafiti wa ukusanyaji wa data na uboreshaji wa usafiri wa reli za abiria jijini Dar es Salaam kuanzia mwezi huu.
Kwa
mujibu wa mkutano wao wa kwanza uliofanyika Novemba 4, 2021 jijini Dar es
Salaam, utafiti huo wa miezi minne unaotarajia kukamilika Februari 2022, utachunguza
miundombinu ya reli za abiria zilizopo Dar es Salaam (reli ya Pugu na Ubungo)
na kupendekeza hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu hiyo.
Mkutano
huo uliohudhuriwa na washiriki 18 kutoka Ofisi ya JICA Tanzania, Wizara ya
Ujenzi na Uchukuzi, TRC na Washauri kutoka Japani na Tanzania walipendekeza
mpango wa uboreshaji wa ufuatiliaji wa uendeshaji wa reli, uwekaji ishara,
usafirishaji wa bidhaa, ujenzi wa stesheni katika vituo, majengo ya biashara
katika stesheni na namna bora ya kutoa huduma ya usafiri katika njia za treni
za abiria zilizopo.
Timu
ya watafiti iliyoundwa, itajadiliana na maafisa wa serikali ya Tanzania ili
kurekebisha Mpango Kabambe wa Usafiri wa Mijini wa Dar es Salaam wa mwaka 2018,
ambao ulifadhiliwa na JICA.
Mpango
huo kabambe unakadiria kwamba Dar es Salaam itakuwa na zaidi ya watu milioni 10
mapema mwaka 2030, hivyo usafiri wa barabara pekee hautaweza kutoa usafiri wa
uhakika na kuondoa kero ya msongamano wa magari (foleni) na kutumia muda mrefu
wa kusafiri ndani ya jiji hilo.
Mkutano
huo pia ulipendekeza namna bora ya uboreshaji wa mfumo wa reli uliopo kwa ajili
ya maendeleo ya usafiri na mipangilio mizuri yenye uwiano.
Mikutano
zaidi ya majadiliano itaendelea kufanyika kila inapohitajika, hadi kukamilika kwa
utafiti huo mnamo Februari 2022.
Shirika la la Maendeleo la Kimaitaifa la Japani (JICA) limekuwa likisaidia sekta ya uchukuzi kwa zaidi ya miaka 40 hapa Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...