Na Projestus Binamungu,WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amewakabidhi Bendera ya Taifa, timu ya Taifa ya mchezo wa Netiboli (Taifa Queens) kama baraka na kheri katika mashindano ya kombe la Netiboli kwa nchi za Afrika yanayotarajiwa kufanyika nchini Namibia kuanzia Novemba 9, 2021.
Waziri Bashungwa amewakabidhi bendere hiyo leo Novemba 6, 2021 jijini Dar es Salaam akiwasisitiza kutambua dhamana waliyoibeba kwa niaba ya watanzania wote.
Waziri Bashunhgwsa amesema Serikali itaendelea kuwekeza nguvu, juhudi, maarifa na fedha katika kukuza kila aina ya michezo akiutaja mchezo wa netiboli kuwa ni miongoni mwa michezo sita iliyopewa kipaumbele na Wizara yake.
“Mkifanya vizuri huko hiyo ni furaha ya nchi, na mkifanya vibaya ni fedheha ya nchi, kwa maandalizi mliyoyafanya sisi kama taifa tunawaamini na tunaamini mtafanya vizuri, naomba niwaahidi kwamba siku mnaporejea hapa nchini mkiwa na kombe letu mikononi, nitakuja kuwapokea uwanja wa ndege kwa namna ya kipekee “ alisema waziri Bashungwa.
Awali akiongea na wachezaji wa timu hiyo Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Neema Msita amewataka wachezaji hao kuthamini hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa kiasi cha fedha, zaidi ya shilingi milioni 60 ili kugharamia usafiri na malazi ya wachezaji huko nchini Namibia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) Dkt. Devotha Marwa ameipongeza Serikali kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kuwezesha timu hiyo kushiriki katika mashindano hayo ya kimataifa akisema huo ni mwanzo mpya katika kuupaisha mchezo wa netiboli hapa nchini.
Timu ya Taifa ya mchezo wa Netiboli (Taifa Queens) inatarajiwa kuondoka nchini Novemba 7, kuelekea nchini Namibia kushiriki mashindano ya kombe la Netiboli kwa nchi za Afrika ikiwa na matumaini kemkemu ya kuibuka bingwa katika mashindano hayo kutokana na maandalizi aliyoyafanya.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akimkabidhi bendera ya taifa kapteni wa timu ya Taifa ya mchezo wa Netiboli (Taifa Queens) Mwanahidi Ngubege kama ishara ya kuwatakia kila la kheri katika mashindano ya kombe la Netiboli kwa nchi za Afrika yanayotarajiwa kufanyika nchini Namibia kuanzia Novemba 9, 2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...