Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo, anayesimamia nchi tisa za Afrika katika Benki hiyo, ambazo ni Tanzania, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Eritrea, Somalia na Uganda, akipewa maelezo na Mhandisi Mshauri, Jailos Chilewa, utekelezaji wa mradi wa Maji wa Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 520, alipomtembelea mradi huo.



Na. Peter Haule, WFM, Arusha

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeridhishwa na kasi utekelezaji wa mradi wa maji katika jiji la Arusha kwa gharama za shilingi bilioni 520 zilizotolewa kwa njia ya mkopo wa masharti nafuu na benki hiyo.

Hayo yamebainishwa jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anaesimamia nchi  tisa za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Eritrea Uganda na Somalia, katika Benki hiyo Bw. Kipronoh Amos Cheptoo, wakati alipotembelea na kukagua Mradi wa Maji wa Arusha ikiwa ni ziara yake ya kukagua miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.

“Nimeridhishwa na kasi na umadhubuti wa utekelezaji wa mradi wa maji jijini Arusha unaofadhiliwa na Benki AfDB na ninaipongeza Serikali kwa kuwekeza katika Sekta ya Maji ambayo ni muhimu katika maendeleo ya nchi yeyote duniani ambayo pia hupunguza magonjwa yanayohusiana na maji”, alieleza Bw. Cheptoo.

Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia wananchi wa Tanzania hususani katika wakazi wa jiji la Arusha, watakao nufaika na mradi huo.

 Aidha ameishukuru Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Arusha (AUWASA) kwa kuhakikisha wanafanya jitihada za kukamilisha mradi huo kwa wakati ifikapo mwezi Juni mwaka huu kwa kuwa kazi kubwa tayari imefanyika.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi. Nadhifa Kemikimba, amewashukuru wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kusaidia katika upatikanaji wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 520 za kutekeleza mradi wa Maji Arusha ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini ukitanguliwa na mradi wa Maji wa Tabora Zenga uliogharimu shilingi bilioni 620.

Alisema utekelezaji wa mradi huo umewezekana kutokana na ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika na pia Wizara ya Fedha na Mipango kuweka usimamizi madhubuti wa Fedha za Mradi na kusaidia mradi huo kutekelezwa ndani ya muda uliopangwa kwa kuwa unatarajiwakukamilika mwezi Juni mwaka huu.

“Tunaahidi tutasimamia mradi huu katika maeneo yaliyosalia na kufikia mwezi Juni mwaka huu mradi utakuwa umekamilika kama ulivyopangwa kwa kuwa tukipata fedha hatuleti mchezo tunafanya kazi iliyokusudiwa ndio maana Mkurugenzi wa AfDB na wajumbe wake kila walipotembelea wamepongeza kazi kubwa iliyofanyika”, alisema Mhandisi Kemikimba.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Arusha (AUWASA), Mhandisi. Justine Rujomba, amesema kuwa kwa muda mrefu jiji la Arusha lilikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, lakini sasa kiwango cha upatikanaji maji kimepanda kutoka lita milioni 40 hadi zaidi ya lita za ujazo milioni 60 kwa siku kutokana na matunda ya mradi huo.

Amesema kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 80 na tayari umeaanza kutoa huduma katika baadhi ya maeneo ambayo yamekamilika ambapo kwa upande wa maji safi zaidi ya visima 15 vinatoa huduma na upande wa maji taka tayari huduma ya kutoa maji taka katika jiji la Arusha inafanyika.

Aidha amewapongeza wakazi wa jiji hilo kwa kuwa wavumilivu hususani katika kipindi cha utekelezaji wa mradi kwa kuwa kulikuwa na usumbufu wakati wa utekelezaji wa mradi, hata hivyo alitoa rai kwa wakazi wa nje ya jiji  hilo kuendelea kuwa na uvumilivu kwa kuwa kazi inayoendelea kwa sasa ni ulazaji wa bomba la maji safi ili zoezi likamilike na waweze kupata huduma kikamilifu

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya AfDB akiwa Arusha ametembelea miundombinu ya mradi wa maji wa jiji la Arusha, likiwemo Tanki la Maji leje ujazo wa Lita milioni 10 katika eneo la Seed Farm, Ofisi ya Kanda ya Idara ya Maji eneo la Moshono na Pampu za kusukuma maji eneo la Kikwe.

Katika ziara yake aliambatana na Mshauri Mwandamizi wa masuala ya kiuchumi wa AfDB, Bw. Jonathan Nzayikorera pamoja, Kaimu Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dkt. Jacob Oduorn na Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia dawati la Benki hiyo, Bw. Said Nyenge.


Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Arusha (AUWASA), Mhandisi. Justine Rujomba (kushoto) akimuongoza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo ,anayesimamia baadhi ya nchi za Afrika katika Benki hiyo kutembelea  Tanki la maji la mradi wa maji wa jiji la Arusha (AUWASA) eneo la Themi. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi. Nadhifa Kemikimba. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo, akizungumza jambo na Mkandarasi wa Mradi wa Maji jiji la Arusha, Bw. Ma Ziheng, alipotembelea na kukagua mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 520 zilizotolewa kama mkopo nafuu na Benki hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi. Nadhifa Kemikimba (kulia) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo, anayesimamia nchi tisa katika Benki hiyoalipotembelea mradi wa maji jijini Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 520 zilizotolewa kama mkopo nafuu na Benki hiyo.
Pampu za kusukuma maji katika mradi wa Maji Arusha unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi bilioni 520 katika eneo la Kikwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo (mbele), akitembelea na kukagua mradi wa Ofisi ya Kanda ya Idara ya Maji, jijini Arusha eneo la Moshono.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi. Nadhifa Kemikimba (wa nne kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo (wa sita kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Maji, Wizara ya Fedha na Benki ya AfDB, baada ya kukamilika kwa ziara ya kutembelea mradi wa maji wa jiji la Arusha (AUWASA).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi. Nadhifa Kemikimba (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Kipronoh Cheptoo, anayesimamia baadhi ya nchi za Afrika katika Benki hiyowakiagana baada ya kutembelea mradi wa Maji Arusha.

(Picha na Peter Haule, WFM, Arusha)





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...