Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikao maalumu cha kupitia rasimu ya bajeti ya matengenezo na ujenzi wa barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA,) kwa Wilaya ya Ilala na kuwataka Madiwani kushiriki katika kupitisha bajeti hiyo kwa manufaa ya jamii, Leo jijini Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Massaka, Michuzi TV.)
Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Eng. Geofrey Mkinga akizungumza wakati wa kikao hicho naa kueleza kuwa katika uwajibikaji wataendelea kushirikiana na viongozi hao katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma muhimu hasa miundombinu ya barabara.




WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA,) imekutana na Madiwani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ilala na kupitia rasimu ya bajeti ya matengenezo ya barabara za Wilaya hiyo pamoja na kuona mahitaji halisi kupitia vipaumbele vilivyowasilishwa katika maeneo wanayohudumia ambapo miundombinu ya barabara inapita katika kila Kata.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha kupitia rasimu ya bajeti ya matengenezo na ujenzi wa barabara inayosimamiwa na TARURA kwa Wilaya ya Ilala iliyowakutanisha Madiwani wa Manispaa ya Ilala na Wakala hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija amesema kuwa ni muhimu Madiwani hao kushirikiana na TARURA katika kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu imara na kwa wakati na kueleza kuwa Wilaya ya Ilala ni kubwa na huko mbeleni wataangalia hatua za kuchukua hasa kwa Jimbo la Ukonga na hadi sasa vikao vya Chama vimeshakaa na kujadili suala hilo.

"Ni lazima jimbo la Ilala ligawanywe, ni kubwa sana....Lazima tupate Wilaya, Manispaa na Majimbo ikiwezekana hata mawili ni kubwa sana, itarahisisha kufikisha huduma zote kwa urahisi." Amesema.

Amesema suala la ugawaji wa Wilaya lipo wazi kwa kuwa wakati Wilaya nyingine zinagawanywa Ilala haikugawanywa, na hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokuwa Makamu wa Rais alifahamu hilo.

"Suala hili katika ngazi ya Chama limeshapita na Halmashauri inaendelea na uandishi wa andiko na Baraza hili lazima suala hili lipite, hivyo tushirikiane katika kufanikisha hili." Amesema.

Aidha amewataka Madiwani hao kupanga vyema bajeti hiyo kwa kuzingatia inagusa maeneo husika katika jamii.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Eng. Geofrey Mkinga amesema lengo na kukutana na viongozi hao ni kupitia rasimu ya bajeti ya Wakala hiyo kwa kuangalia namna ilivyogusa maeneo wanayoyahudumia kwa kuhakikisha barabara zinapitika kila Kata.

Amesema kuwa katika uwajibikaji na ushirikiano watapitia vipaumbele vyote vya Kata kwa kuona mahitaji halisi na yale ya kiutaalam.

Mkinga amesema Wakala hiyo inapata fedha kutoka Serikali kuu, Halmashauri na Wadau wa Maendeleo wakiwemo DMDP na kwa kuona umuhimu wa viongozi hao wamekutana na kuona kilichopo ni kipi na kipi wataongeza.

"Madiwani wana wajibu wa kuitengea Wakala fedha, tunawapitisha katika rasimu hii ili waone ni kiasi gani kilichotengwa na Serikali ili waweze kuongeza kupitia vikao vyao." Amesema.





Matukio mbalimbali wakati wa kikao hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...