Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAKATI kesho Machi 19,2022 Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza mwaka mmoja tangu achukue nafasi hiyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelezea   hatua kwa hatua mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kwenye nyanja mbalimbali ikiwa pamoja na   kuimarika kwa uchumi nchini

Ambapo katika kipindi hicho wamejionea kuwepo kwa mwenendo mzuri wa ukuaji chanya wa uchumi, ambao kutokana na taarifa za kitaalam, umechangiwa na kuwepo kwa ongezeko la uwekezaji, mathalani katika miradi ya kimkakati kwenye miundombinu  ya nishati ya umeme, maji, afya, elimu, ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege. Aidha, uzalishaji wa madini hususan ya dhahabu, makaa ya mawe na mazao ya kilimo ambao umeongezeka sana.

Akizungumza leo Machi 18,2022 wakati akielezea mwaka mmoja wa Rais Samia , Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema kumekuwa na ukuaji wa kiwango kikubwa katika sekta za madini na mawe (asilimia 10.9), habari na mawasiliano (asilimia 10.2), huduma za kijamii (asilimia 9.8), umeme (asilimia 9.7), na maji (asilimia 7.0).

Amesema ukuaji chanya wa uchumi umeleta matokeo ya wazi yanayoonekana, mathalani kuongezeka kwa mzunguko wa fedha (ukwasi) kwa wastani wa asilimia 9.3, kutoka asilimia 4.8 iliyokuwepo mwaka wa fedha wakati anakabidhiwa dhamana.

Ameongeza hiyo imesababishwa na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, msisitizo wa kuhakiki na kulipa malimbikizo ya madeni ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na hata wastaafu. Jambo lingine linaloonekana wazi kutokana na ukuaji chanya huo wa uchumi, ni kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi kutoka asilimia 3.1 hadi kufikia asilimia 10.

" Hili nalo limesababishwa na kuwepo kwa fursa mbalimbali katika shughuli za kiuchumi, ambazo tumeziona katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani.

"Kanuni za kawaida katika masuala ya ukuaji wa uchumi zinatuambia kuwa ongezeko hilo maana yake ni kwamba kuna shughuli nyingi zinafanyika katika sekta binafsi ambayo ni mojawapo ya injini muhimu katika kukuza ajira na hivyo kugusa maisha ya mtu mmoja mmoja kwenye ngazi ya kaya,"amesema.

Chongolo amesema kuwa pia kumekuwa na nafuu kubwa upande wa mikopo chechefu kwa mabenki yetu nchini, ambapo imepungua kutoka asilimia 9.3 hadi sasa ni asilimia 8.2. Matokeo haya yamesababishwa na kuboreshwa kwa fursa anuai, ushikirikishwaji wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo na ulipaji wa malimbikizo ya madeni baada ya uhakiki kufanyika, hasa kwa wakandarasi.

" Lingine ni kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Kimarekani 60 bilioni hadi kufikia Dola za Kimarekani 64 bilioni. Kwa mujibu wa BoT, akiba hii inatosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua nusu mwaka.

"Wanasema pia, ni zaidi ya lengo la nchi wanachama wa EAC la miezi walau 4.5 na miezi 6 kwa wanachama wa SADC. Aidha, katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imeweka ‘record’ ya kukusanya kiwango kikubwa cha mapato tangu kuanzishwa kwake, kwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 2.5, mwezi Disemba, mwaka jana."

 Mbali ya jambo hilo la kipekee, Chongolo amesema ndani ya kipindi hiki pia kumekuwa na ongezeko la mapato ya ndani kutoka shilingi trilioni 11.6 ya mwaka wa fedha wa 2020 – 2021, hadi kufikia shilingi trilioni 15.9, mwaka wa fedha 2021 – 2022, ikiwa ni sawa na asilimia 93.5 ya makadirio ya kukusanya trilioni 17.0.

Ambapo ongezeko hilo (shilingi trilioni 11.6-15.9) ni sawa na ongezeko la shilingi trilioni 2.1.  Kwa ujumla, kutokana na utashi mkubwa wa kisiasa wa Kiongozi Mkuu wa nchi katika kutekeleza Ilani ya Chama tawala na kwamba wameshuhudia kiwango kikubwa cha uboreshwaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara, mashauriano, uwazi, uwajibikaji na elimu kwa umma.

"Kwa mwaka huu mmoja yamekuwa yakienda sambamba na utekelezaji wa kasi kubwa wa miradi ya maendeleo inayohusisha ushiriki wa sekta binafsi, mfano hai ukiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii na Mapambano ya UVIKO-19 pamoja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2021 – 2022.

"Utashi huo pia umesaidia kuwepo kwa ongezeko la makusanyo ya kodi inayolipwa kwa hiari (imewezesha ujenzi wa madarasa elfu 15, vituo vya afya, maji n.k),"amesema.

Kuhusu huduma za kijamii amesema katika eneo hili, Sura ya Tatu ya Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, imeahidi kwa wananchi masuala kadhaa ili kuendelea kuimarisha na kupanua huduma za jamii, nchini; ikiwemo elimu, afya, maji na ustawi wa jamii.

Hivyo Chama hicho  kilielekeza Serikali, kupitia sera, mikakati na mipango mbalimbali, kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na fursa ya kupata huduma hizo kwa ubora, kwa kiwango cha kutosha na bila vikwazo. CCM kama chama kinachotawala, kinaelewa katika eneo hili ndiko taifa litafanikisha mapambano ya maadui wetu wakubwa, Ujinga, Malazi na Umaskini.

Katika eneo la elimu ,Chongolo amesema  ndani ya mwaka huu mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na mafanikio na mapinduzi makubwa. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, wanafunzi wa kidato cha kwanza wote wameingia shuleni kuanza masomo yao kwa siku moja bila kuwepo waliosubiria nyumbani kujiunga sekondari kwa chaguo la pili.

"Jambo ambalo kwa  miaka yote lilikuwa linasababishwa na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya (UPUNGUFU) miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, hasa vyumba vya madarasa na madawati. Hilo limewezekana baada ya kujengwa kwa madarasa 12,000, bila kusahau madarasa mengine 3,000 ya shule shikizi.

"Hiyo inafanya jumla ya madarasa 15,000 ambayo yalijengwa ndani ya miezi 3!Ndani ya mwaka huu mmoja kumekuwa na uimarishaji na uboreshaji mkubwa wa utoaji wa elimu katika maeneo yote yaliyoelekezwa katika Ilani ambayo ni elimumsingi, elimu ya sekondari, elimu ya ualimu, elimu ya ufundi na elimu ya juu.

"Tumeshuhudia namna ambavyo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa kuboresha utoaji wa elimu maalum na kuongeza nafasi za mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Aidha, kuna ujenzi wa shule zingine za sekondari mpya zipatazo 245 unaendelea, lengo likiwa ni kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Sekondari hususan kwa watoto wa kike katika kata ambazo hazina shule za sekondari ili kuwapunguzia watoto umbali wa kutembea sana,"amesema na kuongeza

"Hivyo kuimarisha ulinzi wao waendapo na watokapo shuleni. Pia Serikali imetekeleza vyema maelekezo ya Ilani kuhusu uboreshaji na upanuaji wa elimu ya ufundi, ambapo jumla ya vyuo vya ufundi stadi 25 vimejengwa katika wilaya na halmashauri za wilaya maeneo mbalimbali nchini, ujenzi wa vyuo vya VETA katika mikoa 4 ambayo hapo awali haikuwa navyo kabisa pamoja na uboreshwaji wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii (FDC).

"Kwenye elimu ya juu, Chama kilielekeza Serikali kuimarisha na kuboresha mfumo wa ugharamiaji wa elimu ya juu ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji na sifa stahiki wanapata fursa hiyo.

"Katika eneo hili pia namba za wanufaika na uwekezaji, hazidanganyi, zinasema zenyewe, kuanzia kwenye ongezeko la bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 464 hadi shilingi bilioni 570, ambazo limeenda sambamba na kuongezeka kwa wanufaika wa mkopo wa mwaka wa kwanza kutoka wanafunzi 55,287 mwaka 2020/21 hadi takribani 76,300 mwaka 2021/22.

"Hivyo kufanya jumla ya wanufaikaji wote pia kuongezeka kutoka wanafunzi 142,170 mwaka 2020/21 hadi wanufunzi 176,617 kwa mwaka 2021/22.Sote tunajua namna wanufaikaji wa mikopo hii walivyoshusha pumzi za ahueni ya kuondolewa mizigo mikubwa miwili iliyokuwa inalalamikiwa kuwaelemea

" kwanza ile tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mkopo na pili tozo ya adhabu ya asilimia 10 ya mkopo ambayo ilikuwa ikitozwa kwa wanaochelewa kurejesha mkopo ilikuwa amesema ikitozwa kwa wanaochelewa kurejesha mkopo.  Pia ni muhimu kuwakumbusha Watanzania kuwa Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya mwaka huu mmoja, imeendelea kutekeleza sera ya elimu bila malipo kwa wanafunzi wa elimumsingi nchini kote na kwamba hakuna dhamira ya kurudi nyuma katika hilo,"amesema Chongolo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...