SERIKALI wilayani Lushoto Mkaoni Tanga imeeleza kutoridhishwa kwake na utendaji wa Bodi za Jumuiya za Watumiaji wa Maji Vijijini hususan katika ukusanyaji wa malipo ya maji na urejeshaji wa fedha hizo kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya miradi ya maji.

Kufuatia hilo Mkuu wa Wilaya hiyo Kalisti Lazaro amesema ataanza kufanya ukaguzi wa bodi zote kujua kiasi gani kimekusanywa na kimetumikaje.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa vyombo vya watoa huduma za maji ngazi ya jamii, Mkuu huyo wa Wilaya amesema taarifa alizonazo ni kuwa kumekuwa na hali duni ya ukusanyaji wa mapato, matumizi na kuibuka kwa migogoro kwenye miradi ya maji.

“Inashangaza kuwa migogoro ipo katika sehemu ambazo miradi ya maji imejengwa na kuna Bodi za Jumuiya za Watumiaji maji. Sehemu ambazo hakuna maji hakuna migogoro,” amesema.

Amesema kuwa fedha hizo zilikuwa zinalengwa kurudishwa katika jamii ili kusaidia matengenezo ya miundombinu inayoharibika na kupanua eneo la usambazi kwa kutumia fedha hizo hizo.

“Tutafanya ukaguzi tuone fedha zilizokusanywa ni kiasi gani na zimetumikaje au kwa nini hazikusanywi. Tunachoona ni kuwa hazirudi kwa jamii,” amesema.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa mtindo wa ukusanyaji hauridhishi kwa sababu hakuna risiti maalum. “Kule Mgwashi kuna Bodi inakusanya malipo kwa kutumia risiti za nyumba ya wageni ya Mwenyekiti wa Bodi. Hii haikubaliki,” amesema

Alieleza kuwa malipo waliyokubaliana ni Sh 3,000 kwa mwezi na kueleza kuwa kuna sehemu ambazo hazina maji na wanalipa sh 3,000 hadi Sh 5,000 kwa siku kwa ajili ya maji hivyo haoni mantiki ya watu kutoona umuhimu wa kulipia huduma hiyo.

Alishauri Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuanzisha mfumo wa malipo ya kielektroniki ili kuepuka upotevu wa fedha za miradi hiyo.

Lazaro alidokeza sababu mojawapo ya watu kutolipa malipo ya maji inatokana na siasa ambapo baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa serikali kutumia nia zao za kisiasa wanawaahidi wananchi kuwa wao wakichaguliwa wataondoa malipo hayo.

“Miradi imejengwa kwa fedha nyingi za serikali, hivyo lazima wananchi wakubali kulipia huduma ili iwe endelevu,” amesema

Aliwaonya viongozi wa serikali kuacha kuwa sehemu ya migogoro kwa kuendekeza maslahi yao.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Upendo Lugongo alisema kuwa wataanzisha mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Alieleza kuwa kila wilaya itateuwa Bodi mbili ambazo zitatumia mfumo kwa majaribio na mategemeo yao ni kuwa ifikapo mwaka 2023 na 2024 bodi zote katika wilaya zote nchini zitatumia mfumo huo ili kukabiliana na upotevu wa fedha.

Pamoja na hilo, Meneja huyo amesema kuwa RUWASA imeanza kutoa vitabu vya risiti kwa ajili ya jumuiya za watumiaji wa maji na kuajiri wahasibu.

Juu ya ujenzi wa miradi ya maji amesema kuwa serikali ya Rais Samia imetoa Sh Bilioni 6.7 kwa ajili ujenzi wa miradi 13 ya maji mkoani Tanga kupitia fedha za UVIKO 19. Alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umefikia asilimia 30 hadi hivi sasa.

Naye Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Lushoto, Erwin Sizinga jumla ya vyanzo 12 kati ya vyanzo 48 ambavyo vimetambuliwa katika zoezi la utambuzi vimeshawekewa mabango ya katazo la kufanya shughuli yoyote ya kibinadamu.

Hata hivyo, Sizinga alieleza kuwa vynazo 20 vimevamiwa na wananchi. Alisema jambo linaloshangaza ni kuwa baadhi ya wavamizi wa vyanzo hivyo ni viongozi ambao wanalima katika vyanzo hivyo.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Diwani wa Kata ya Mayo, Hamidu Ramadhani Hamza (Kitambi) aliishukuru serikali kwa kuipatia kata hiyo mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Sh milioni 470 ambao alisema kuwa utaondoa shida ya maji kwa asilimia 75.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...