Na Said Mwishehe, Michuzi TV
VIONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo wamefanya ziara kukagua maeneo ya vivutio vya utalii wa majini na misitu uliopo ndani ya Wilaya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya Jokate Mwegelo amesema leo Machi 10,2022 walikuwa na ziara mahususi kujaribu kuibua utalii wa majini na msituni kwenye eneo lao la Temeke na miongoni mwa maeneo ambayo wametembelea ni Kijiji cha Wavuvi Kurasini ambako kuna utalii wa maji, fukwe nzuri na msitu wa mikoko.
"Tunatambua Temeke unapokuja kwenye utalii wa maji na misitu unaweza kujiuliza kweli linawezekana?Kwa hiyo tunasema inawezekana na utalii Temeke upo na katika kujiridhisha leo tupo na mtalamu wetu aliyefanya utafiti kwa takribani miaka 10 kwenye eneo la Dar es Salaam.
"Pamoja na mambo mengine amebaini kuna maeneo yakipangwa vizuri na kushirikisha wadau wakiwemo TFS tunaweza kuja na kitu kizuri cha kitalii na kikawa chanzo cha kuiingiza mapato serikali.Kwenye nchi nyingine kama Singapore,Instanbul na Uturufki wametumia maji kama sehemu ya utalii na sehemu ya kuingiza mapato ya serikali,"amesema Jokate.
Amefafanua katika Kijiji cha Wavuvi Kursani ni eneo ambalo linafaa kwa utalii na ndipo Mto Kizinga na Mzinga inakutana na kuingia baharini , eneo hili likipangwa vizuri litakuwa eneo nzuri la utalii. "Maji yapo na msitu wa miti ya mkoko upo.
" Unajua wenzetu huko nje hawana mambo mengi lakini wanatengeneza mambo yao na yanakuwa , kwa hiyo kutokea hapa Kurasini hadi Mtoni Kijiji tunaweza kufanya jambo kubwa na likaleta likaleta tafsiri mpya hasa katika Jiji letu la Dar es Salaam na Wilaya ya Temeke.
"Huu ni mwanzo na kwa sasa eneo hili la Kijiji cha Wavuvi ni la kawaida, hivyo tunataka watu walifahamu kwenye jicho la utalii.Temeke tunayo historia nzuri inayoanzia miaka mingi iliyopita, tutafanya kitu cha kihistoria ndani ya Wilaya ya Temeke na Dar es Salaam kwa ujumla."
Ameongeza wananchi wanatambua Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya utalii ameipa kipaumbele na filamu ya kuutangaza utalii wa Tanzania ya Royal Tour itakayozinduliwa Aprili 16 mwaka huu nchini Marekani.
"Kwa hiyo Rais ametuonesha kabisa yeye dhamira yake na moyo wake viko wapi kwenye utalii, kwa hiyo lazima nasi kwenye maeneo yetu tuuibue utalii kama sehemu ya kuunga mkono kwa vitendo maono ya Rais Samia katika sekta ya utalii.Katika eneo la Kijiji cha Wavuvi Kurasini wiki ijayo kuna jambo kubwa tutafanya Temeke."
Kwa upande wake Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Wilaya ya Temeke Francis Kiondo amesema TFS na Mkuu wa Wilaya wameamua kufanya ziara hiyo ziara katika maeneo hayo kwa kuzingatia uwepo wa mito ya mikoko.
"Wasimamizi na waangalizi wa mikoko hiyo ni sisi TFS, kwenye eneo la Kijiji cha Wavuvi Kurasini linavutia kwa kufanya utalii ukizingatia kuna msitu mzuri unaotokana na miti ya mikoko.Lakini tuko hapa kama sehemu ya kutekeleza maelekezo Waziri Mkuu ya kuangalia maeneo ya vivutio vya utalii katika mkoa wetu wa Dar es Salaam.
Wakati huo huo Jafari Jongo ambaye ni Mtafiti Huru wa mambo ya kuendeleza miji kwa kutumia maji, misitu na rasilimali mbalimbali zilizopo mjini amesema katika utafiti wake amebaini kuna fursa ambazo zinaambatana na maji na misitu katika Jiji la Dar es Salaam.
"Kwa kuanzia tumeona uanzie huku Temeke ambako kuko katikati kwani unaweza kwenda upande wa Kusini na kaskazini.Pia kuna mito inayoingia bahari na mito inapongilia kuna mikoko iliyotunzwa vuzuri , hivyo kufanya eneo hili kuvutia kwa utalii.
"Hapa Kijiji cha Wavuvi Kurasani ndioko Mto Mzinga na Kizinga inapoingilia Bahari ya Hindi lakini wote tunafahamu Dar es Salaam imebaba historia kubwa tangu enzi za ukoloni,"amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo(katikati) akiwa amemshika samaki aina ya Kaa baada ya kufanya ziara ya kutembelea Kijiji cha Wavuvi Kurasani ambako eneo hilo linatarajiwa kuwa kama eneo la utalii ndani ya Wilaya ya Temeke kutokana na uwepo wa fukwe nzuri na msitu wa miti ya mikoko.Wa kwanza kulia ni Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Wilaya ya Temeke Francis Kiondo.Wa pili kulia ni kiongozi wa wavuvi wa samaki kwenye kijiji hicho na wengine kwenye picha hiyo ni maofisa wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
Sehemu ya msitu wa mikoko uliopo kwenye Fukwe ya Bahari ya Hindi katika eneo la Kijiji cha Wavuvi Kurasini wilayani Temeke.
Mtafiti Huru wa mambo ya kuendeleza miji kwa kutumia maji, misitu na rasilimali mbalimbali zilizopo mjini Jafari Jongo(katikati)akielezea jambo wakati wa ziara hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari.
Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam akiangalia vijidudu vilivyopo kwenye fukwe ya Bahari ya Hindi akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yenye vivutio vya utalii.
Mtafiti Huru wa mambo ya kuendeleza miji kwa kutumia maji, misitu na rasilimali mbalimbali zilizopo mjini Jafari Jongo(katikati) akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo(kushoto) na Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Francis Kiondo(kulia) wakati wa ziara ya kukagua maeneo ya utalii ndani ya Wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Wavuvi Kurasini kuhusu mpango wa Wilaya hiyo kulifanya eneo hilo kuwa la utalii mbali ya kuendelea kwa shughuli za uvuvi wa samaki.Jafari Salehe Jongo ambaye ni Mtafiti Huru wa mambo ya kuendeleza miji kwa kutumia maji, misitu na rasilimali mbalimbali zilizopo mjini akielezea sababu za kufanya utafiti kwa ajili ya kubaini maeneo ya utalii unaotokana na majini na misitu maeneo ya mijini.
Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Francis Kiondo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kulinda na kuhifadhi misitu pamoja na miti ya mikoko ikiwemo iliyopo katika fukwe ya Bahari ya Hindi eneo la Kijiji cha Wavuvi Kurasini.
Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam akieleza jambo kuhusu mikakati ya wilaya hiyo katika kuibua maeneo yenye utalii kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya utali nchini .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...