Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIKA hatua ya kupambana na changamoto inayoendelea ya matumizi ya bidhaa za plastiki zinazotumika mara moja, serikali katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimehimizwa kutekeleza kikamilifu zuio la matumizi ya bidhaa za plastiki zitumikazo mara moja katika ukanda huo.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakati akitoa ripoti ya uchunguzi kuhusu biashara haramu ya mifuko ya plastiki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Lê Rocha, amesema uchafuzi wa mazingira utokanao na bidhaa za plastiki ni tatizo la kimataifa, linahitaji hatua za haraka kulikabili dunia nzima, hasa ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa plastiki unaendelea kuongezeka kadiri siku zinavyosonga.
"Kwa sasa, tunazalisha takriban tani milioni 381 kila mwaka. Mara tu vitu hivi vimetumiwa na kutupwa, 75% yao huishia katika mazingira yetu au kwenye madampo. Taka zinazobaki uteketezwa kwa moto, na hivyo kuongeza hatari kwa afya za watu, na kiasi kidogo hurejelezwa," Bi. Rocha alisema.
Ripoti ya uchunguzi iliandaliwa na Nipe Fagio kwa ushirikiano na Bio Vision Africa (BiVA Africa) ya Uganda, Global Initiative for Environment and Reconciliation (GER) ya nchini Rwanda, na Kituo cha Haki na Maendeleo ya Mazingira (CEJAD) nchini Kenya, ili kuchambua hali ya sasa katika nchi zote nne na kuelewa biashara na mtiririko mzima wa mifuko ya plastiki, ambayo imepigwa marufuku kabisa nchini Tanzania, Kenya na Rwanda lakini bado inapatikana sokoni na mitaani.
Rocha ameeleza kuwa kwa kupiga vita matumizi ya bidhaa za plastiki zinazotumika mara moja katika mfumo wa mifuko ya kubebea, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimechukua juhudi binafsi kuanzisha kanuni za kupiga marufuku utengenezaji, uingizaji/usafirishaji na utumiaji wa mifuko ya kubebea ya plastiki.
Rwanda ilianza juhudi zake mwaka 2008 na imekuwa na matokeo ya mafanikio zaidi ndani ya EAC. Kenya ilifuata mwaka wa 2017 na Tanzania mwaka wa 2019. Uganda imetangaza kupiga marufuku mifuko ya plastiki itumikayo mara moja mara kadhaa (2007, 2009, 2015, 2018 na 2021) lakini utekelezaji bado uko nyuma.
“Licha ya kupigwa marufuku kwa mifuko ya kubebea ya plastiki inayotumika mara moja, tafiti katika kila nchi za EAC zimeonyesha kuwa zuio hizo zimetoa nafasi za utoroshwaji wa mifuko hii ya plastiki kuvuka mipaka.
"Biashara haramu inalenga kuhudumia soko la walaji ambalo bado halijawekwa wazi juu ya njia mbadala, licha ya kadhaa kupatikana, zikiwemo za jadi za kiafrika," alibainisha.
Katika ripoti hiyo ya uchunguzi kulingana na tafiti za uchunguzi, hatua kadhaa zimependekezwa kuchukuliwa ili kukomesha biashara hiyo haramu na tatizo linaloongezeka la mifuko ya plastiki inayotumika mara moja ndani ya eneo la Afrika Mashariki (EAC).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...