Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema miongoni mwa mafanikio makubwa inayojivunia katika Kipindi cha Mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni Ujenzi wa Mifumo mbalimbali 14 inayotumika katika Usajili na Utambuzi wa watu ukilinganisha na Mifumo 11 iliyojengwa kabla ya kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya Sita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu Mafanikio ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa katika kipindi cha Mwaka Mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Msemaji wa NIDA Bw. Geofrey Tengeneza amesema mifumo hiyo 14 ni ongezeko la asilimia 127 na inafanya jumla ya mifumo iliyojengwa na NIDA mpaka sasa kuwa 25 jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa Mamlaka.
Amesema mifumo hiyo imejengwa na Watumishi wa NIDA ambao ni wataalamu wa masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kitendo ambacho kimesaidia Mamlaka kuondokana na utegemezi wa Mkandarasi na kuokoa fedha za Serikali.
“ Faida nyingine ni kuondokana na ukomo wa leseni ya matumi, Mamlaka kumiliki nakala halisi ya Programu za mfumo na kuweza kufanya maboresho ya mfumo pindi yanapohitajika” alisema Tengeneza. Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja kukusanya maduhuli ya Serikali ya shilingi bilioni 20.5 ikilinganishwa na maduhuli ya shilingi bilioni 17.5 zilizokusanywa kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani.
Akizungumzia mafanikio upande wa Watumishi Tengeneza amesema jumla ya Watumishi 485 wa Mamlaka wamepandishwa vyeo na kubalishwa kada huku jumla ya watumishi 69 wakihudhuria mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu. Aidha, Watumishi 22 wameajiriwa wameajiriwa katika Kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Msemaji huyo wa NIDA amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Serikali yote ya Awamu ya Sita kwa kuiwezesha NIDA kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa katika Kipindi hiki cha mwaka mmoja cha Serikali ya Awamu ya Sita na kusisitiza kuwa NIDA imejipanga kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho vyao haraka na kwa wakati..
Mkuu wa KItengo cha Habari na Mawasiliano ambaye pia ni msemaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Bw. Geofrey Tengeneza akionyesha kitambulisho cha Taifa kwa waandishi wa habari alipokuwa akisisitiza jambo katika mkutano na waandishi hao Makao makuu ya NIDA leo jijini Dar es salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...