Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa na Siku ya Misitu Duniani mwaka 2022 yatafanyika Wilayani Magu, Mkoani Mwanza yakiongozwa na kaulimbiu isemayo Mti wangu, Taifa langu, mazingira yangu, Kazi Iendelee.

Taarifa iliyotolewa Wizara ya Maliasili na Utalii leo jijini Dodoma imeeleza kuwa maadhimisho hayo ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ambayo hufanyika Aprili 1 ya kila mwaka sasa yatafanyika Machi 21, 2022 yakiwa yameunganishwa.

Maadhimisho hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania yakiwa yameongozwa na malengo makuu mawili ambayo ni kuwakumbusha na kuwahamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa upandaji na utunzaji wa miti kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa na huduma za misitu hapa nchini.

Pia yatajikita katika kukumbusha na kuhamasisha umma wa watanzania juu ya umuhimu wa kuendelea kutunza na kuhifadhi misitu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuhamasisha wananchi waendelee kupanda miti hasa katika kipindi hiki cha mvua, kuitunza, na kuihifadhi misitu iliyo katika maeneo yao kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Sekta ya Misitu ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira na kuongeza kuwa watanzania wanategemea nishati ya miti kwa zaidi ya asilimia 90.

Aidha, imeeleza kuwa misitu inatoa asilimia 45 ya mahitaji ya malighafi ya ujenzi, hulinda vyanzo vya maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Vile vile, misitu husaidia kunyonya hewa ukaa na hivyo kuchangia katika juhudi za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

Katika hatua nyingine tarifa hiyo imeeleza kuwa kwa ujumla maisha ya mwanadamu yanategemea misitu kuanzia kuzaliwa kwake hadi mwisho wa maisha yake. Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inapoteza eneo la misitu lenye ukubwa wa hekta 469,000 kwa mwaka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ukataji wa miti usio endelevu, mioto kichaa, na upanuzi wa mashamba.

Hivyo, ili kuziba pengo la miti na misitu inayopotea kila mwaka jamii inatakiwa kupanda miti ya kutosha, na kuhakikisha misitu inasimamiwa kiuendelevu.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...