Na Karama Kenyuko, Michuzi Tv

Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maji kuendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana kwa wananchi wote na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

Amesema upatikanaji wa maji nchini umefikia asilimia 72.3 vijijini na asilimia 86 mijini.Mahundi ameyasema hayo leo Machi 15, 2022 Dar es Salaam wakati ufunguzi wa kikao cha wadau cha Shirika la WaterAid lililowakutanisha wadau wa maji usafi ma Mazingira ili kushirikishana ujuzi ili kujenga maarifa yenye tija katika kuboresha utoaji huduma za maji nchini.

Ameseka, takwimu hizo zinaonyesha bado kuna kazi kubwa ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu hasa lengo namba sita la kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana kwa watu wote ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wake, Serikali inalenga kuweka mkazo katika utekelezaji wa miradi mikubwa yenye vyanzo vya maji vya uhakika ambavyo vitahudumia wananchi wengi na kwamba pia vitaongeza uwezo wa kuhifadhi vyanzo vya maji na kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Aidha, tunalenga kuongeza chachu ya maji machafu na usafi wa mazingira mijini na vijijini,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi  wa shirika la WaterAid nchini Anna Mzinga amesema shirika la WaterAid kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wamejitahidi kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji safi, vyoo bora na usafi wa mazingira kwa kila mtu popote pale.

Amesema kuna haja ya kuangalia namna ya kufikia mabadiliko ya kudumu mbali na uchimbaji wa visima vya maji, ufungaji wa mabomba ya maji, ujenzi wa vyoo na ufungaji wa vifaa vya usafi wa kibinafsi. 

"Tunaamini uwepo wa Shirika hili nchini utaendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na wananchi na wananchi ikiwemo wale wa Makundi maalumu ili kupata huduma za maji na usafi wa mazingira stahiki na zenye tija na endelevu", amesema Mzinga.

Ameongeza kuwa malengo mengine ni pamoja na kujielekeza katika utekelezaji wa miradi mikubwa yenye vyanzo vya maji vya uhakika na itakayohudumia idadi kubwa ya wananchi  na kuongeza nguvu katika utunzaji wa vyanzo vya maji na juhudi kubwa katika kukabiliana  na mabadiliko ya tabia nchi.

Nao wadau  wa sekta ya Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi (Wash) wamebainisha mambo  yatakayoboresha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na uwekezaji zaidi katika usimamizi wa maji, pamoja na kulinda vyanzo vya maji vilivyopo.

Aidha wamesisitiza kuangalia namna ya kusimamia matumizi ya maji na namna ya  kusambaza rasilimali zilizopo, huku wakitahadharisha kuwa juhudi zote zisiwekwe katika kuwekeza kwenye usafi wa mazingira bali kuweka mfumo ambao utawakwamua hasa katika ongezeko la wananchi ili uendane na ongezeko la mahitaji ya huduma ya maji.

Getrude Mapunda, Kiongozi wa Ujumbe kutoka Ofisi ya Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) (Human Team Lead) amesema mahitaji ya maji yamekuwa yakiongezeka kwa miaka mingi kufuatia uwekezaji zaidi katika nyumba za makazi, viwanda pamoja na shughuli nyingine za usafi.

"Pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya maji bado kuna umuhimu wakuwekeza zaidi katika sekta hiyo," alisema.

Naye, Mtaalamu wa Usimamizi wa Miradi (Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi), USAID, Francis Mtitu amesema nchi ina mfumo mzuri wa mijadala unaohitaji kupitia upya programu na kuandaa vipaumbele katika sekta hiyo.

"Nchi ina programu ya 2030 ambapo kila mtu kila mahali anapaswa kupata huduma ya maji," amesema.Aidha amesema kulikuwa na haja ya kufikiria upya vipaumbele kwa sababu milipuko kama vile kipindupindu inatuma ujumbe kwamba bado kuna changamoto kwenye upatikanaji wa huduma hio.

Sambamba na hayo, Mkutano huo ulitawaliwa na majadiliano mbalimbali ya umuhimu wa maji, vyoo bora na Shia binafsi kama chachu ya Maendeleo pamoja ujumuishaji wa huduma za maji na vyoo bora katika sekta ya umma kama vile shule  na vituo vya afya ili kuwepo uwiano wa kijinsia.

Naibu wa waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi akizungumza na wadau mbali mbali wa maji wakati akifungua kikao cha wadau wa Shirika la WaterAid ili kujadiliana na kushirikishana ujuzi wa kujenga maarifa yenye tija katika kuboresha utoaji huduma za maji nchini
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid Tanzania akizungumza na wadau mbali mbali wa maji wakati akifungua kikao cha wadau wa Shirika la WaterAid ili kujadiliana na kushirikishana ujuzi wa kujenga maarifa yenye tija katika kuboresha utoaji huduma za maji nchini


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...