Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuna mafanikio makubwa yamefanyika yakiwemo ya kuchukua hatua za kufanyia marekebisho ya Sheria , Kanuni na Sera kwenye sekta zilizopo kwenye Wizara hiyo ili ziandane na hali halisi,wakati na mahitaji.

Akizungumza wakati akitoa taarifa mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema katika kipindi hiki cha mwaka mmoja yameshuhudiwa mabadiliko makubwa kwenye sekta kadhaa zilizopo chini ya Wizara hii, mabadiliko haya yamegusa pamoja na maeneo mengine , uhuru wa wananchi kujieleza na uhuru wa habari kuongezeka nchini.

"Aidha uwekezaji kwenye sekta za habari, mawasiliano na teknolojia ya habari na mchango wa sekta hizi kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu umeongezeka na hivyo kuongeza pia ajira.Pia mabadiliko haya yamesababishwa na mabadiliko katika sheria na kanuni kadhaa zilizokuwa zinasimamia sekta hizi, marekebisho yaliyofanywa ni katika kipindi cha mwaka mmoja,"amesema Nape.

Ameyataja baadhi ya marekebisho hayo ni katika Sheria ya Mawasiliano ya kieletroniki na Posta 2010 ambapo marekebisho yamefanywa kwenye sheria ili kutoa unafuu kwa wananchi katika kupata huduma za mawasiliano na wawekezaji kuendelea kuwekeza.

"Marekebisho haya ni kuondoa leseni ya biashara ya simu za mkononi ili simu za mikononi zisambae kwa wingi kwa wananchi kuwawezesha kupata mawasiliano wakati leseni za mamlaka zingine zitaendelea kutolewa na mamlaka huska.Kuwapa wawekezaji wa huduma ya maudhui muda wa miaka miwili kujenga miundombinu husika badala ya mwaka mmoja tangu wanapopata leseni.

"Sheria ya Shirika la Posta ya 1993, ambapo marekebisho yalifanywa katika sheria ya posta ya mwaka 1993 kwa lengo la kuboresha utendaji wa Shirika na pia kulipa Shirika nguvu ya kisheria kufanya kazi za kidigitali.Pia Sheria ya ulinzi wa taarifa binafsim,"amesema.

Amefafanua katika eneo hilo kuna mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa lengo la kusaidia kuingia katika uchumi wa kidigitali yameandaliwa na yanawasilishwa katika ngazi mbalimbali kwa ridhaa."Kukamilika kwa sheria hii kutakuwa kichocheo cha uwekezaji katika biashara mbalimbali zinazotumia mitandao na mifumo ya kieletroniki katika ukusanyaji , uchakataji na ubadilishanaji wa taarifa binafsi nchini."

Kuhusu kanuni , Nape amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita kanuni za utangazaji kwa njia ya kidigitali za 2018 zimerekebishwa ili matangazo ya televisheni yawafikie wananchi wengi na kuvutia uwekezaji kwa vyombo vya utangazaji .

"Marekebisho hayo ni pamoja na kuruhusu watoa huduma wanaotoa maudhui ya bila malipo kwa wananchi kubebwa katika visambuzi vya kulipia kama vile DSTV na ZUKU.Kabla ya marekebisho haya televisheni hizi zilikuwa zikibebwa na watoa huduma wenye miundombinu ya ardhini tu hivyo kusababisha kutokuonekana kwenye visambuzi vya Setilaiti.

"Mabadiliko haya yameongeza wigo wa chaneli zaidi ya 14 kuonekana kwenye ving'amuzi vya setilaiti .Ili kulinda miundombinu ya ardhini kanuni hizi kwa sasa zinamlazimu mtoa huduma wa FTA kuhakikisha kuwa kwanza amejiunga kwa mtoa huduma wa miundombinu ya ardhini kama takwa la msingi na kukamilisha upelekaji wa huduma kwa kutumia miundombinu hiyo.

"Chaneli za kulipiwa kwa sasa zinaruhusiwa kutoa matangazo ya kulipiwa na kuwa na vipindi vinavofadhiliwa na wadau ili kuvutia uwekezaji kwa chaneli hizo na kukuza maudhui ya ndani na kukuza vipaji vya wasanii wa ndani,"amesema Nape.

Aidha amesema Kanuni za Leseni za 2018 nazo zimefanyiwa marekebisho kwa lengo la kuongeza uwekezaji katika eneo la mawasiliano ya kieletroniki.Badhi ya marekebisho hayo ni kupunguza ada za baadhi ya leseni ili kuvutia uwekezaji.

Pia kuhusisha Mamlaka ya Mawasiliano na Waziri mwenye dhamana na mawasiliano katika mchakato wa kuuzwa kwa kampuni ya mawasiliano kwa lengo la kutaka uhamishaji wa hisa ufanyiwe tathmini kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa.

Nape amesema Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za 2020 zimefanyiwa marekebisho kuboresha matumizi ya mtandao na hivyo kukuza fursa na vipaji.Marekebisho hayo ni pamoja na kuondoa leseni kwa watoa maudhui mbalimbali mfano mapishi, michezo,usanii ikiwemo muziki na filamu.

"Kwa marekebisho haya habari na matukio ya sasa ambayo hutolewa pia na vyombo vya habari vya kawaida ndio zitakazokatiwa leseni na pia kutakuwa na leseni kwa wakusanya habari mbalimbali wenye lengo la kuzitoa kwa watoa maudhui ya habari mtandaoni,"amefafanua.

Marekebisho mengine ni kuondoa zuio la matangazo ya kubahatisha inayofanyika katika mtandao yataendelea kusimamiwa na sheria na kanuni ya nchi ya kubahatisha , hivyo Serikali iliona kwamba hakuna haja ya kuwa a zuio katika kanuni hizo.

"Mengine ni kupunguzwa ada ya maombi ya leseni ya maudhui ya mtandaoni kutoka Sh.milioni moja hadi Sh.500,000.Kanuni za utangazaji katika redio na televisheni za 2018 kanuni hizi zimefanyiwa marekebisho kuvutia wawekezaji,'amesema.








 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...