Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge)Dk.Pindi Chana ametoa mwito kwa halmashauri zote nchini asilimia 10 ya mikopo iliyotengwa kwa ajili ya vijana na wanawake itolewe pia kwa watu ambao wameamua kuachana na utumiaji wa dawa za kulevya na sasa wanaendelea kupatiwa dawa za methadoni katika Kliniki za Waraibu kote nchini.

Atoa mwito huo leo Machi 16,2022 baada ya kutembelea Kliniki ya Waraibu wanaopata dawa za Methadoni katika Hospitali ya Mwananyamala mkoani Dar es Salaam akiambatana na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambapo amesema kuna kila sababu ya halmashauri kutoa kipaumbele kwa wananchi hao ambao wengi wao ni vijana na wameachana kutumia dawa za kulevya.

"Wakati tukiendelea kuadhimisha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani tumeshuhudia maeneo mengi yameguswa ,yameboreshwa na yamefanikiwa, miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vituo vingi vya kuwahudumia Waraibu wa dawa za kulevya vimefunguliwa maeneo mbalimbali na miongoni mwa vituo hivyo ni hiki cha Mwananyamala.

"Dawa hizi za Methadoni zinatolewa kwa watanzania pasipo malipo yoyote ili waweze kupona kwa haraka.Tunazo fursa mbalimbali za kuwaunganisha Waraibu na fursa za maendeleo, nitumie fursa hii kuutangazia umma kwamba kwenye halmashauri zote nchini tumetenga asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya kukopesha vijana asilimia nne, wanawake asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili,"amesema Dk.Pindi Chana.

Ameongeza pamoja na fursa nyingine za kuwaunganisha vijana na vyuo mbalimbali kama VETA, kupata mafuzo chini ya SIDO na sasa kuna vijana zaidi ya 200 wanaunganishwa na mafunzo ya ufundi stadi , hivyo wakati  umefika kuendelea kutumia fursa hizo za mikopo kwa vijana hao walioacha kutumia dawa za kulevya kwani wanao uwezo wa kufanya shughuli za ujasiriamali.

"Watu hawa wanaweza kufanya shughuli za usafi, kufyatua matofali, kufuga kuku na aina nyingine ya shughuli za kimaendeleo, katika halmashauri watalaamu wa kuwafundisha wapo na halmashauri zipo tayari, kwa hiyo  niombe na muhimu sana kutumia fursa zilizopo kuwawezesha watu hawa ili nao washiriki kwenye ujenzi wa maendeleo ya nchi yetu.Katika ziara hii ambayo nimefanya leo hapa kwenye Kliniki ya kutoa dawa ya Methadon kwa Waraibu wa dawa za kulevya nimieelezwa sababu nyingi zinazosababisha watu kujiingiza kwenye utumaji wa dawa hizi.

"Miongoni mwa sababu hizo watalaamu wanasema masuala ya ndoa kwani ndoa zinapoparaganyika yamkini vijana wanakosa malezi na hivyo wanakwenda kulelewa na ndugu,jamaa na marafiki, wakati mwingine katika maeneo hayo wanafanyiwa ukatili , wanapata changamoto na kukata tamaa, na hivyo kujingiza kwenye utumiaji dawa za kuleva.Nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wa dini waendelee kutusaidia ndoa zinazofungwa na ndoa zilizopo ziendelee kuimarika,"amesema Dk.Pindi Chana.

Pamoja na hayo amesisitiza Waraibu wanayo haki ya kujiunga kwenye vikundi ili nao wapate fursa ya kupata mikopo inayotolewa na halmashauri ambayo haina riba na hizo ni jitihada za Serikali yetu za kuwasadia wanawake na vijana."Hivyo fursa hizi zinatolewa kwa vikundi , ni muhimu Waraibu wakajiunga maana tunafahamu umoja ni nguvu na vijana wakiwa kwenye vikundi itakuwa rahisi kukopesheka.

"Na kwenye kliniki zote za kutoa dawa za Methadon kuna maofisa wa ustawi wa jamii , hivyo natoa mwito maofisa hawa waweke taratibu za kuwaunganisha vijana hao na maofisa wanaoratibu utoaji mikopo kwenye halmashauri na jambo hili lizingatiwe.Pia nitoe rai kwa waraibu kutoacha kutumia dawa za Methadoni ili waweze kupona, na wasikubali kurudi kwenye kutumia tena dawa."

Kwa upande wake Kamishna wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi amesema kwa ujumla kuna vituo vya kutoa dawa ya Methadon 15 na kati ya hivyo vituo vikubwa viko 11 na vidogo vinne ambavyo vipo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Tuna vituo vikubwa 11 katika Mkoa wa Dar es Salaam ambako viko vitatu(Muhimbili,Temeke na Mwanyamala), kituo kingine Mwanza, Mbeya, Dodoma,Tanga, Arusha na Pwani ambako kuna vituo viwili(Bagamoyo na Hospitali  ya Tumbi. Katika vituo hivyo vyote mpaka kufika Desemba mwaka jana vilikuwa vimesajili Waraibu wapatao 10,600 lakini wanaokunywa dawa mpaka sasa wanafika kati ya 7000 au 8000,"amesema Dk.Mfisi.

Kuhusu vituo vidogo vilivyopo Dar es Salaam amesema vinalenga kupunguza wingi wa watu kwenye vituo vikubwa, kutokana na idadi kubwa ya Waraibu wanaokwenda kupata dawa kila siku ambapo ametoa mfano Kituo cha Mwananyamala kwa siku wanahudumia watu 350."Watu ambao wamesajiliwa kwenye vituo hivyo vyote ni wale waliokuwa wanatumia dawa ya kulevya aina ya Heroine tu."

Awali Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dk.Zavel Benela amesema kwa sasa Kliniki ya Methadon Mwanyamala inajumla ya wateja 1,350 ambao wanapata dawa kila siku lakini tangu kliniki hiyo ilipoanzishwa mwaka 2011 wameshahumia watu zaidi ya 3000 na wengine wamepona na wanaendelea na maisha yao.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu( Sera, Uratibu na Bunge) Dk.Pindi Chana(katikati) akizungumza leo Machi 16,2022 baada ya kufanya ziara ya katika Kliniki ya kutoa dawa ya Methadone kwa waraibu wa dawa za kulevya iliyopo Hospital ya Mwananyamala mkoani Dar es Salaam Kulia ni Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dk.Zavela Benela na kushoto ni Kamishna wa Uchunguzi na Sayansi Jinai wa Mamlaka ya  Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevy Betha Mamuya
Kamishna wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dk  Peter Mfisi( wa kwanza kulia) akifafanua jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge Dk Pindi Chana(katikati)aliyoifanya Hospitali ya Mwananyamala katika Kliniki ya kutoa dawa za Methadone kwa waraibu wa dawa za kulevya
Mmoja ya watoa huduma kwa Waraibu wa dawa za kulevya katika Kliniki ya kutoa dawa za Methadone katika Hospitali ya Mwananyamala akizungumza na Waandishi wa habari
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge Dk.Pindi Chana akipata maelezo katika Kliniki ya kutoa dawa za Methadone kwa waraibu wa dawa hizo alipotenbeke Kliniki iliyopo Hospitali ya Mwananyamala

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge Dk.Pindi Chana(kulia) akifafanua jambo kwa maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya alipotembelea Kliniki ya kutoa Dawa za Methadone kwa Waraibu wa dawa hizo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...