Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kilimanjaro
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Kilimanjaro umesema unatambua umuhimu wa ziara zinazofanywa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania Bara Kanali mstaafu Abdulrhaman Kinana.
Hayo yamesemwa na Katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro Jonathan Mabiyo alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya Chama hicho kwa Makamu Mwenyekiti huyo ambaye ameendelea na ziara yake ya mkoani hapa.
“Makamu Mwenyekiti wa Chama chetu tunakukaribisha katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro, tunatambua umuhimu wa ujio wako ambao utakwenda kuhamasisha shughuli za Chama na serikali katika kuwatumikia wananchi wa mkoa huu.
“Tunakumbuka ziara zako ambazo ulizifanya siku za nyuma ilipokuwa Katibu Mkuu wetu, ziara zile na maelekezo yako ambayo uliyatoa zilileta mafanikio makubwa, maelekezo yako yalisadia kufunguliwa kwa soko Kuu ambalo lilifungwa kwa muda mrefu.
“Tunaendelea kuamini hekima na busara zako ziara hii itaamsha ari katika mkoa wetu na tunaamini CCM Tanzania iko salama chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, tunakuahidi tuko pamoja na tutaendelea kujenga Chama imara kwa kuisimamia vizuri Serikali kutekeleza Ilani ya CCM,”amesema.
Kuhusu hali ya kisiasa Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro amesema imeendelea kuimarika lakini hiyo haitafanya wabwete kwani wenzao nao wanaendelea kufanya siasa za chini kwa chini.”Uchaguzi uliopita katika nafasi ya wabunge tulishinda majimbo yote tisa.Pia kwenye madiwani nako tulishinda viti vingi.
“Kwa ujumla mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa ndani ya Chama, hivyo tumejipanga kuhakikisha tunapata viongozi wazuri , wanaokubalika na wenye uwezo wa kukivusha chama katika uchaguzi mkuu mwaka 2025.Tumejipanga kuwadhibiti wale wote wanaotaka kutumia uchaguzi wa ndani kupanga safu zao.
“Katika uchaguzi huu wa Chama zoezi la utoaji fomu kwa ngazi ya mashina na matawi mchakato umekamilika na kwa upande wa uchaguzi ngazi ya matawi nako tumekwenda vizuri, tukuahidi kusimamia vema uchaguzi ili kupata viongozi waadilifu na wanaokubalika,”amesema.
Aidha amesema wanaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluh Hassan kwa kutekeleza Ilani ya Chama hicho kwa kasi zaidi.
Meza kuu ikijumuika pamoja na Wana CCM
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...