*Mkuu wa Mkoa wa Mbeya awataka waajiri wa sekta binafsi kufuata sheria kwa kuwasilisha michango ya wafanya kazi kwa wakati
NA MWANDISHI WETU, MBEYA
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Zuberi Homera amewataka baadhi ya waajiri wa sekta binafsi kusimamia Sheria na misingi ya ajira kwa kuwasilisha michango ya wafanya kazi wao kwa wakati kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kuuwezesha Mfuko kulipa madai mbalimbali ya wanachama wanapopatwa na majanga au wanapostaafu.
Akifungua mafunzo kwa waajiri wa sekta binafsi yaliyoandaliwa na Mfuko wa NSSF mkoani Mbeya, Mhe. Homera pia aliwaagiza waajiri hao kujiandikisha katika Mfuko na kuhakikisha wanachama wote wanaandikishwa na kuwasilisha michango kwa wakati.
“Naomba waajiri wote wenye malimbikizo ya michango kulipa michango yao na taarifa hiyo mnipatie ili niweze kuchukua hatua kwa waajiri ambao hawapeleki michango ya wafanya kazi wao kwa wakati,” alisema.
Mhe. Homera aliupongeza Mfuko wa NSSF kwa kufikia malengo hasa katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Naye, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Mhandisi Fredy Kipamila, aliwataka waajiri wa sekta binafsi kutimiza wajibu wao kwa kuwasilisha katika Mfuko michango ya wafanya kazi wao ili watakapopata majanga waweze kulipwa stahiki zao.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Deus Jandwa alisema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya mifumo kwa waajiri na wanachama.
‘‘Mfuko umeanzisha mifumo ambayo tunataka waajiri waifahamu, wajiunge ili waweze kujihudumia popote walipo, wanaweza kuandikisha wanachama, kuwasilisha michango bila ya kufika katika ofisi za NSSF,’’ alisema.
Mafunzo hayo ilihudhuriwa na baadhi ya waajiri wa sekta binafsi 103 kutoka taasisi mbalimbali za Mkoa wa Mbeya.
Akifunga mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Rashid Chuwachuwa, aliushukuru Mfuko wa NSSF kwa namna unavyotekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo ulipaji wa mafao kwa wastaafu wanaokidhi vigezo.
*****************************
Baadhi ya waajiri wa sekta binafsi Mkoa wa Mbeya wakifuatilia semina iliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyokuwa na lengo la kuwajengea uelewa juu ya maboresho yaliyofanywa na NSSF kuhusu mifumo mbalimbali ya TEHAMA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...