BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema dirisha la uombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 linatarajia kufunguliwa kabla ya tarehe 15 Julai, 2022.

 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumatano Julai 6, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa HESLB (pichani), Abdul-Razaq Badru ilisema HESLB inakamilisha taratibu za uombaji mikopo kwa mwaka 2022/2023 na dirisha litafunguliwa katika kipindi cha siku 10 zijazo.

 

“Taarifa hii inatolewa kufuatia maombi mengi ya taarifa ya ufafanuzi kutoka kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka 2022 na matokeo yao kutangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), jana, Jumanne Julai 5, 2022.” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru.

 

Badru amesema kwa sasa waombaji mikopo watarajiwa wanatakiwa kuwa watulivu na kuanza maandalizi ya awali ya kuandaa nyaraka muhimu kama vyeti vyao vya kuzaliwa au vyeti vya vifo vya wazazi wao vilivyohakikiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Wakala wa Usajili wa Matukio Muhimu Zanzibar (ZCSRA).

 

Kuhusu sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa mwaka 2022/2023, Badru amesema maelezo yatapatikana katika ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2022/2023’ utakaoanza kupatikana katika tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz kuanzia Julai 15, 2022.

HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika.

 

 

 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...