Na Karama Kenyunko Michuzi TV
JAJI Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amewaasa watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke kinachojishughulisha na masuala ya familia kutunza siri za wateja wao pindi wanapofika mahakamani hapo kwa sababu mbali mbali.
Amesema kutokana na uhalisia wa kituo hicho, wadaawa wengi wakifika hapo wanazungumzia mambo yao ha ndani hivyo amewataka watumishi hao kuwa na vifua vigumu vinavyohifadhi siri.
Jaji Profesa Juma ameyasema hayo leo Julai 20, 2022 alipokuwa akizungumza na watumishi wa kituo hicho, kilichoko Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake kituoni hapo iliyolenga kujifunza na kuangalia namna ya utoaji wa haki katika kuelekea mahakama ya mtandao.
"⁸Mnaposhughulika na kesi za mirathi, kesi za Talaka na watoto mnagusa mambo mengine ambayo ni siri sana binafsi za watu, ndio maana mara nyingine kwenye maamuzi yetu huwa tunaficha majina ya wahusika hususani kama ni mtoto...., tunapoingia katika mahakama ya kidigitali tutunze zile siri kwa sababu wadaawa wanapokuja mbele yenu wakati mwingine wanazungumzia mambo ambayo kwa kawaida huwa hawapendi yatoke, mambo ya ndani kabisa, hivyo kuelekea mfumo huu wa kidigitali tunaweza kuwa vyanzo vya hizi siri. Amesema Jaji Profesa Juma.
“Pale unapoona neno usiposema neno hutakutwa na neno amesema Jaji Juma
Pia amewashauri watumishi wanaotoa huduma katika kituo hicho wakiwemo mahakimu na majaji kujifunza na kujiongeza katika maeneo ambayo siyo ya kisheria ikiwemo saikolojia, sosholojia, ili kumfahamu binadamu, kwa kuwa wengi wanaofika kupata huduma huwa na msongo wa mawazo.
Aidha Profesa Juma amewataka watumishi hao, wakati wanaposhughulikia kesi hizo, ambazo nyakati zingine hugusa maeneo mengine ya kitaalamu na siyo sheria kama vile mikopo, mikataba, hisa na mabenki wasisite kutafuta wataalamu kabla ya kutoa uamuzi ili uamuzi mtakaotoa uwe umekamilika na wenye kuzingatia Idara zote.
Akizungjmzia, usimamizi wa mirathi, Profesa Juma amesema sehemu hiyo ina fedha nyingi, ambapo kumekuwepo na ujanja ujanja hivyo ili mahakama hiyo isiwe sehemu yake, inapaswa kuwasimamia.
Alibainisha kuwa malalamiko aliyoyasikia maeneo mengi ni ya wasimamizi wa mirathi, ambao huchukua mali kama zao badala ya kuwa za warathi, na wengine wakiwa hawakamilishi hesabu ndani ya muda.
“Sisi wengine tutakuja kujifunza kutoka kwenu namna mnavyowadhibiti wasimamizi wa mirathi, ikiwemo kukamilisha hesabu na kuhakikisha migao yote imefanywa kwa mujibu wa sheria,”
Naye Jaji Mfawidhi wa kituo hicho, Ilvin Mugeta akiwasilisha taarifa za utendaji kazi wa kituo amesema, kuanzia tarehe 27 Agosti, 2021 hadi kufikia jana tarehe 19 Julai, 2022, mashauri 4,687 yamesajiliwa katika ngazi zote za Mahakama na asilimia 68 yamesikilizwa na kuamuliwa.
Amesema kati ya mashauri yote yaliyosajiliwa, asilimia 62, yaani mashauri 2,911 ni ya mirathi ambapo asilimia 82 ya mashauri hayo tayari wasimamizi wa mirathi na watekeleza wosia wameteuliwa na kuthibitishwa, mtawalia.
“Hadi kufikia Julai 19, 2022 jumla ya mashauri 424 yalihusisha malipo ya fedha na 15,413,629,678/63 ziliwekwa katika akaunti ya mirathi ya Mahakama. Asilimia 91 ya kiasi hiki kimelipwa kwa wanufaika kupitia mashauri 371. Bakaa iliyopo kwenye akaunti hadi tarehe ya ripoti hii ni Tshs 1,321,830,690/22 ambayo ipo katika hatua za malipo,” amesema.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani kulia akiteta jambo na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma akipanda mti, katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi kituoni hapo leo Julai 20 2022 mkoani Dar es Salaam.Sehemu ya watumishi katika kituo hicho (juu na chini) wakishangilia hotuba ya Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma (hayupo katika picha).Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma (katikati aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya viongozi kutoka Makao Makuu ya Mahakama. Wengine waliokaa ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani (wa pili kushoto), Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Ilvin Mugeta (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayehudumu katika Kituo hicho, Dkt. Modesta Opiyo (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...