Dkt.Noel Lwoga ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa akiweka sawa majarida mbalimbali yanayoelezea majukumu ya Makumbusho hiyo pamoja na Utalii wa malikale na makumbusho za Taifa alipokuwa kwenye banda lao.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MKURUGENZI Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt.Noel Lwoga ameelezea hatua kwa hatua sababu za wao kushiriki katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimaita yanayoendelea viwanja vya Sabasaba mkoani Dar es Salaam na miongoni mwa sababu hizo ni kuendelea kuelimisha jamii kuhusu kazi zinazofanywa na makumbusho hiyo.
Akizungumza leo akiwa katika banda la Makumbusho ya Taifa lililomo kwenye ukumbi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ndani ya maonesho hayo , Dkt.Lwoga amefafanua makumbusho ya taifa ni taasisi yenye kufanya utafiti za kielimu inayoshughulika na kukusanya urithi wa kihistoria , lakini kuhifahi na kuelimisha jamii.
“Mwaka huu 2022 tumeshiriki Maonesho ya Sabasaba kwa makusudio matatu , kwanza ni kwa lengo la kuendelea kuelimisha jamii kuhusu kazi ya Makumbusho ya Taifa, na hasa juu ya urithi wa taifa husika na ndio maana kwenye banda letu tuna vionesho mbalimbali zama damu au mazalia ya binadamu wa kale, lakini tuna maonesho ya nyumba za asili, maonesho ya kihistoria.
“Pili tunashiriki ili kuutangaza urithi huo kwa jamii, sisi kama Makumbusho ya Taifa kwenye mkakati wa kutangaza urithi wa taifa tumejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo kushiriki maonesho ya kitaifa kama haya ya Sabasaba, kwa hiyo kwetu sisi ni fursa ya kutangaza urithi huo kwa jamii na kuwaalika washiriki kutembela maonesho ya mali kale ili kuendelea kujifunza historia yao, kujifunza uzalendo lakini kuielewa wa nchi yao katika masuala ya mali kale.
“Suala la tatu ni kutangaza fursa za Makumbusho ya Taifa kwenye eneo la malikale inazitoa hasa katika kuendeleza uchumi wa taifa, fursa huduma za kitalii na fursa za kiuekezaji ili wadau waelewe na tuweze kufungua fursa za mali kale na maeneo yetu ya utalii katika nyanja nzima ya uwekezaji katika sekta ya utalii,”amesema Dkt.Lwoga wakati anaelezea sababu za wao kushiriki maonesho hayo.
Aidha amesema Makumbusho ya Taifa kwa ujumla wake ni taasisi inayosimamia vituo vya makumbusho takriban saba, ambapo vituo viwili viko Dar es Salaam, vituo viwili Arusha , kituo kimoja Butiama na vituo vingine viwili viko Songea mkoani Ruvuma.
“Ukiacha maeneo haya ya makumbusho tuna maeneo ya malikale zaidi ya 91 ikiwemo Mji Mmkongwe wa Mikindani, Mji wa Kigamboni , maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam , maeneo kadhaa ya Tanga , Kitandaguro Lindi na maeneo kadhaa nchini, sasa maeneo ya fursa yamegawanyika katika maeneo mawili ya malikale na makumbusho.
“Kwenye makumbusho zetu tunatoa fursa za maduka ya zawadi kuhakikisha wananchi mbalimbali wanawekeza kwenye kuuza bidhaa za kitamaduni, hivyo basi kutumia fursa hii, na uzuri makumbusho zetu ziko kwenye miji hapa na tunazungumzia Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam, tmakumbusho ya Azimio la Arusha, Makumbusho ya Maji maji katika Mji wa Songea, sasa haya maeneo ukiweka maduka ya bidhaa za kitamaduni utafanya biashara.
“Lakini biashara nyingine ni migahawa ya kitalii katika maeneo hayo. Makumbusho ya taifa kwa sasa inapata wageni takribani 400,000 kwa ujumla wake kwa hiyo ukifungua mgahawa unapata wateja ambao wanahitaji kupata chakula cha asili na maeneo ya kufurahi.
“Kwa hiyo tunawakaribisha wananchi kuwekeza katika migahawa, vile vile tuna maeneo ya kuweka studio za kitamaduni lakini ATM za biashara kwani wageni wakifika katika maeneo yetu wanahitaji kufanya miamala ya kifedha .Pia tunayo maeneo ya kupiga picha filamu na video , ukiacha maeneo haya ya makumbusho tuna maeneo ya malikale kama nilivyosema tuna Mji Mkongwe wa Mikindani , mji huo uko baharini , uko Pwani na hivi karubini tumeweka mazingira wezeshi kama gati kwa ajili ya bahari ile, kwa hiyo kuna fursa katika uwekezaji katika utalii wa boti, tunakaribisha wawekezaji kuja katika mji mkongwe wa Mikindani,”amesema.
Ameongeza katika mji wa Kigamboni wananchi wanaweza kuwekeza katika misafara ya boti za kitalii, pia kuna maeneo ya malazi kama Kitendaguru Lindi mjini , mji ya Mikindani na maeneo ya Kigamboni na hata maeneo kadhaa ya Tanga yaliyoko baharini yanahitaji huduma za malazi.“Huduma hiyo inaweza kuwa hoteli kupitia majengo ya magofu ambayo tunayasimamia , majengo ya kihistoria ambapo ukiweka hoteli inakuwa na thamani kuliko majengo ya kisasa, lakini huduma ya malazi ya kambi kwa ajili ya watafiti mbalimbali,”amesema Dk.Luwoga.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt.Noel Lwoga (kulia) akifafanua jambo kwa Mwandishi Ally Thabiti aliyetaka kufahamu ni kwa namna gani Makumbusho hiyo imeweke miundombinu rafiki kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum wanaokwenda katika maeneo ya Makumbusho ya Taifa na vivutio vyake.
Mmoja wa maofisa wa Makumbusho ya Taifa (kulia) akiendelea kutoa ufafanuzi kuhusu majukumu ya Makumbusho hiyo kwa wananchi waliofika katika banda lao ambalo lipo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya Sabasaba mkoani Dar es Salaam.
Mhifadhi wa mambo ya kale katika Makumbusho ya Taifa Rahel Kisusi akielezea jambo kwa waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya Sabasaba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...