Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Lindi, mara baada ya kuwasili bandarini hapo kwa ziara ya kikazi Mkoani humo.

 

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amempa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wiki mbili kuhakikisha analeta watumishi wa kudumu katika Bandari ya Lindi ili kurahisisiha usafirishaji wa abiria na mizigo katika Bandari hiyo.

Akizungumza mkoani Lindi mara baada ya kutembelea Bandari hiyo Naibu Waziri Mwakibete pamoja na maelekezo hayo amesisitiza umuhimu wa Bandari kufanya vikao na wadau wote ili kuwa na mkakati wa pamoja wa namna ya kuifanya bandari hiyo kurejea katika ufanisi kama awali.

“Bandari hii naelezwa ilikuwa inahudumia mzigo mkubwa sana miaka ya nyuma lakini kwa sasa inaonekana imepoa sana na hakuna mzigo unaosafirishwa hapa wakati gharama za mzigo kwa kusafirisha kwenye maji ni rahisi kuliko kuupitisha barabarani", amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameeleza kuwa kwa sasa Serikali imeamua kupunguza tozo kwa asilimia 30 kwa mizigo inayosafirishwa kupitia Bandari za Mtwara na Lindi ili kuruhusu mzigo mkubwa kupita bandarini ili kuongeza ufanisi kwa utendaji wa Bandari hizo.

Naye, Mbunge wa Lindi Mjini, Hamida Abdallah, ameiomba Serikali kuiboresha Bandari hiyo kwani hapo awali ilikuwa ni eneo ambalo lilitoa ajira na kukuza pato la mkoa kwa usafirishaji mkubwa wa bidhaa za mbalimbali ikiwemo mbao na saruji.

“Mhe Naibu Waziri Bandari hii ilikuwa inasafirisha mizigo na ilifika mahala mpaka meli za Zanzibar zilikuwa zinakuja hapa kuchukua mizigo lakini kwa sasa tunapokea meli ndogondogo ambazo zinabeba mzigo mdogo na kufanya ufanisi usionekane", amefafanua Mhe. Hamida.

Awali akitoa taarifa ya Bandari, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdilah Salim, amesema miongoni mwa juhudi zinazofanywa na TPA kwa sasa ni kuendelea na kufanya upembuzi yakinifu lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya kibandari, vyombo vya kuhudumia shehena na meli ili kuruhusu bandari kufanya kazi wakati wote.

Bandari ya Lindi kwa mwaka wa fedha  2021/2022 imehudumia shehena ya tani zaidi ya 8,574 ambazo zinajumuisha mizigo mbalimbali ikiwemo mazao ya miti pamoja na bidhaa nyingine.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa Uongozi na watumishi Mamlaka ya Usimamizi wa bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Lindi mara baada ya kutembelea bandari hiyo mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mbunge wa Lindi Mjini, Hamida Abdallah.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akifurahia jambo na Uongozi wa Mkoa wa Lindi, Watumishi wa Mzani wa Mingoyo na dereva wakati  alipotembelea mzani huo Mkoani Lindi. Kushoto ni Mbunge wa Lindi Mjini Hamida Abdallah.
Muonekano wa gati lililopo katika bandari ya Lindi. Bandari hiyo kwa sasa chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inafanyiwa usanifu ili kufanyiwa maboresho na kuruhusu mzigo mkubwa zaidi kuhudumiwa.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete (kushoto) akimsikiliza Msimamizi wa Mzani wa Mingoyo, Esther Mushi, akimweleza kuhusu utendaji wa mzani huo wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mzani huo mkoani Lindi.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...