Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete kushoto,akitoa maelekezo kwa Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi kuhusiana na upanuzi wa kiwanja cha ndege Songea ambacho kimefanyiwa upanuzi kwa lengo la kuruhusu ndege kubwa kutoa katika kiwanja hicho.
NAIBU Waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete,amekagua mradi wa
ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Songea ambacho Serikali
imetoa Sh.bilioni 37.09 kutekeleza mradi huo.
Akizungumza mara baada ya kukagua ukarabati huo,Naibu Waziri Mwakibete
amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo
zinakwenda kuufungua mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla katika
usafiri wa anga.
Naibu Waziri Mwakibete ameridhika na kazi iliyofanywa na wakala wa
Barabara nchini(Tanroads)mkoa wa Ruvuma katika utekelezaji wa mradi huo
muhimu kiuchumi.
Hata hivyo,ameiagiza Tanroads kumsimamia mkandarasi kampuni ya Chico ili
kukamilisha kazi zilizobaki ikiwamo kufunga taa ili kuruhusu ndege
kutua na kuruka saa 24 badala ya kutumika mchana tu.
Naibu Waziri Mwakibete,ameishauri Tanroads na mamlaka ya viwanja vya
ndege(TAA)kuangalia namna ya kuongeza ukubwa wa uwanja huo kwa kuanza
mchakato wa kuwalipa fidia baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo
jirani,hasa upande wa Barabara kuu ya Songea-Mbinga ili kuwezesha ndege
kubwa zaidi kama AirBus na Dream liner katika kiwanja hicho.
“nawaomba wenzetu wa Tanroads na mamlaka ya viwanja vya ndege nchini,kwa
sasa ndege pekee inayoweza kutua katika uwanja huu ambayo ni kubwa
zaidi ni aina ya Bombadier tu,lakini ndege kama AirBus au Dreamliner
haziwezi kutua,kwa hiyo ni vyema kuanza mchakato wa kuongeza ukubwa wa
kiwanja chetu”alisema.
Mwakibete alieleza kuwa,mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza
kwa uzalishaji wa mazao ya chakula,uchimbaji wa makaa ya mawe na kuna
ziwa maarufu la nyasa ambapo lengo kubwa la Serikali ya awamu ya sita
kiwanja hicho kitatumika kusafirisha bidhaa ikiwamo makaa ya mawe.
Aidha,amewataka wakazi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani ya nyanda za
juu kusini,kuhakikisha wanatumia fursa ya upanuzi wa kiwanja hicho
kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kusafiri kwa ajili ya shughuli
mbalimbali za kibiashara na utalii.
Alisema,upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege Songea kunatoa fursa
za uwekezaji na utalii kwa sababu mkoa wa Ruvuma una vivutio vingi na
vya kila aina ikiwamo Ziwa Nyasa,Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na maeneo
mengi yenye utalii wa kihistoria na kiutamaduni.
Kwa upande wake Meneja wa wakala wa Barabara Tanroads mkoa wa Ruvuma
Mhandisi Ephatar Mlavi alisema, kazi ya upanuzi na ukarabati wa kiwanja
cha ndege Songea ilianza 2019 ulitakiwa kukamilika mwezi Disemba 2020.
Hata hivyo alisema,kutokana na kuongezeka kwa baadhi ya kazi
walilazimika kuongeza muda hadi tarehe 30 JUNI 2022 na muda wa matazamio
ni miezi kumi na mbili.
Alisema, gharama ya mradi ni Sh.bilioni 37.9 na hadi sasa mkandarasi
ameshalipwa shilingi bilioni 21.381 na fedha nyingine ambazo ni
Sh.bilioni 2.1 zinaendelea kushughulikiwa ili ziweze kulipwa na kazi
hiyo imefikia asilimia 90.
Alisema,kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa sehemu ya kutua na
kurukia ndege,upanuzi wa sehemu ya usalama wa uwanja kila upande,sehemu
ya maegesho ya ndege,kuchora mistari na kujenga mifereji yenye urefu wa
mita 6000.
Aidha alitaja kazi nyingine zilizofanywa na mkandarasi ni kujenga uzio
kuzunguka uwanja,kujenga barabara mbili ndani na nje ya uzio kuzunguka
uwanja,kufunga taa za kuongozea ndege ambazo ujenzi wake utakamilika
mwishoni mwa mwezi Julai ili kuruhusu ndege kuruka na kutua usiku.
Kwa mujibu wa Mlavi kazi nyingine ni zilizofanyika ni ujenzi wa jengo la
kuongozea ndege(Control Tower) ambalo umefikia asilimia 75,ununuzi wa
gari la zimamoto lenye uwezo wa kubeba maji lita 10,000 ambalo
limeshaagizwa,kujenga jengo la kupokea na kusambaza umeme.
Mlavi alisema,mkandrasi kwa sasa anaendelea kukamilisha kazi ndogo ndogo
zilizobaki ambazo zitafanywa katika muda wa matazamio na atakabidhi
kazi zote Mwezi Agosti mwaka huu.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Songea Dkt Frederick
Sagamiko,ameishukuru Serikali kwa kazi nzuri ya upanuzi wa kiwanja cha
ndege Songea na kuhaidi kwamba wananchi wa Songea na mkoa wa Ruvuma kwa
ujumla watahakikisha wanatumia kiwanja hicho kupanua shughuli za
kiuchumi ikiwamo kufanya biashara na kusafirisha bidhaa mbalimbali
kwenda mikoa mingine na nje ya nchi.
Dkt Sagamiko ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea alisema,katika
mkoa wa Ruvuma kuna fursa nyingi ambazo kupitia kiwanja hicho watabadili
mtazamo katika shughuli za kilimo kwa kuanza kulima maua na bustani za
mboga mboga ambazo mahitaji yake ni makubwa hapa nchini na nje ya nchi.
Kwa upande wake kaimu meneja wa kiwanja cha Ndege Songea Jafari Mbayo
alisema,mara baada ya serikali kufanya ukarabati na upanuzi wa kiwanja
hicho idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa ndege imeongezeka hadi
kufikia 72.
Alisema, hali hiyo inaonesha kuwa kuna abiria wengi wanaosafiri kwa
kutumia kiwanja cha ndege cha Songea kutokana na ukweli kwamba usafiri
wa ndege ni wa haraka na salama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...