Janeth Raphael - Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za mashujaa ambayo kitaifa yatafanyika Jijini Dodoma.
Akizungumza katika viwanja vya mashujaa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema maandalizi yanaenda vizuri na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa imeridhishwa na maandalizi hayo.
"Sherehe za mashujaa kitaifa kwa mwaka 2022 zinafanyika Dodoma na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa mgeni rasmi kwenye siku ya mashujaa kitaifa tarehe 25/7 ambayo itakuwa siku ya jumatatu na shughuli zitaanza asubuhi mapema,matarajio yetu nikwamba wananchi wote wa mkoa wa Dodoma watajumuika na Rais kwenye siku ya Sherehe ya mashujaa kitaifa.
Mheshimiwa Rais amewapa heshima kubwa sana wakazi wa mkoa wa Dodoma kwani ipo mikoa mingi yenye minara ya mashujaa lakini imempendeza Mheshimiwa Rais shughuli hii kitaifa iweze kuwafanyika hapa,"amesema Mtaka.
Aidha amesema kuwa wako tayari kuhakikisha eneo hilo la mashujaa linakuwa hai kama ambavyo maeneo kama hayo kwenye maeneo mengine duniani yanavyotumika.
"Kwetu sisi mnara wa kumbukumbu za mashujaa wetu ndani ya Jiji la Dodoma tutautunza lakini tunatamani liwe ni eneo ambalo litatembelewa,liwe ni eneo ambalo litakuwa ni moja ya alama za mkoa wa Dodoma na ni moja ya eneo la kuvutia watu kwasababu ni eneo lipo kwenye eneo zuri na linaonekana na linafikika kwaiyo Ofisi ya mkoa,ofisi ya Jiji la Dodoma na Ofisi ya maadhimisho tutakutana pamoja tukubaliane namna gani eneo hili litatunzwa vizuri," amesema Mtaka.
Aidha amesema kuwa tarehe 24 usiku saa sita kamili uongozi wa mkoa na viongozi mbalimbali watakuwa katika viwanja hivyo kwaajili la zoezi la kuuwasha mwenge kuamkia siku ya mashujaa kitaifa na siku ya tarehe 25 ambayo ndio siku ya mashujaa usiku saa sita kamili mwenge huo utazimwa katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa maadhimisho Taifa Ofisi ya Waziri Mkuu Bathlomeo Jungu amesema kuwa maandalizi yanakwenda vizuri Kutokana na kuwa eneo hilo halikuwa zuri lilikuwa limechoka na kazi ya ukarabati wamewakabidhi SumaJkt ili kuhakikisha eneo hilo linakarabatiwa na kuwa katika hali nzuri.
Siku ya mashujaa kitaifa itafanyika tarehe 25 mwezi huu katika viwanja vya mashujaa Jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa Antony Mtaka akikagua maandalizi katika uwanja wa mashujaa Jijini Dodoma kuelekea siku ya mashujaa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...